Mfumo mpya kuizalishia mabilioni ya fedha Yanga

0

NA MWANDISHI WETU

KLABU ya Yanga imelichukulia kwa umakini mkubwa suala la mfumo mpya wa mabadiliko ikishirikiana na La Liga, na inaelezwa mambo yakikamilika, Yanga itakuwa inajiendesha kisasa, ikizalisha mabilioni ya fedha kwenye uwekezaji.

 Tayari semina ya mchakato wa mabadiliko imeanza kwa viongozi wa kamati ya utendaji ya timu hiyo tangu.

Hiyo ni siku chache tangu mshauri wa timu hiyo, Senzo Mazingisa akabidhiwe rasimu ya mfumo wa mabadilio na mwenyekiti wa timu hiyo, Dk Mshindo Msolla aliyoipokea kutoka Kampuni ya La Liga ya nchini Hispania.

 Yanga ilikabidhiwa rasimu na Makamu wa Mashindano na Usajili wa Yanga ambaye ni Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM, Injinia Hersi Said waliopewa jukumu la kusimamia mchakato huo wa mabadiliko.

Viongozi hao walikutana na kufanya kikao chake kwenye ofisi mpya ya GSM iliyopo Posta jijini Dar es Salaam ambapo waliongozwa na mwenyekiti wao, Dk Msolla.

Kwa mujibu wa mmoja wa mabosi wakubwa ndani ya Yanga, semina hiyo imeandaliwa maalum kwa ajili ya kuwajengea ufahamu viongozi juu ya ripoti ya mabadiliko kabla ya kwenda kwa wanachama wa klabu hiyo.

Yanga inataka kila mwanachama awe na uelewa mkubwa juu ya Yanga SC ya mabilioni inakuja mabadiliko hayo kabla ya kuyaingia.

Semina hiyo ilisimamiwa na Hersi ambaye kampuni yake inasimamia mchakato wa mabadiliko kwa asilimia 100 baada ya kupewa jukumu hilo na uongozi wa klabu hiyo.

Akizungumzia hilo, Makamu Mwenyekiti wa timu hiyo, Frederick Mwakalebela amesema: “Ni kweli semina ilifanyika kwa viongozi kabla ya kwenda kwa wanachama.

“Kikubwa tunataka kuona mfumo huo unakamilika kwa haraka ambao utakuwa wa uwazi ili kila mwanachama afahamu umiliki wa timu. Elimu itaendelea kutolewa kwa wadau wote ili kuhakikisha kila Mwanayanga anakuwa na ufahamu wa mfumo huo mpya kabla ya wanachama wa Yanga kupitisha mapendekezo hayo yaliyotolewa na La Liga.”

Katika mfumo huo, Yanga inatarajiwa kujiendesha kisasa kama klabu za La Liga, huku ikiwekeza vitega uchumi katika mtaji mkubwa wa wanachama ilionao.

Timu hiyo inatarajiwa kujiendesha kama kampuni huku ikichukulia soka kama biashara na kuingiza fedha nyingi. Pia itajenga viwanja vya kisasa Kigamboni, pamoja na gym, hosteli, mabwawa ya kuogelea na kadhalika.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here