Mama Samia;CCM imefanya kazi kubwa ya kuleta maendeleo Zanzibar

0

Na Mwandishi wetu

MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alisema hakuna shaka kazi iliyofanywa na serikali ya CCM itatoa matunda makubwa kutokana na hatua kubwa za maendeleo ziliofanyika kisiwani Pemba, kuanzia ujenzi wa barabara kutoka Kengeja- Hole na ujenzi wa hoteli za kitalii zilizozalisha ajira za kutosha.

Samia ameyasema hayo katika mkutano wa kufunga kampeni za CCM kwa upande wa Pemba, uliofanyika katika uwanja wa Gombani ya Kale, Chake Chake Kusini Pemba.

Alibainisha kuwa, Awamu ya Saba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ndani ya miaka 10 ya Rais Dk. Ali Mohameed Shein, imefanyakazi nzuri ikiwemo kuongeza pato la taifa na ukuaji uchumi kwa wastani wa asilimia saba.

Alisema serikali ya Rais Dk. Shein imefanikiwa kupunguza utegemezi wa bajeti kwa kutegemea wahisani kutoka asilimia 30 hadi kufikia asilimia 5.7.

Akizungumzia mapinduzi ya Zanzibar, Samia alisema wananchi wanapaswa kuyalinda mapinduzi hayo na sasa kazi iliyopo ni kuleta mapinduzi ya kiuchumi ndani ya Zanzibar.

“Nataka kusema sisi tuliozaliwa masikini, leo tunaweza kusema mbele ya wananchi. Ungekuwa utawala ule tusingeweza kusimama hapa. Mambo mengi yamefanyika tangu mapinduzi hadi sasa. Tumefungua dira ya mpango wa maendeleo ya Zanzibar, miaka 30 ijayo ambayo kuna mambo yanayopaswa kutekelezwa na kizazi kipya.

“Ndani ya dira hiyo, yapo mambo ambayo Dk. Mwinyi anapaswa kuyetekeleza. Kila watu na zama zao. Dk. Shein anamaliza, mawazo na maono mapya ya Dk. Mwinyi, yataingia kuanza kuleta maendeleo ya Zanzibar yetu,” aliwaeleza wananchi katika mkutano huo.

Alisema CCM ndio chama kilicholeta muungano kupitia CCM na ASP, ambapo umetoa fursa nyingi kwa bara na Zanzibar kunufaika ikiwemo kutumia ardhi na bahari.

Samia alisema muungano umetoa fursa kwa Zanziba kuingia kwenye mabaraza ya kutunga sheria kwa uwiano sawia na sasa umefikia kuwa muungano wa watu kwa kujenga udugu wa damu.

Alisema CCM ndio chama chenye mifumo thabiti ya kuendesha serikali kwa kuwaletea wananchi maendeleo.

Mgombea mwenza huyo wa urais, alibainisha kuwa mgombea urais wa Zanzibar, Dk. Mwinyi amekidhi sifa za kuwa kiongozi wa Zanzibar kwa sababu ni kiongozi mwenye hekima, busara, mtu wa kutulia na kiongozi mwenye kujiheshimu na kuheshimu watu.

“Dk. Mwinyi hana visa moyoni. Amekuja kuungana na wenzake kuja kuleta maendeleo ya Wazanzibar, sio kama wengine wanaotaka urais wakiwa na vinyongo. Wote kwa pamoja Oktoba 28 tukapige kura kwa CCM kwa sababu ndicho chama kinacholeta maendeleo kwa Watanzania.

“Sisi sio watawala, sisi ni watumishi wa Watanzania. Kura yako ndio kielelezo chako na itakupa kujiamini kwa sababu ukikichagua CCM unakuwa sehemu ya kuleta maendeleo,” alisema.

Alisema dalili zinaonyesha CCM kupata ushindi mnono lakini isiwe sababu ya watu kutokwenda kupiga kura kwa kujiamini kwa CCM itashinda kwani Chama kinataka kupata ushindi wa kishindo.

Samia aliwatoa hofu wakazi wa Pemba kuhusu usalama wao kupiga kura, ambapo aliwataka wananchi kwenda kupiga kura pasipo kuwa na hofu kwa sababu serikali imejipanga vizuri kuwalinda wananchi.

“Salam zao hazijatuteteresha, kuna ulinzi wa kutosha, wasiwatishe. Tokeni mkapige kura. Serikali imewawekea mazingira mazuri ya kupiga kura, tokeni mkapige kura.

“CCM ndio chama pekee kinachoendesha siasa na vyama vingine ni vya kiharakati. Watanzania tunajitegemea, bajeti zetu tunaziweza. Wanaharakati wanajambo lao wanalolitafuta,” Samia, alisisitiza.

Akizungumza katika mkutano huo wa ufungaji wa kampeni kwa upande wa Pemba Mgombea wa Urais wa Zanzibar Dk. Mwinyi alisema akipata ridhaa ya kuiongoza Zanzibar serikali atakayoiongoza itahakikisha inaiboresha bandari ya Mkoani na uwanja wa ndege wa Pemba.

Alisema serikali atakayoiongoza itahakikisha uwanja wa ndege wa Pemba unakuwa wenye hadhi ya kimataifa ambapo ndege zote za kimataifa zitakuwa zinafika kisiwa Pemba.

 Dk. Mwinyi alisema mikutano ya kampeni aliyoifanya imemsaidia kutambua na kutafakari kujipima tena dhamira yake ya kugombea nafasi ya urais wa Zanzibar na kwamba ameridhika na dhamira yake hiyo ya kugombea nafasi hiyo.

Alisema pia katika mikutano hiyo aliyoifanya imemsaidia kutambua matamanio ya wanzanzibar ya namna gani Zanzibar inatakiwa iwe.

“Sababu ya kwa nini nyinyi mnichague ni kwa sababu nitakuwa Rais wa kwanza niliyezaliwa baada ya Mapinduzi na Muungano hivyo nitahakikisha ninaleta mapinduzi ya kiuchumi,” alisema.

Aliwaomba wanachama kujitokeza kuipigia kura CCM mnamo Oktoba 28 mwaka huu na si kama baadhi ya wapinzani wanavyowahamasisha kujitokeza Oktoba 27 ambayo ni siku ya watu maalum.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Zanzibar Dk. Abdulla Juma Sadala ‘Mabodi’ alisema kampeni zilizofanywa kuanzia ngazi ya mashina hadi matawi zilifanywa kisayansi.

Alisema maeneo ambayo ametembea Dk.Mwinyi si kidogo amekwenda nyumba kwa nyumba kijiwe kwa kijiwe ambapo katika makundi hayo alikuwa akisikiliza changamoto zao na kwamba amejitahidi sana.

“Kishindo hichi cha kampeni hizi ndizo wapinzani wameingiwa kiwewe kwanza wamehatarisha amani visiwani hapa wanawapiga mapanga katika misikiti wakati wakiwanafunga swala,”alisema

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here