Mapenzi ya Dk. Magufuli kwa mikoa ya Kusini hayana mfanowe

0

NA BWANKU M BWANKU

Mikoa ya Mtwara na Lindi inayopatikana ukanda wa Kusini mwa Tanzania ni moja ya mikoa iliyopelekewa fedha nyingi sana za miradi ya maendeleo na kuwekewa mipango mizito kwa miaka mitano ijayo. Top 10 ya mikoa yenye miradi mingi mikubwa ya kimkakati na kiuchumi huwezi kuiacha mikoa hii ya Kusini. Serikali hii imekuwa na mahaba na mapenzi makubwa sana na Kusini. Hii ni miradi mikubwa ya kimkakati na kazi iliyofanyika iliyoibadirisha na  itakayoibadirisha Kusini kiuchumi na ukanda huo kuwa kitovu kingine cha uchumi wa Tanzania.

  1. Kwenye sekta ya Korosho. Watu wa Kusini wanafahamu na wanajua korosho ilivyokuwa huko nyuma. Ukizungumzia korosho kwa watu wa ukanda wa Kusini ndio kiini na maisha kwa sababu zaidi ya asilimia 80 ya watu wake wanategemea kilimo cha zao hilo.

Huko nyuma korosho ilikuwa shamba la bibi na haikuwahi kuzidi kununuliwa zaidi ya bei ya elfu mbili. Watu wa Kusini waliwahi kuuza korosho mpaka elfu moja na kulipwa mia 4 kwa kidogo kidogo. Yani unauza korosho unalipwa kidogo kidogo mia mbili na mia nne tu. Korosho ilidharauliwa mno. Watu wa Kusini wanafahamu ninachokiongea hapa.

Kuingia madarakani kwa Rais Magufuli mwaka 2015 kulibadirisha kabisa korosho, akaboresha bei mpaka watu wakaiita korosho dhahabu nyeupe. Miaka mitano ya Rais Magufuli korosho haijawahi kushuka wastani wa chini ya elfu mbili na mia tano na kuna wakati bei ya korosho ilifika mpaka elfu 4. Kutoka kulipwa mpaka mia mbili tena kwa kidogo kidogo sasa mkulima anavuta mpunga wake wote mara moja na bei ikipanda tu. Kusini kuchele.

  1. Bandari ya Mtwara bilioni 137. Bandari hii ni moja ya bandari kuu 3 nchini na kubwa ukanda wa Kusini mwa Afrika. Ni mradi wa kimkakati kiuchumi wa mikoa hiyo na Tanzania kiujumla. Katika bajeti ya uboreshaji wa bandari 3 za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara, Mtwara pekee yake imepelekewa bilioni 137 kupanua gati nne za kisasa za bandari hiyo na kuikarabati bandari nzima ya Mtwara ili sasa iweze kupokea na kuhudumia meli kubwa zaidi zenye shehena ya gesi, mafuta, mizigo na mazao ya kilimo, jambo litakaloifanya Mtwara kuwa kitovu cha uchumi Kusini kwa kuifanya kuwa lango kuu la bidhaa na huduma za ukanda mzima wa Kusini na nchi jirani kama Malawi, Msumbiji na Zambia.
  2. Uwanja wa ndege wa Mtwara bilioni 50. Uwanja wa ndege wa Mtwara ni moja ya viwanja vya ndege ambavyo Serikali imepeleka fedha kujenga, kuviboresha na kuvikarabati. Uwanja wa ndege wa Mtwara umepelekewa bilioni 50 ili kuupanua na kuufanya sasa upokee ndege kubwa kubwa zaidi. Hiki ni kitega uchumi kingine ambacho kitaikuza Kusini na kuzidi kucha zaidi.
  3. Barabara ya Mtwara hadi Masasi Km 210. Hii ni moja vitu vilivyowatesa watu wa Kusini kwa miaka mingi sana. Watu wamezaliwa na kufa wakisubiri sana hii barabara lakini wapi wengine walikufa bila ya kuona lami kwenye barabara hii muhimu. Wanasiasa wameombea kura na kujipatia sifa na umaarufu mkubwa sana kupitia barabara hiyo. Ni barabara kubwa inayounganisha wilaya zote za mkoa wa Mtwara kwenda Lindi mpaka Ruvuma kuingia Msumbiji huko.

Ukisikia kero ya barabara Kusini basi ungetajiwa hii barabara. Miaka kwa miaka ilikuwa vumbi na kuathiri sana shughuli za watu hasa ikizingatiwa ni barabara muhimu kiuchumi na muunganiko wa mkoa mzima wa Mtwara na Kusini yote.

Kwa hali isiyo ya kawaida miaka mitano tu ya Rais Magufuli, barabara hiyo imeingizwa kwenye utekelezaji wa utengenezaji wake na awamu ya kwanza kutoka Mtwara mpaka Mnivata Km 50 imejengwa huku kazi ya kuitandika kwa lami barabara hiyo mpaka Masasi ikiwa kwenye mpango kazi. Hakuna aliyeamini lakini ndiyo hivyo leo baada ya kilio cha miaka kwa miaka sasa Serikali ya Rais Magufuli inaijenga barabara hiyo muhimu sana Kusini.

  1. Hospitali kubwa ya kanda ya Kusini ya bilioni 15.8. Ujenzi wa hospitali kubwa ya kanda ya Kusini pale Mikindani unaendelea. Kusini kuna idadi kubwa sana ya watu kwahiyo mpango huu wa Serikali ya Rais Magufuli kujenga hospitali hii kubwa kutaongeza nguvu kubwa sana kwenye sekta ya afya na kuokoa mamia kwa mamia ya watu wa Kusini wakiwemo akina mama, watoto na Watanzania wote waliokuwa wanategemea sana hospitali ya Ligula, Ndanda, Nyangao na zingine chache. Hii ni neema kwa watu wa Kusini.
  2. Ujenzi wa kiwanda cha kuchakata Gesi asilia pale Liganga katikati ya Mtwara na Lindi. Mradi mwingine mkubwa wa kuchakata gesi asilia ambayo imegunduliwa kwa kiasi kikubwa sana ukanda wa Kusini kwenye kina cha bahari ya Hindi. Hapo patatoa ajira za kutosha kwa vijana wa Kusini na kuipeleka kwenye matumizi gesi hii.
  3. Miradi mingine ya Kusini. Ukiachana na miradi hiyo mikubwa ya kimkakati na kazi kubwa iliyofanyika, Kusini imetekeleza miradi zaidi ya 50 ya maji, umeme wa REA umefika na vijiji vyote vilivyobaki vitapelekewa umeme miaka miwili mitatu inayokuja, kwenye vituo vya afya, hospitali, zahanati, mabarabara mengine na vingine vingi sana vimefanyika. Mapenzi ya Rais Dkt John Pombe Magufuli kwa watu wa mikoa ya Mtwara na Lindi hayana mfanowe.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here