Mawakala wa kura za Urais waapishwa,ACT Wazalendo na Ada Tadea vikikosa uwakilishi

0

Na Mwandishi Wetu 

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imewaapisha mawakala wa vyama vya siasa 13 watakaoshuhuhudia uhesabuji wa kura za urais, huku vyama vya Ada Tadea na ACT wazalendo havikuwa na  mawakala.

Mkurugenzi wa tume hiyo, Wilson Mahera amesema hayo leo, Oktoba 27, 2020 wakati akiwaapisha mawakala  hao.

Mahera amesema vyama ambavyo vimepeleka mawakala a ambao wameapishwa ni CCM, SAU, Chauma, AAFP, ADC, Chadema, CUF, Demokrasia Makini, DP, NCCR Mageuzi, NRA, UPDP na UMD

Amesema mawakala wa chama cha Ada Tadea wamechelewa kufika kwa ajili ya kuapishwa, lakini wakifika wataapishwa na kwa upande wa ACT Wazalendo wamedai hawana mawakala.

“Wasaidizi wangu waliwasiliana na naibu katibu mkuu wa ACT Wazalendo amewaeleza kuwa hawana mawakala wa urais,” amesema.

Amewataka mawakala hao kuhakikisha wanakuwepo kwenye chumba cha ujumuishaji wa kura za urais na wanafuata kanuni na taratibu kwa mujibu wa sheria.

Pia mawakala hao wametakiwa kuzingatia katiba ya nchi na wajibu wa kusaini nyaraka za matokeo ya urais.

“Kazi ya mawakala ni kushughulikia uhesabu wa kura wa rais na kulinda maslahi ya mgombea kuhakikisha kanuni, sheria na taratibu zinafuatwa,” amesema.

Naye wakili wa Serikali Mkuu, Rose Chilongozi amesema kanuni ya uchaguzi chini ya kanuni ya 50 kanuni ndogo ya 4 ya kanuni za uchaguzi wa rais na mbunge, tafsiri ya kiapo jukumu la kutunza siri, ukivujisha utashtakiwa kwa kosa la jinai chini ya sheria ya usalama wa Taifa kwa sababu nyaraka inayopokea matokeo ya uchaguzi ni ya siri, hivyo ukivujisha utachukuliwa hatua.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here