MARUFUKU MGAO WA UMEME-DK. KALEMANI

0
Naibu Waziri wa Nishati, Stephen Byabato

NA MWANDISHI WETU

Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani ameuelekeza uongozi wa Shirika la Umeme (TANESCO) kuhakikisha kuanzia sasa hakuna mgawo wa umeme nchini na hakutokei ukataji wa umeme kabisa.

Waziri Kalemani aliyasema hayo Desemba 11,2020 wakati akiwa kwenye kikao na Wakuu wa Taasisi na Menejimenti zake zilizopo chini ya Wizara ya Nishati, kilichofanyika katika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa PSSSF eneo la Makole, jijini Dodoma.

Kauli hii ya Dk. Kalemani inatokana na ukweli kwamba hivi sasa Tanzania inazalisha umeme mwingi kuliko mahitaji yake kwa zaidi ya MW 500. Wakati uzalishaji wa umeme ukiwa ni MW 1,601 mahitaji ya umeme nchini ni MW 1,151.

Hata hivyo Dk. Kalemani aliagiza pale wanapolazimika kukata umeme kutokana na sababu za msingi, taarifa itolewe kwa wananchi na warudishiwe umeme kama ilivyoahidiwa katika taarifa ya ukataji huo wa umeme.

Alisema, hii itawezesha uzalishaji viwandani pamoja na kuwezesha kufanyika kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii kwa wananchi wote na hivyo kupelekea upatikanaji wa fedha zinazochangia katika ukuaji wa pato la Taifa linalotokana na Sekta ya Nishati na hivyo kuliletea Taifa maendeleo makubwa ya kiuchumi.

Aidha Dk. Kalemani,aliwataka wakuu wa Taasisi zilipo chini ya Wizara ya Nishati kuhakikisha kuwa  wanafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa, kwa kasi kubwa, ufanisi na umakini ili kuhakikisha sekta ya Nishati inazidi kukua na kuimarika kwa maendeleo ya nchi na watu wake.

Katika kikao hicho, aliambatana na Naibu Waziri wa Nishati, Stephen Byabato, Kaimu Katibu Mkuu Mhandishi Leornad Masanja, Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Eward Ishengoma, Kamishna Msaidizi wa Umeme, Mhandisi. Innocent luoga, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu, Raphael Nombo na viongozi mbalimbali wa Wizara na Taasisi zake.

Akizungumza katika kikao hicho, Dk. Kalemani, aliwataka viongozi wa Taasisi hizo, kuhakikisha  kuwa miradi yote inayotekelezwa na Wizara hiyo inakamilika kwa wakati na kwa ubora zaidi.

Kwa upande wake,Naibu Waziri wa Nishati, Stephen Byabato, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano katika utendaji kazi, kufanya kazi kwa weledi na kujituma na amewaagiza Wataalam wa Habari na Mawasiliano wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake kuhakikisha taarifa za Wizara na Taasisi zake, zinawafikia wananchi kwa usahihi na kwa wakati.

Naibu Waziri wa Nishati, Stephen Byabato

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here