Magufuli, Wang Yi washuhudia utiaji saini ujenzi SGR Mwanza – Isaka

0


Na Bethsheba Wambura

Rais Dk. John Magufuli na Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi wameshuhudia utiaji saini kati ya Tanzania na kampuni mbili za China ambazo zimeshinda zabuni ya ujenzi wa mradi wa mkubwa wa Reli ya Kisasa (SGR) kwa dola za Marekani bilioni 1.32 sawa na Sh trilioni 3.06 ikiwa ni awamu ya tano ya mradi kuanzia Mwanza mpaka Isaka wenye urefu wa kilometa 341.

Reli hiyo inayounganisha nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Rwanda na Burundi, itakapokamilika itakuwa na uwezo wa kubeba treni yenye kuvuta mabehewa 100 na kubeba mzigo wa mpaka tani 10,000 kwa mkupuo sawa na uwezo wa malori 500 ya mizigo.

Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi, kampuni zilizoshinda zabuni ni Kampuni ya Ujenzi ya Civil Engineering Construction (CCEC) na Kampuni ya Reli ya China (CRCC), ambazo ujenzi huo unatarajiwa kumalizika ndani ya miezi 36.

Utiaji saini huo umefanyika na pande mbali ambapo kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mkurugenzi wa ShirIka la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa amesaini na upande wa Mkandarasi amesaini Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Ujenzi ya CCECC, Jiang Yigao

Akizungumza baada ya kutia saini Kadogosa amesema makampuni zaidi ya 18 yalijitokeza na baada ya kufanya mchakato kwa mujibu wa sheria za nchi Kampuni hiyo ilishinda zabuni hiyo.

“Makampuni zaidi ya 18 ya Kimataifa yalijitokeza kujenga reli ya kisasa kipande cha Mwanza – Isaka ni 108, baada ya kufanya mchakato kwa mujibu wa sheria za nchi yetu, kampuni za CCECC zilishinda zabuni, gharama ya mradi ikiwa ni Sh Trili 3.0677,” amesema Kadogosa.

Ujenzi wa reli hiyo upo katika awamu tano, awamu ya kwanza ni Dar es Salaam – Morogoro, ya pili Morogoro – Makutupora, awamu ya tatu Makutupora – Tabora, awamu ya nne Tabora – Isaka na awamu ya tano Isaka – Mwanza. Awamu ya kwanza ilizinduliwa na Rais Magufuli, Aprili 12, 2017 na awamu ya pili Machi 14, 2018 ukitekelezwa na Kampuni ya Uturuki ya Yapi Markez.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here