Mhagama aagiza vibali vya kazi kwa raia wa kigeni kuharakishwa

0

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama amewaagiza watendaji katika wizara hiyo kukamilisha mfumo wa kieletroniki wa utoaji wa vibali vya kazi kwa raia wa kigeni haraka ili kuondokana na changamoto zilizopo katika utoaji wa vibali hivyo.

Mhagama alitoa kauli hiyo wakati alipokuwa akizungumza na Menejimenti ya wizara yake na taasisi zilizopo chini ya ofisi hiyo.

Kikao hicho kilikuwa ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Rais John Magufuli alipokuwa anafungua Bunge la 12 na pia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 – 2025.

Mhagama alisema usimikaji wa mfumo wa kielektroniki wa kushughulikia vibali vya kazi utasaidia kuimarisha ushughulikiaji wa maombi ya vibali vya wageni.

Aidha, wakati akiapisha baraza jipya la mawaziri,Disemba 9 mwaka huu, Rais Magufuli alisema bado kuna wageni wanapata vibali vya kazi hata kwa nafasi ambazo zinaweza kushikwa na Watanzania na kutaka mawaziri wapya wa wizara hiyo kulishughulikia hilo.

“Idara ya Kazi kwa mujibu wa sheria inajukumu la kuratibu ajira za wageni nchini, hivyo kutokana na changamoto zilizopo katika utoaji wa vibali hivyo hivyo suluhisho pekee la kutoa vibali kwa wakati ni kuharakisha mfumo wa kielektroniki ambao utashughulikia vibali vya kazi,” alisema.

Alisema mfumo huo wa kielektroniki ambao unaandaliwa utakuwa na manufaa ikiwemo kuongeza ufanisi katika kushughulikia maombi ya vibali vya kazi na kuokoa muda wa kushughulikia maombi ya vibali hivyo.

Aidha, Mhagama alisisitiza suala la uboreshaji wa sheria za kazi ili ziendane na mfumo huo unaoandaliwa.

“Hakikisheni mnafanya mapitio sheria za kazi kwa kushirikisha wadau ambao wanahusika katika uandaaji wa mfumo huo ili kuboresha utoaji wa huduma katika kushughulikia maombi ya vibali,”alisema.

Aidha, Mhagama aliagiza kuwepo na utaratibu wa kushughulikia malalamiko mbalimbali yanayohusu vibali vya kazi ambayo yanatolewa na wadau.

 

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here