Messi: Nataka kucheza soka Marekani

0

BARCELONA, HISPANIA

NAHODHA wa Barcelona Lionel Messi amesema kwamba anatumai ataelekea kuendeleza soka yake Marekani wakati kandarasi yake itakapokamilika mwezi Juni.

Mshambuliaji huyo wa Argentina mwenye umri wa miaka 33 anaweza kuanza mazungumzo na klabu za ughaibuni kuanzia Januari.

Uvumi kuhusu hatma yake ya siku zijazo umekuwa ukiendelea tangu alipowasilisha ombi la kutaka kuondoka katika klabu ya Barcelona mwezi Agosti.

”Sijui nitafanya nini bado” , Messi aliambia runinga ya Uhispania La Sexta.

”Nitasubiri hadi msimu utakapokamilika”.

”Ningependelea kucheza Marekani na kuona hali ya maisha ilivyo na jinsi ligi hiyo ilivyo kabla ya kurudi Barcelona kwa wadhfa fulani”.

”Kwa sasa kitu muhimu ni kuendelea kuichezea Barcelona na kumaliza msimu huu katika nafasi nzuri , kuangazia kushinda mataji na kutoathiriwa na vitu vingine”.

Barcelona ambayo haikushinda taji lolote msimu uliopita , wako katika nafasi ya tano katika ligi ya La Liga baada ya kuanza vibaya zaidi katika kampeni ya kushinda taji la ligi baada ya kipindi cha miaka 33.

Tangu alipojiunga na klabu hiyo akiwa na umri wa miaka 13, Messi amekuwa mfungaji bora wa mabao katika klabu hiyo , mbali na kushinda mataji 10 ya ligi ya La Liga, kombe la klabu bingwa Ulaya mara nne na kushinda mara sita taji la Ballon d’Or linalokabidhiwa kwa mchezaji bora duniani.

Ombi lake la kutaka kuondoka Barcelona lililozua utata lilitokana na tofauti kati yake na rais wa klabu hiyo Josep Maria Bartomeu, ambaye alijiuzulu mwezi Oktoba.

Messi alielezea hatua ya Bartomeu kujiuzulu kama ‘janga’.

”Ni wakati mgumu kwa klabu hii , na kwa kila mtu lakini wale walio ndani ya klabu hii wanajua kwamba iko katika hali ngumu , mambo ni mabaya na mambo yatakuwa magumu kuirejesha klabu pale ilipokuwa” , aliongezea.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here