Mgunda: Tumeadhibiwa kwa makosa yetu

0

NA MWANDISHI WETU

BAADA ya kulazimishwa kugawana pointi mojamoja na wapinzani wake Gwambina kwenye sare ya kufungana bao 1-1 Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, Kocha Mkuu wa Coastal Union, Juma Mgunda amesema kuwa waliadhibiwa kutokana na makosa ambayo waliyafanya.

Kwenye mchezo huo wa ligi uliochezwa juzi, Oktoba 24, Coastal Union ilianza kufunga kupitia kwa Yusuph Soka dakika ya pili bao hilo lilipinduliwa na Meshack Abraham kinara wa utupiaji ndani ya Gwambina akiwa na mabao manne dakika ya 36.

Mgunda, alisema hayo mara baada ya mchezo huo kukamilika, kuwa wachezaji walishindwa kulinda ushindi wao na kufanya makosa ambayo pia yalisababisha wawape penalti Gwambina, Yusuph Dunia dakika ya 15 alikosa penalti hiyo wakati timu yake bado ikiwa nyuma kwa bao 1-0.

Mgunda alisema:-“Tumefanya makosa wenyewe na ndio maana tumeadhibiwa, tulianza kushinda mapema tukashindwa kulinda ushindi wetu hivyo tumepata ambacho tulistahili kupata hapa nyumbani.

“Nampongeza mwalimu mwenzangu kwa kuwa tumesoma naye hivyo  tulikuwa tunapambana huku tunajuana sio mbaya, makosa ambayo wachezaji wameyafanya ninayachukua na tunakwenda kufanyia kazi.”

Coastal Union kwenye msimamo ipo nafasi ya 13 ikiwa na pointi tisa baada ya kucheza mechi nane ndani ya Ligi Kuu Bara wa msimu wa 2020/21.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here