Majaliwa azindua safari MV Mbeya II Mbamba Bay

0

Na Merciful Munuo, Nyasa

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alizindua Meli ya MV Mbeya II ambayo inafanya kazi ziwa nyasa pamoja na kukagua Barabara ya Mbamba Bay Njombe ambayo Imejengwa kwa kiwango cha lami, huku akiitaja barabara hiyo kuwa ni ya kiwango cha juu.

Waziri Mkuu Majaliwa aliyasema hayo jana wakati wa uzinduzi wa meli ya MV Mbeya II pamoja na ukaguzi wa barabara ya kuingia Mbambabay.

Aidha waziri Mkuu Majaliwa aliwataka wananchi na wana Ruvuma na Nyasa kuchangamkia fursa za meli pamoja na Ujenzi wa barabara kuhakikisha kuwa wanFanya biashara na nchi jirani.

“Bandari ndio hii, na sasa mbamba bay muanze kuitumia, wenzetu wakipata njaa sasa muwapelekeee vyakula kwa kutumia meli hii na TPA tayari wametuambia, bado tunaendelea kujenga gati kubwa pamoja na nyumba ya abiria” alisema.

Majaliwa alisema kuwa amekagua barabara ya mbamba bay akitokea Njombe ambapo ameeleza kuwa barabara hiyo ambayo imejengwa kwa kiwango cha lami ni ya kiwango.

“Kilometa 66 Barabara pana, nimeshuhudia, barabara hii, hapo zamani ilikuwa ni makorongo lakini kwa sasa ni ya kiwango cha Lami, unateleza tu” aliongeza Majaliwa

Alisema kila mkoa kwa sasa unafikiwa kwa kiwango cha lami, na kueleza kuwa kwa sasa serikali kwa sasa ina mpango wa kujenga barabara kwa kiwango cha lami kuunganisha wilaya.

Aidha Majaliwa alieleza kuwa sasa hivi maeneo ya Nyasa na mengine yatakuwa na miundombinu inayounganisha wilaya.

“Ujenzi wa Meli hii na Ujenzi wa Bandari ya Mbamba Bay ni kwa kukuza uchumi na kuwajengea uchumi wenu na nitoe wito kwa watanzania kuja kuwekeza Mbamba Bay kwani sasa hivi umeme upo, sasa wanaweza kuja kuleta viwanda, kwani mihogo inalimwa huku,” alisema.

Waziri Mkuu Majaliwa aliwataka vijana wa mkoa wa Ruvuma na wilaya ya Nyasa kuanza kufanya biashara, na kueleza kuwa atawaona vijana wa ajabu watakaolalamika hakuna fedha wakati fursa zimeletwa.

“Huwezi kupata maendeleo ya watu bila kuleta vitu, leo vijana wakitaka waanzishe saluni umeme upo ni kitu, ukitaka kupeleka mizigo yako utatumia barabara ni kitu na ukitaka kusafiri kwenda na biashara yako Malawi utatumia meli, ni kitu,” alisema Waziri Mkuu. 

Aidha alibainisha kuwa tayari serikali imejanga bandari ikiwemo bandari kubwa ya Karema inayojengwa kwa bilioni 47, pamoja na kuboresha bandari za Ziwa Victoria huku akieleza kuwa Ujenzi wa Bandari ya Mbamba Bay utakuwa ni mkubwa zaidi.

Waziri Mkuu alisema kuwa serikali inaendelea na ujenzi wa meli ya mabehewa ambayo itakuwa na uwezo wa kubeba mabehewa 50, sawa na tani 3,000.

Majaliwa pia alieleza kuwa Serikali inajenga Meli kubwa ya abiria na mizigo ambayo itakuwa inafanya shughuli zake eneo la Ukanda wa bahari kwenda hadi nchi jirani ikiwemo nchi ya Comoro na Maeneo mengine.

“Chini ya Miaka Mitano Serikali ya awamu ya Tano imeweza kufikia uchumi wa Kati, na Serikali itaendelea kujenga miradi ya usafiri na usafirishaji na kufungua fursa za kijografia kila eneo” alisema Majaliwa.

Aidha Majaliwa alimpongeza Mkandarasi Songoro ambaye amejenga Meli za Ziwa Nyasa pamoja na Meli nyinginezo alizozijenga.

“Alipojitokeza Mtanzania huyu aliowaajiri wote ni Watanzania, na Ujenzi wa barabara kutoka Mbinga hadi Mbamba Bay wameajiri watanzania 500 na nimetoa maagizo watanzania wanaofanya kazi za ujenzi wa madaraja na Meli tuwajue ili waendelezwe na tuwape miradi mingine, watanzania tunaweza,” aliongeza Waziri Mkuu.

Pia aliagiza wizara ya maji kuhakikisha kuwa wananchi wa Nyasa wanapata maji kutoka ziwa Nyasa kama ilivyo kwa Ziwa Victoria

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya alisema kuwa ujio wa waziri mkuu kwenye bandari ya mbamba bay ni wa kuweka historia kwani kuna mahusiano makubwa kati ya bandari na barabara.

 

Aidha ameeleza kuwa wakati wa kutembea kwa bajaji nchi nzima umewadia na kupongeza jitihada za serikali za uboreshaji wa miundombinu ikiwemo, miundombinu ya barabara.

“Nitoe shukrani kwa ushirikiano tulioupata kwa wananchi na uongozi wa mkoa na wilaya kwani mkandarasi ameshukuru sana kwa ushirikiano huo,” aliongeza.

Alisema kuwa ujenzi wa miundombinu hii sasa utafungua Ushoroba wa Mtwara na kueleza kuwa sasa hivi bandari hizi zitatumika kwa tija.

“Tunajua watu wa madini wapo huku, watu wa maliasili na watu wa mifugo na uvuvi, ili sasa fursa hii iwe na tija kwa ukuaji wa Nyasa” alisema.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme, alitaka wananchi wa mkoa wa Ruuma kuchangamkia fursa hiyo kwani kwa sasa fursa hiyo itainua uchumi wa Wanaruvuma.

Aidha alipongeza jitihada za serikali kwani imekuwa ikitoa fedha kwa wakati ambapo pia amepongeza serikali kuwapa wazawa mirafi mikubwa kwani meli hii imejengwa na mkandarasi wa Marine Songoro ambaye ametekeleza ujenzi wa meli ya MV Mbeya II.

“Waziri Mkuu, kitendo ulichojifanya leo ni cha kihistoria, kwani kwa sasa meli za Mv Mbeya II ipo majini, Mv Ruvuma na Mv Njombe nazo zipo majini” alisema RC Mndeme na kuongeza kuwa;

“Sasa usafiri wa mizigo utaongezeka kwa kutumia meli za mv mbeya II, mv njombe na meli ya mv ruvuma pamoja na kukamiika kwa barabara ya lami inayounganisha mji wa songea na  Nyasa.

“Niipongeze serikali ya awamu ya tano kwa kuhakikisha kuwa mkoa wetu unanufaika na huduma muhimu ikiwemo huduma za afya, ambazo pia zimekuwa zikinufaisha hadi nchi jirani ya msumbiji.”

Aidha alipongeza jitihada za serikali za kuinua ndoto za vijana kwa kuleta vyuo vya Veta pamjoja na Sido pamoja na Kuimarisha Maeneo ya kiutendaji ya serikali ikiwemo ujenzi wa ofisi za mkuu wa wilaya Nyasa pamoja na Ujemzi wa ikulu Ndogo

Mkuu wa Mkoa huyo pia alipongeza ujenzi wa bandari ya Ndumbi pamoja na Ujenzi wa Daraja la Ruhuhu Pamoja na Miradi mingine mingi ambayo inaleta Tija kwa wananchi.

Akizungumza kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama vya Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Ruvuma alipongeza jitihada za serikali kutekeleza ahadi zake kwa kuleta umeme, kujenga barabara pamoja na kuleta meli kubwa ambazo zitaleta tija na amaendeleo kwa wana Ruvuma na Nyasa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here