Mfumuko wa bei wabakia asilimia 3.1

0

NA DOTTO KWILASA, DODOMA

OFISI ya Taifa ya Takwimu (NBS) imesema Mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwaka unaoishia mwezi Oktoba,2020 umebaki kuwa asilimia 3.1 kama ilivyokuwa kwa mwaka ulioishia mwezi Septemba,2020.

Hali hiyo inamaanisha kuwa ,kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Oktoba,2020 imebaki kuwa sawa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia mwezi Septemba,2020.

Hayo yamebainishwa jana jijini hapa na Kaimu Mkurugenzi wa Sensa ya watu na Takwimu za jamii Ruth Minja wakati akiongea na vyombo vya habari  juu ya  taarifa ya Mfumuko wa bei ya Taifa unaopima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi nchini.

Kaimu Mkurugenzi huyo alisema,Mfumuko wa bei unaoishia mwezi Oktoba,2020 kuwa sawa na Mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Septemba,2020 umechangiwa na kupungua na kuongezeka kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula na zisizo za vyakula kwa kipindi kilichoishia mwezi Oktoba,2020  zikilinganishwa na bei za Oktoba,2019.

“Baadhi ya bidhaa za vyakula zilizopungua kwa mwezi Oktoba,2020 zikilinganishwa na bei za mwezi Oktoba 2019 ni Pamoja na mchele kwa asilimia 4.2,mahindi kwa asilimia 12.4 na unga wa mahindi kwa asilimia 3.2,”alifafanua na kuongeza;

Bidhaa nyingine za vyakula  ni pamoja na unga wa ngano kwa asilimia 0.9,unga wa mtama kwa asilimia 0.8,unga wa muhogo kwa asilimia 1.4,mihogo mibichi kwa asilimia 2.5,viazi vitamu kwa asilimia 5.4 na ndizi za kupika kwa asilimia 6.3,”alisema Minja.

Licha ya hayo Minja alizungumzia bidhaa zisizo za vyakula zilizoongezeka bei kwa mwezi Oktoba,2020 zikilinganishwa na bei za mwezi Oktoba,2019 ni mavazi kwa asilimia 2.2,gesi ya kupikia kwa asilimia 6.5,mkaa kwa asilimia 8.8,ukarabati wa vifaa vya usafiri Kama magari kwa asilimia 8.3 huku samani ikiwa asilimia 1.4.

Mbali na hayo alieleza kuwa mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwezi Oktoba,2020 umebaki kuwa asilimia 3.4 Kama ilivyokuwa kwa mwaka ulioishia mwezi Septemba,2020.

Katika hatua nyingine Minja alieleza hali ya Mfumuko wa bei kwa nchi za Afrika mashariki kwa mwaka ulioishia mwezi Oktoba,2020 .

Alieleza kuwa,nchini Kenya Mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Oktoba,2020 umeongezeka hadi kufikia asilimia 4.48 kutoka asilimia 4.20 kwa mwaka ulioishia mwezi Septemba,2020.

“Kwa upande wa Uganda Mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Oktoba,2020 umebaki kuwa asilimia 4.5 Kama ilivyokuwa kwa mwaka ulioishia mwezi Septemba,2020,”alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here