Majaliwa aagiza watendaji AMCOS Mbinga wakamatwe

0

NA MWANDISHI WETU, RUVUMA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Ruvuma, Hamza Mwenda ahakikishe anawakamata viongozi wa AMCOS kwa tuhuma za kutoa fedha za wanachama na kuwapa madiwani ili wakawashawishi madiwani wenzao wakubali kubadilisha eneo la ujenzi wa ofosi za Halmashauri ya Wilaya hiyo.

Madiwani waliohusika katika mvutano huo ni wa kata za Mkumbi (Bruno Kapinga), kata ya Lukalasi (Bosco Ndimbo) na wa kata ya Linda (Haule), ambao wanadaiwa kuchukua fedha kutoka kwa watendaji wa AMCOS kwa ajili ya kwenda kushawishi madiwani wenzao wakubali kuhamishwa kwa eneo la ujenzi wa makao makuu ya halmashauri hiyo.

Alitoa agizo hilo jana baada ya kuzindua jengo la utawala la Halmashauri ya Mji wa Mbinga akiwa wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma. Waziri Mkuu alimuagiza Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christine Mndeme asimamie ujenzi wa halmashauri hiyo unaoendelea katika eneo la Kigonsera.

Hatua hiyo imekuja baada ya kuwepo kwa mvutano wa Madiwani wa Halmashauri ya Mbinga Vijijini ambao baadhi yao hawataki makao makuu ya halmashauri hiyo yajengwe Kigonsera na kuamua kuendesha mchakato wa kushawishi wengine wagomee mradi huo jambo ambalo linakwamisha maendeleo kwa sababu tayari mradi huo umeshaanza kujengwa.

Mvutano huo unaongozwa na Madiwani wa Kata tatu za Mkumbi, Lukalasi na Linda ambao wanataka makao makuu yajengwe kwenye kata ya Mkumbi katika eneo ambalo litailazimu Serikali ilipe fidia ya zaidi ya Sh milioni 400 huku kukiwa na eneo la bure la ekari 150 ambalo ndiko yanakojengwa makao makuu.

“Hatuwezi kukubali, huko mnakotaka nyie ni lazima tulipe fidia ya zaidi ya Sh. milioni 400 na kuna eneo la bure ekari zaidi ya 150, hii haikubaliki hatuwezi kufanya mambo ya siasa kwenye fedha za wananchi haiwezekani. Mmeamua kila AMCOS ichange Sh. 600,000 mpate milioni tatu mfanye kampeni ya kutaka halmashauri ijengwe kwenu. Hiyo ni rushwa,” alisema Majaliwa.

Waziri Mkuu aliongeza; “Kwa kuwa zile ni fedha za wakulima, Kamanda wa TAKUKURU kawakamate watendaji wa AMCOS hizo wahojiwe kwa nini walitumia fedha za kuwapa Madiwani wakahonge ni lazima wahojiwe waeleze ni nani aliyetoa maagizo ya kutoa Sh. milioni tatu. Hatuwezi kutumia fedha za wananchi kwa ajili ya kuhonga watu lazima fedha hizo za wakulima zirudishwe ni mali ya wakulima.”

Mapema, Waziri Mkuu alizindua jengo la utawala la Halmashauri ya Mji wa Mbinga na kukagua ujenzi wa nyumba nane za watumishi wa halmashauri hiyo ambapo alisema ameridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo iliyogharimu Sh. bilioni 3.7

Pia, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kumpongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mbinga, Grace Quintine kwa usimamizi mzuri wa miradi hiyo ambayo imejengwa kwa viwango bora na majengo hayo yanalingana na kiwango cha fedha kilichotolewa.

“Tulimletea Sh. milioni 350 hapa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba saba za watumishi na ametumia milioni 321 na tulimletea Sh. milioni 300 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya Mkurugenzi lakini ametumia shilingi milioni 251 na hakuna ubabaishaji majengo yote yamejengwa kwa viwango bora. Nampongeza sana Mkurugenzi huyu amefanya vizuri sana endelea kujenga miradi mingine ikiwemo ya vyumba vya madarasa,” alisema Majaliwa.

Baada ya kupokea pongezi Mkurugenzi huyo alisema halmashauri yao katika mwaka wa fedha 2019/2020 ilipokea Sh. milioni 650 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za watumishi zikiwemo saba za Wakuu wa Idara na moja ya Mkurugenzi.

Alisema gharama za ujenzi wa nyumba saba za Wakuu wa Idara ni Sh. milioni 321.771 ambapo kila nyumba iligharimu sh. milioni 45.967 badala ya Sh. milioni 50 zilizoidhinishwa na kupokelewa ambapo ilikadiriwa kutumika Sh. milioni 350 kwa nyumba zote.

“Ujenzi wa nyumba ya ghorofa moja ya Mkurugenzi wa Mji umegharimu Sh. milioni 251.780 huku makadirio yakiwa ni Sh. milioni 300. Lengo la miradi hii ni kuboresha mazingira ya makazi ya watumishi wa halmashauri ikiwa ni pamoja na kupunguza kulipa posho za nyumba kwa kila mwezi.”

Alisema Sh. milioni 28.228 zilizobaki katika ujenzi wa nyumba za Wakuu wa Idara zitatumika kujenga mnara wa tenki la maji na uwekaji wa tenki moja la maji kwa kila nyumba na kuanza ujenzi wa uzio kuzunguka nyumba zote saba.

Mkurugenzi huyo alisema mbali na utekelezaji wa ujenzi wa miradi hiyo ya nyumba za makazi, pia Serikali ilitoa Sh. bilioni 3.1 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la utawala la halmashauri hiyo ambalo lilijengwa na kampuni ya SUMA-JKT Kanda ya Mtwara.

Alisema ujenzi wa jengo hilo la utawala lina jumla ya vyumba 52 vikiwemo vyumba vya ofisi za watumishi na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji, ukumbi mkubwa wa mikutano na ukumbi mdogo kwa ajili ya vikao vya Wakuu wa Idara na Vitengo. “Ujenzi umekalika na lilianza kutumika Januari 2020. Naishukuru Serikali kwa utekelezaji wa miradi hii.”

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo Kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Mbinga, Grace Quintine (kushoto) kuhusu ukumbi wa Halmashauri ya Mji Mbinga wakati alipofungua jengo la Halmashauri hiyo, jana. Wa pili kushoto ni Mke wa Waziri Mkuu, Mama Mary Majaliwa na wa tatu kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here