Majaliwa athibitishwa na Bunge kuwa Waziri Mkuu kwa kipindi cha pili

0

Bunge la Tanzania limemuidhinisha mbunge wa Ruangwa (CCM), Kassim Majaliwa kuwa Waziri Mkuu baada ya kupigiwa kura za ndiyo 350.

Majaliwa alikuwa Waziri Mkuu kuanzia mwaka 2015 hadi Novemba 5, 2020 siku ambayo Rais John Magufuli alikula kiapo cha kuwa kiongozi mkuu wa nchi.

Kwa kuangalia mwenendo, historia, tabia ya marais waliopita na uteuzi ulioanza kufanyika, haikuwa vigumu kukuna kichwa kujiuliza kama Majaliwa atarejeshwa katika nafasi ya Waziri Mkuu.

Licha ya kuwa Katiba hailazimishi kuteua mtu yuleyule kuendelea na nafasi ya Waziri Mkuu, inampa Rais nafasi ya kuteua mtu mwingine kama hakuridhishwa na utendaji wa aliyekuwepo awali.

Tangu mfumo wa vyama vingi uliporejeshwa mwaka 1992, marais wawili walioanzia mwaka 1995 hawakubadili mawaziri wao wakuu kwa utashi; Benjamin Mkapa, aliyeongoza awamu ya tatu, alianza na kumaliza na Frederick Sumaye na Jakaya Kikwete, aliyeongoza awamu ya nne, aliendelea na Mizengo Pinda aliposhinda Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.

Lakini Kikwete alilazimika kuteua Waziri Mkuu mwingine mwaka 2008 baada ya aliyekuwepo, Edward Lowassa kujiuzulu kutokana na sakata la mkataba wa Richmond.
Dalili za kujirudia kwa hali hiyo  zilianza kuonekana baada ya Rais Magufuli na makamu wake, Samia Suluhu Hassan kukubaliana Profesa Kilangi Adelardus aendelee na nafasi yake ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Pia Kamati Kuu ya CCM ilipitisha majina ya Job Ndugai na Dk Tulia Ackson kuwania nafasi za Spika na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano ambapo Ndugai alichaguliwa kuwa Spika na leo unafanyika uchaguzi wa naibu spika.

Swali lililokuwa vichwani mwa watu ni je Rais Magufuli, ambaye ni mthubutu na asiyetabirika, ataendeleza utamaduni huo katika nafasi ya Waziri Mkuu.
Jibu ni ndio, ameendelea na utaratibu huo na kumteua tena Majaliwa kuwa Waziri Mkuu.

Majaliwa aliteuliwa Novemba 19, 2015 lakini uteuzi huo ulikosolewa kwa hoja kuwa mbunge huyo hakuwa na uzoefu baada ya kuingia bungeni mwaka 2010 na baadaye kushika nafasi ya naibu waziri wa Tamisemi kwa miaka mitano.

Lakini utu, ukweli, uadilifu, uzoefu wake kama mwalimu na kiongozi wa vyama vya wafanyakazi, ulimuwezesha kuonyesha wakosoaji kuwa alikuwa mtu sahihi kushika wadhifa huo.

Amekuwa mstari wa mbele na mtekelezaji mkubwa wa maagizo ya Rais na Serikali, akizunguka mikoani na kuanika uozo katika ngazi ya kuanzia wilaya hadi mkoa.

Majaliwa alizaliwa Desemba 22, 1961 alisema Shule ya Sekondari ya Kigonsera.

Alipata diploma ya ualimu Chuo cha Ualimu Mtwara alikomaliza mwaka 1993 kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alikomaliza mwaka 1998.

Baadaye alikuwa katibu wa wilaya wa Chama cha Walimu kabla ya kuteuliwa kuwa mkuu wa wilaya ya Urambo mwaka 2006. Mwaka 2010 aligombea ubunge wa Ruangwa na kushinda.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here