Mfumo wa vocha za simu kama LUKU waja

0

NA DOTTO KWILASA, DODOMA

SERIKALI ipo katika Mchakato wa kuweka sera ya kuhakikisha makampuni ya simu  yanakuwa na mfumo wa uuzaji wa  vocha kama ilivyo kwenye mfumo wa uuzaji wa LUKU kwenye Umeme  ili kuondoa malalamiko ya wananchi kuibiwa vifurushi vyao na makampuni hayo.

Waziri wa  Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt.Faustine Ndungulile amebainisha hayo  jana jijini Dodoma  wakati akifanya mahojiano kufuatia wananchi kutoka maeneo  mbalimbali nchini kutoa malalamiko kwa kampuni za simu juu ya vifurushi ama bando walizojiunga  kuisha mapema ikilinganishwa na kiasi cha fedha walizotumia kujiunga.

Waziri huyo alisema,Malalamiko  yamekuwa mengi kutoka kwa wananchi kutokana na vifurushi kuisha kabla ya wakati  ikilinganishwa na fedha walizotumia kujiunga .

“Hivyo sisi kama serikali tumeamua kuchukua hatua hii ili wananchi wanufaike na mawasiliano ya  simu ambapo kuna haja sasa kuwa na mfumo wa vifurushi  kama ilivyo kwenye LUKU za Umeme “alisema.

Aidha,Dkt.Ndugulile alisema tayari ameshatoa maagizo kwa mamlaka ya Mawasiliano Tanzania [TCRA]kulifanyia Uchunguzi kwa Muda wa miezi mitatu pamoja na kuwa na mpango wa kupeleka malalamiko Wizarani kila mwezi.

“Tumeagiza TCRA kwenda kulifanyia uchunguzi  suala hili kubainisha nini changamoto lakini pili waje na mapendekezo kwa serikali na tuone namna ya kuyafanyia uchunguzi na maagizo hayo tumetoa ndani ya miezi mitatu” alisema.

Hata hivyo, Dkt. Ndugulile amebainisha kuwa hadi sasa zaidi ya simu kadi milioni 50 zimesajiliwa ,huku watanzania milioni 27 wanatumia internet na Watanzania milioni 29 wakitumia miamala ya fedha kwa njia ya Simu.

“Mhe. Rais alivyoanzisha hii wizara mpya alikuwa na makusudi yake ,moja ni kuongeza wigo wa Matumizi ya TEHAMA kwa manufaa ya Watanzania,hivi tunavyoongea  hadi sasa zaidi ya simu kadi milioni 50 zimesajiliwa ,huku watanzania milioni 27 wanatumia internet na Watanzania milioni 29 wakitumia miamala ya fedha kwa njia ya Simu” amesema.

Kutokana na hayo baadhi ya wananchi  jijini Dodoma waipongeza Serikali kufikia uamuzi huo na kusema kuwa suala la kuishiwa virufurushi kabla ya matumizi  limekuwa changamoto kubwa katika maisha yao .

“Tunaipongeza serikali  kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari  kwa kuanza kufuatilia malalamiko yetu ya muda Mrefu,” alisema

Danson Mwaluko miongoni mwa Wananchi waliopata fursa ya kuzungumza na Gazeti hili .

Licha ya hayo  alisema jambo hilo limekuwa ni kero kubwa kwani hurudisha nyuma uchumi.

“Kwa kweli siku hizi changamoto mno ukijiunga bando la Tsh.1000 ndani ya Dk 15 au 7 linakata tunashindwa tufanyaje”alisema Danson.

Tatizo la Wananchi kulalamika vifurushi kukata mapema katika simu zao limekuwa la nchi nzima ambapo serikali ya awamu ya tano imejipanga kutatua malalamiko hayo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here