MAMBO 10 YALIYOTIKISA MAZISHI YA JPM

0

NA DOTTO KWILASA

HAKIKA usiku wa Machi 17 utabaki kuwa ni usiku mgumu kuwahi kutokea kwa watanzania , kufuatia kutangazwa kifo cha mpendwa wao aliyekua Rais Dk. John Magufuli ambaye kutokana na uchapa kazi wake alipachikwa majina mengi ya kishujaa kama jembe, Tingatinga, Jeshi, Jiwe, mwamba na mengine mengi .

Utabaki kuwa ni usiku wa kukumbukwa kufuatia aliyekuwa makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan akiwa Mkoani Tanga katika ziara yake kutangazwa kwamba mpendwa wao huyo amefariki na watanzania hawatamuona tena.

Nani asiyejua mazuri ya Magufuli, nani asiyejua uthubutu wa Magufuli, nani asiyejua jinsi alivyoipenda nchi yake,?! Ukiunganisha haya yote utaelewa ni kwa nini watanzania walikuwa wakimkilia na wasisikie hata kufarijiwa.

Magufuli huyu ambaye anatazamwa kama zawadi kwa watanzania, ni mtoto wa tatu kuzaliwa kati ya watoto 12 wa Magufuli Marco Nyahinga na Suzana Musa ambao kati ya mwaka 1960 na 1961 waliamua kuvuka ziwa Victoria kutoka Katoma Nkome, Wilaya ya Geita, Mkoa wa Mwanza wakati huo, kwenda Kijiji cha Lubambangwe, Chato, Wilaya ya Biharamulo, Mkoa wa Kagera wakati huo, kutafuta fursa za kiuchumi.

Magufuli alizaliwa Oktoba 29, 1959 katika Wilaya ya Chato ambayo ni mojawapo ya wilaya tano za mkoa mpya wa Geita uliopo kaskazini magharibi mwa Tanzania.

Kutokana na mambo mengi aliyowasaidia watanzania mazishi yake yalionekana kutikisa wakati wa kuuga mwili wake sehemu tofauti tofauti kuanzia Jijini Dar Es Salaam (Uhuru), Dodoma(Jamahuri), Zanzanibar(Amaan), Mwanza(Kirumba) hadi Chato, haya ni Miongoni mwa Mambo yaliyotikisa Wakati wa Kuuga mwili wa Hayati Dk. Magufuli ;

1.MARAIS AFRIKA WAMLILIA

Kutokana na ukarimu wake Marais wa Mataifa mbalimbali ya Afrika wamejitokeza kuomboleza na kutoa heshima zao za mwisho kwa Aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyeagwa Kitaifa katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma baada ya kifo chake kilichotokea Machi 17, 2021.

Marais waliojumuika na Rais wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan na Watanzania wote kwa pamoja walikuwa ni Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambaye ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Mhe. Félix Tshisekedi, Rais wa Msumbiji na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Mhe. Filipe Nyusi, Rais wa Kenya na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC)na Mhe. Uhuru Kenyatta.

Wengine ni Rais wa Afrika Kusini, Mhe. Cyril Ramaphosa, Rais wa Comoro, Azali Assoumani, Rais wa Botswana, Mokgweetsi Masisi, Rais wa Zambia, Mhe. Edgar Lungu, Rais wa Zimbabwe, Mhe. Emmerson Mnangagwa huku Mataifa ya Rwanda, Uganda na Burundi yakituma Wawakilishi kutoa salamu za rambirambi na pole kwa Wananchi watanzania.

Pamoja na mambo mengine, Marais hao wamemuelezea Hayati Dkt. Magafuli kuwa alikuwa Kiongozi muadilifu, mwenye uthubutu, mpenda amani na mtumishi mwadilifu kwa Wananchi wenye kipato cha chini katika Taifa la Tanzania.

Pia Viongozi hao wa Afrika wameeleza kuwa Hayati Dkt. Magufuli hakupendelea kusafiri kuonyesha kuwa maendeleo yanaweza kupatikana hata bila ya kusafiri hivyo kupata muda mwingi wa kuwa na watanzania kwa  shida na raha, usiku na mchana ili kutatua changamoto mbalimbali .

2.JESHI

Kutokana na heshima ya kuwa Amiri Jeshi Mkuu, Jeshi la Wananchi (JWTZ)pamoja na  la Kujenga Taifa (JKT) lilihakikisha kila Jambo linaenda vizuri kuanzia kwenye vibanda vya kuuhifadhia mwili wa marehemu hadi ulinzi wa wananchi wa kawaida .

Hii ni katika kuyaenzi yale yaliyoacha na Hayati Maguli kwa kuwajali watu wa hali zote bila kuwabagua kiitikadi,kidini wala kisiasa.

Licha ya hayo ni lazima tuyape heshima na majeshi mengine kwa jinsi ambavyo yamepambana kuhakikisha ulinzi unakuwa wakutosha.

3.KUTANDIKA NGUO BARABARANI,MATAWI

Maelfu ya Waombolezaji walijitokeza barabarani kutoa heshima zao za mwisho kwa jemedari wa taifa hilo, Vilio vya majonzi vilisikika kando kando mwa barabara ambapo msafara uliobeba mwili wa marehemu Rais Magufuli ulipita, baadhi ya watu walimwaga maua, wengine walivua khanga na mashati yao kuyatandika chini ikiwa ni ishara ya kuomboleza msiba wa kiongozi huyo aliyefariki akiwa mamlakani .

4.VILIO,MAJONZI NA SIMANZI

Hali ya simanzi ilitawala karibu kila pembe ya Tanzania nan je ya mipaka ya Tanzania ,wengi waliomboleza na kushindwa kujizuia.

Wapo waliopoteza fahamu kutokana na kushindwa kustahimili walipoona Janeza la mwili wa hayati Magufuli ,ni jambo la kusikitisha na bado watanzani wataenelea kuomboleza.

5.IDADI YA WATU WENGI VIWANJANI, BARABARANI

Viwanja vyoye vilifurika kupita kiasi kuanzia  Uhuru Dar es Salaam, Jamhuri Dodoma, Amani  Zanzibar  na CCM Kirumba Mwanza na Magufuli Chato huku vilio na majonzi vikitawala katika viwanja hivyo, ambapo shughuli ya kutoa heshima ya mwisho kwa kiongozi huyo iliyekuwa na misisimamo ya kujitegemea kiuchumi, zikifanyika huku baadhi ya wananchi wakibeba mabango mbalimbali ambayo baadhi yalisomeka “ Chuma cha Afrika kimedondoka,Mtetezi wa wanyonge hayupo tena”.

Mbali na viwanjani Maelfu ya wananchi walijitokeza na kujipanga barabarani wakiwa wametoka maeneo mbalimbali na wote wakiwa na hamu ya kushuhudia shughuli mbalimbali za kutoa heshima zao za mwisho kwa Dk.Magufuli ambaye kwenye uongozi wake aliamini katika kuwasadia na kusikiliza wananchi wanyonge wenye changamoto mbalimbali za kimaisha.

Hata hivyo kote ambako mwili wa Dk. Magufuli ulipitishwa Wananchi walishindwa kabisa kuwa na ustahimilivu kwani asilimia kubwa ya wananchi hao walionekana wakibubujikwa na machozi kutokana na mapenzi makubwa waliyokuwa wanayo kwa Dk.Magufuli ambaye kwenye utawala wake alihakikisha awatetea na kuwapigania.

  1. UTAWALA MPYA NA WA KIHISTORIA

 Ili Taifa liendelee ,ilikuwa ni lazima apatikane mrithi wa Hayati Magufuli ambapo kulingana na katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Makamo wa Rais ndiye alipaswa kuwa Rais.

Na hapo ndipo Tanzania iliingia katika historia mpya ya kuwa chini ya mwanamke anayeonekana mwenye haiba ya upole na unyenyekevu, Rais Samiha Suluhu, ambaye kwa jicho lingine anautazama wadhifa wa urais si kazi rahisi, kwani umebeba jukumu la kuwahudumia wananchi kwa usawa.

Hata hivyo watanzania wanamwamini  Samia kwa kuwa anaifahamu nchi, anajua vipaumbele vyake na kuwatoa hofu watanzania kuyaendeleza kwa juhudi mema yalioshughulikiwa na hayati Magufuli.

7.BENDERA UMOJA WA MATAIFA KUPEPEA NUSU MLINGOTI

Si jambo la kawaida kifo cha rais wa nchi moja kuufanya Umoja wa Mataifa kupeperusha bendera zake nusu mlingoti kote ulimwenguni.

Umoja wa Mataifa ulifanya hivyo siku ya maziko ya Hayati Dk. Magufuli Machi 26, 2021 ambapo ilitangaza kufanya hivyo katika makao yake makuu jijini New York nchini Marekani na kuagiza ofisi zake zote ulimwenguni kufanya hivyo.

Lengo ilikuwa kumuenzi Rais Magufuli kutokana na utendaji wake uliotukuka.

8.KILA MKOA ALIKOPITA SHUGHULI ZILISIMAMA

Kwa ujumla nchi ilizizima,Hakuna ambaye alitamani kufanya biashara,kila mtu alitamani kuungana na watanzania wengine katika kuombolea.

Kila alikopita Magufuli vijana wengi wake kwa waume na watoto waliingilia msafara na kuanza kumuita ‘chuma,chuma,chuma’

Na hii ni kiashiria tosha kuwa Hayati Magufuli ametuacha wamoja kwa kutuzoesha kupendana na kulia na wanaolia.

9.MWILI WAKE KUSAFIRI KUPITIA NJIA ZOTE BARABARA, ANGA NA MAJI

Ni upendo wa kipekee ambao Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliamua kumuenzi kwa namna yake ambapo ilitoa nafasi ya mwili wa kiongozi huyo kusafiri na kuacha alama kwa kila aina ya miundombinu ambayo ameiacha.

Tanzania imeshuhudia mwili wa hayati Magufuli ukisafirishwa kwa njia Maji, Ndege na Barabara.

Hali hii imewarahisishia watanzania wengi kushuhudia safari ya mwisho ya shujaa wao.

  1. BODABODA,MAMALISHE,WAMACHINGA WAONYESHA MAPENZI YAO

Katika msafara uliobeba mwili wa Kiongozi huyo aliyepewa jina la “tingatinga” kwa jinsi alivyojipambanuwa kama mpambanaji dhidi ya ubadhirifu kwenye sekta ya umma,watu wa hali ya chini walipata fursa ya kunuaga.

Halikuwa jambo rahisi wa mamalishe,wamachinga na bodaboda kuamini ukweli uliopo kwamba Mwamba huyo hayupo tena.

Wenye bodaboda wengi walionekana kufuatilia msafara huo kuonyesha kumuenzi rafiki yao kipenzi.

“Nenda baba nenda Jemedari wetu, nenda Rais wetu hakika mbio zako umezimaliza,umetuliza baba umejua kutuumiza,tumeumia tuliokupenda,utaishi katika mioyo yetu,tutaishi katika matendo yako, hakika Kulunafsin dhaikatul mauti (Kila nafsi itaonya mauti),” ni maneno aliyosikika kutoka kwa waombolezaji.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here