Matulanga rasmi Meya jiji la Dar

0
Diwani wa Kata ya Tabata (CCM), Omary Matulanga akila kiapo cha kuwa Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam, katika ukumbi wa Karimjee jana.

Na Bethsheba Wambura, Dar es Salaam 

Diwani wa Kata ya Tabata (CCM), Omary Matulanga ameapishwa rasmi kuwa Mstahiki Meya wa jiji la Dar es Salaam akiwa ni Meya wa 18 tangu mwaka 1949.

Matulanga alichaguliwa kuwa Meya katika Uchaguzi uliofanyika Disemba 16, 2020 kwa kupata kura 140 za ndiyo na hakukuwa na kura za hapana.

Akizungumza jana mara baada ya kila kiapo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi, Sokoine Drive, Anifa Mwingira, katika hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Karimjee Matulanga alisema Baraza atakaloliongoza litafanya kazi kwa kufuata taratibu na sheria.

“Nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kutuwezesha kufika siku hii na kukamilisha mchakato wa kuunda jiji letu la Dar es Salaam lakini pia kwa kuniwezesha mimi binafsi kuteuliwa kuwa Meya wa jiji la Dar. Pili nikishukuru chama changu cha CCM  chini ya Mwenyekiti wetu Rais MagufuliJP kwa kuniamini kuwa Meya na kuongoza jiji hili.

“Baada ya kuapa sasa tutakuwa na kikao na hiki kitakuwa kikao chetu cha kwanza ambacho kina dhamana kubwa ya kujadili namna ya kulisimamia jiji letu.  Nawaomba tumtangulize Mungu katika dhamana hii tuliyopewa Ili tutende haki.

“Jiji letu hili mnajua kabisa ni jiji  la kibiashara na ni lazma tuliendeleze mbali na hayo kuna miradi mbalimbali ambayo tunaletewa na Rais wetu hivyo ni wajibu Wetu kuitunza na kuisimamia miradi hiyo, alisema Matulanga na kuongeza kuwa;

“Niwaahidi tu kuwa Baraza la Halmashauri ya jiji nitakaloongoza mimi litafata taratibu zote za kusimamia miradi na tutafanya kazi sana.”

Aidha pia Matulanga alisema wameunda Kamati tano ambazo zitasaidia katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo na kijamii.

Akizitaja Kamati hizo Matulanga alisema; “ziko Kamati tano ambazo ni Kamati ya Fedha na uongozi, mipango na uratibu, mipango miji, mazingira na miundombinu, kamati ya huduma za jamii na kamati ya maadili ya Madiwani.”

Miongoni mwa Madiwani waliohudhuria uapisho huo ni pamoja na Diwani wa Kata ya Kilungule, Said Fella maarufu Mkubwa Fella na Diwani wa Kata ya Mbweni, Single Mtambalike maarufu kwa jina la uigizaji Richie Richie ambapo wote walisema watampa Ushirikiano Meya Matulanga.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here