Majaliwa: Mabenki wakopesheni wakulima

0
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza kwenye mkutano wa pamoja na wadau wa sekta ya kilimo, ikiwemo wakulima wa michikichi, wamiliki wa viwanda vya kukamua mafuta, taasisi mbalimbali za kifedha na mamlaka za kiutafiti katika ukumbi wa NSSF katika Manispaa ya Kigoma.

Na Merciful Munuo, KIGOMA

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amezitaka taasisi za fedha kuwaamini na kuwapa mikopo wakulima wa michcikichiki kwani kwa sasa serikali imewekeza kwenye zao la mchikichi kama miongoni mwa mazao ya kimkakati.

Pia amezitaka kutengeneza mikopo itakayoangalia muda wa wakulima kupanda zao la mchikichi hadi kivuna ili kuwawezesha wakulima kurejesha mikopo bila tabu.

Waziri Mkuu ameyasema hayo kwenye mkutano wa pamoja na wadau wa sekta ya kilimo, ikiwemo wakulima wa michikichi, wamiliki wa viwanda vya kukamua mafuta, taasisi mbalimbali za kifedha na mamlaka za kiutafiti.

“Hili suala la mikopo muangalie muwe na vifurushi vya walahu miaka mitatu kwa wakulima hawa maana hauwezi kumpa mkulima kifurushi cha miezi 6 halafu yeye anategemea kuvuna baada ya miaka mitatu utamdai tu,” alielezea Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu Majaliwa aliyataja mazao mengine ya kimkakati kuwa ni pamoja na tumbaku, chai, kahawa, pamba, katani (mkonge) pamoja na korosho.

Alisema kuwa Serikali ya awamu ya tano imejidhatiti kuimarisha kilimo cha mchikichi ili kulifanya zao hilo kuwa na manufaa kwa wananchi wa mkoa wa Kigoma.

Aidha Waziri Mkuu alieleza kuwa serikali imeazimia kuimarisha zao la mchikichi kimkakati, ikimo kuhakikisha kuwa wakulima wa zao hilo wananufaika  kwa kutengeneza vifungashio vya pamoja ambavyo vitawezesha mkulima kufungasha  mafuta ya mchikichi na kuwezesha kuuza bidhaa hivyo kwa bei moja ili kuwaepusha wakulima na ulanguzi.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipanda mche wa mchikichi wakati wa makabidhiano ya miche hiyo kwa wawakilishi wa vyama vya msingi vya ushirika katika kijiji cha Mahembe mkoani Kigoma.

Waziri Mkuu pia amezitaka mamlaka za serikali, ikiwemo serikali ya mkoa, wilaya pamoja na halmashauri kuhakikisha kuwa kunakuwepo na ardhi ya kutosha, kwa wakulima wa mchikichi na wawekezaji kwa kutafuta maeneo yanayofaa ikiwemo maeneo yaliyokaa muda mrefu bila kuwekezwa.

“Wakurugenzi angalieni maeneo ambayo hayajaendelezwa muwapatie wakulima wa michikichi, pamoja na wawekezaji ili zao hili liwanufaishe wana Kigoma.” aliongeza Waziri Mkuu.

Pia alipongeza jitihada zinazofanywa na maofisa kilimo, na kustaajabishwa na kitendo cha maofisa kilimo kupongezwa na wadau mbalimbali kwani hali ni tofauti maeneo mengi ambapo maofisa wilaya wamekuwa wakikosolewa utendaji kazi wao.

“Mimi nimefanya kwenye taasisi za kilimo nyingi na kila mahali utasikia wanalalamikia maofisa kilimo, lakini nimeshangaa leo hapa wanapongezwa, hongereni sana kwa kazi nzuri, ” aliongeza

Waziri Mkuu pia alimtaka waziri wa kilimo kutafuta wawekezaji wa kilimo cha zao la mchikichi, ikiwemo kumpigia simu muwekezaji  Bakhresa ambaye ameonyesha nia ya kuwekeza kwenye zao hilo.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipatia mche wa mchikichi, idd mbarouk mwakilishi wa Vyama vya msingi vya Ushirika (AMCOS). kulia ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Elias Kwandikwa na wa pili kulia ni Waziri wa Kilimo, Prof. Adolf Mkenda

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here