Mgombea Ubunge CCM Tabora Mjini aahidi ajira kwa vijana

0
Mgombea Ubunge Jimbo la Tabora Mjini kwa tiketi ya CCM, Emmanuel Mwakasaka

NA BENNY KINGSON,TABORA

MGOMBEA Ubunge Jimbo la Tabora Mjini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi CCM Emmanuel Adamson Mwakasaka ameahidi kutatua kero ya ajira kwa vijana wa jimbo hilo kwa kutengeneza fursa za kujiajiri na kuwawezesha mitaji kwa kutumia fedha zake binafsi.

Mwakasaka ametoa ahadi hiyo juzi katika mkutano wa kampeni zake uliofanyika katika Kata ya Kanyenye halmashauri ya manispaa Tabora na kuhudhuriwa na umati mkubwa wa wananchi.

Alisema kuwa katika bunge lililopita akiwa mbunge wa jimbo hilo aliwezesha vikundi zaidi ya 20 vya vijana na akinamama kuanzisha miradi mbalimbali ya ujasiriamali jambo lililowawezesha kujiongezea kipato.

Aliahidi kuwa kama atapewa miaka mitano tena atapanua wigo wa ajira kwa vijana kwa kuwawezesha mitaji ili kuanzisha miradi ya ujasiriamali katika maeneo yao, alibainisha kuwa yuko tayari kutumia sehemu ya fedha zake ili kuwainua zaidi.

Mbali na uwezeshaji huo pia aliahidi kusimamia ipasavyo asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri ya Manispaa hiyo ili kuhakikisha yanavinufaisha vikundi vyote vya vijana, akinamama na walemavu.

Aidha Mwakasaka alisisitiza kuwa kama atachaguliwa tena kuwa Mbunge wa jimbo hilo atalipa kipaumbele kikubwa suala la sanaa na michezo ili kuinua vipaji vya vijana wa kike na kiume kwa kuwa sanaa na michezo ni ajira nzuri pia.

“Ndugu zangu naomba mnichague kuwa Mbunge wenu ili niweze kusimamaia ipasavyo maendeleo yenu na kutekeleza kwa vitendo ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi na ninawaahidi nitaendelea kujitolea kumamia maendeleo yenu” alisema.

Aliwataka kuchagua wagombea wa CCM kuanzia ngazi ya Rais, wabunge na madiwani ili kuharakisha maendeleo yao na kubainisha kuwa kama watachagua wagombea wa upinzani watajicheleweshea maendeleo.

Alitaja baadhi ya kero ambazo zilikuwa kikwazo kikubwa kwa wananchi kuwa ni suala la vitambulisho ambapo wajasiriamali wadogo, aendesha bodaboda  na bajaji walikuwa wakisumbuliwa lakini sasa wako huru kuuza bidhaa popote huku suala jingine likiwa ni kutozwa gharama kubwa akinamama wanapojifungua.

Mwakasaka aliongeza kuwa amechimba visima katika kata mbalimbali ili kutatua kero ya maji kwa wananchi, hivyo akabainisha kuwa jimbo la Tabora mjini sio la majaribio, wapinzani watarudisha nyuma juhudi za maendeleo zilizofanywa CCM.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here