Mahakama yamhukumu Mr Kuku kulipa fidia bilioni 5, faini milioni 5 au jela miaka mitano

0

Na Mwandishi Wetu 

Mahakama ya hakimu mkazi Kisutu imemhukumu mfanyabiashara, Tariq Machibya (29) maarufu Mr Kuku kulipa fidia ya Sh bilioni 5.4 baada ya kupatikana na hatia ya kushiriki  biashara ya upatu na kukubali kupokea miamala ya fedha.

Pia,  imemhukumu kulipa faini ya Sh milioni tano au kwenda jela miaka mitano sambamba na kuamuru Sh bilioni 5.4 zilizopo kwenye akaunti ya mshtakiwa huyo kuhamishiwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwenye akaunti ya mkurugenzi wa mashtaka (DPP).

Hata hivyo, mshtakiwa ameshindwa kulipa faini na kurejeshwa rumande.

Mahakama imetoa hukumu hiyo baada ya kumtia hatiani katika mashtaka mawili ya kushiriki  biashara ya upatu na kukubali kupokea miamala ya fedha baada ya kukiri  mashtaka yake DPP.

Uuamuzi huo umetolewa leo Jumatano Desemba 16, 2020 na hakimu mkazi mfawidhi, Godfrey Isaya.

Awali, wakili wa Serikali mkuu, Paul Kadushi akisaidiana na wakili wa Serikali mwandamizi, Wankyo Simon amedai kuwa kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya kusomewa mashtaka baada ya mshtakiwa huyo kukiri mashtaka yake kwa DPP baada ya kufanya majadiliano naye na kufikia makubaliano Desemba 7, 2020.

Amesema baada ya kufikia makubaliano na DPP amemfutia mashtaka manne kati ya saba yaliyokuwa yanamkabili.

Mashtaka aliyotiwa hatiani ni kusimamia biashara ya upatu na kupokea miamala ya fedha kutoka kwa umma bila kuwa na leseni.

Kati ya Januari 2018 na Mei 2020 katika maeneo mbalimbali ya jijini Dar es Salaam mshtakiwa anadaiwa kusimamia biashara ya upatu.

Machibya anadaiwa alijihusisha na biashara ya upatu kwa kukubali na kukusanya fedha kutoka kwa umma, akijifanya kwamba watafanya ujasiriamali wa ufugaji wa kuku na wangepata faida ya asilimia 70 ya mtaji wa awali waliowekeza kwa miezi minne na asilimia 90 ya mtaji wa awali waliowekeza kwa kipindi cha miezi sita, kiasi ambacho ni kikubwa katika biashara kuliko mtaji uliokusanywa.

Shtaka pili,  siku na maeneo hayo mshtakiwa anadaiwa kuwa alikubali na kupokea miamala ya fedha za umma kiasi cha Sh bilioni 17 bila kuwa na leseni.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here