Magufuli ndiyo chaguo letu- Machinga

0

NA MWANDISHI WETU

IKIWA imebaki siku moja Uchaguzi Mkuu ufanyike, Jumuiya ya wafanyabiashara ndogondogo ‘machinga’ na madereva pikipiki ‘bodaboda’ nchini, wametoa msimamo wao kuwa watampigia kura mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli.

Wamesema hatua hiyo inatokana na mgombea huyo kubeba agenda za Watanzania na makundi yao ikiwamo kuwapatia vitambulisho vya umachinga ambayo ni sababu kuu inayowafanya wao kumpa kura nyingi na za kishindo kesho.

Wakizungumza na waandishi habari jijini Dar es Salaam jana, walisema wanaunga tamko lao ambalo limetolewa na wenzao katika mikoa mitano ikiwamo Simiyu, Mwanza, Iringa, Katavi na Mbeya hiyo jana na kwamba ndiyo msimamo wa wafanyabiashara wote kwani wamechoka kutumiwa kama madaraja na kisha kutelekezwa.

Makamu Mwenyekiti Mwenyekiti wa Machinga Taifa, Steven Lusinde serikali ya awamu ya tano imewafanyia mambo makubwa kwa ujumla na wanamuunga mkono Rais Magufuli haya tunayozungumza yameonekana.

“Tumepewa vitambulisho vina faida kubwa kwetu kwenye maeneo ya mjini, tunapata mikopo, bima ya afya na bado watu wanafanya biashara bila kusumbuliwa.

“Rais ametutoa utumwani kutupeleka nchi ya ahadi na ndani ya miaka mitano tumepata faida kubwa kuliko wakati mwingine. Kwa hiyo sisi wote nchi nzima lengo letu ni moja tu, ashinde hivyo tutajaza kura za kutosha kwenye debe la kura.

“Alituamini bodaboda, machinga na mama lishe, kwanini sisi leo tusimthamini kwa kumpa kura, bado siku moja tu tutamfanyia jambo zuri tutatia tiki tu pale kwa rais, wabunge na madiwani wote wa CCM,” alisema.

Lusinde alisema hawajawahi kuiunga mkono serikali  yoyote tangu nchi hii imepata uhuru na kwamba hii ndiyo serikali ya kwanza.

“Wafanyabiashara wanaenda kuwa matajiri na tunaenda na imani kubwa tusikubali kutumika, tumetumika vya kutosha na wanasiasa wanatufanya madaraja wanatupandia kisha wanatutelekeza.

“Lakini Magufuli ametupelekea sehehemu ambayo hatujawahi kuitegemea tangu nchi ipate uhuru. Wamachinga wote tunakwenda na Magufuli, na wafanyabishara wote kuanzia leo tutafute pesa leo na kesho ili kesho kutwa twende tukapige kura na kwenda nyumbani kula pilau kusubiri rais aapishwe,” alisema.

Kwa upande wake Mweka Hazina wa bodaboda jijini Dar es Salaam, Saidi Chenja alisema wajasiariamali wakiwamo waendesha bodaboda na bajaj lazima wahubiri amani kwani ndiyo tunu ya taifa ambapo Oktoba 28 lazima wafanye maamuzi sahihi.

“Viongozi wa upinzani wamezoea kutupandia sisi kama majukwaa wanatutumia kisasa kisha wanatuelekeza, sasa tumeamua jambo moja, ni bora ule ugali maharage kwa furaha kuliko biriani kuku kwenye machozi.

“Bodaboda ulikuwa nzuio la kuingia mjini tangu sasa tunaingia mjini bila bughudha. Tulikuwa tunaonekana tuna vurugu lakini niwahakikishie Watanzania hakuna atakayevunja amani iwe Dar es Salaam au mkoa mwingine wote tutakwenda kupiga kura,” alisema.

Pamoja na mambo mengine, alisema wameshuhudia kazi imefanyika ndani ya miaka mitano na kusisitiza waendelee kumchagua Magufuli kwani ni kingozi mzuri ili aendelee kuwatendea mazuri.

“Kiongozi mzuri lazima apate upinzani. Ametuteteta wanyonge bodaboda, machinga na mama lishe Oktoba 28 tusifanye masikhara ili atakeyesema kura zake zimeibwa aone Magufuli anaongoza kuanzia asilimia 90. Tusifanye makosa, rais anataka mafiga matatu ili akitaka kutoa mikopo kwetu kusiwe na vikwazo ndiyo maana tunataka kumpelekea mafiga matatu,” alisema.

Naye mfanyabiashara Saidi Mrisho, alisema kitambulisho cha wamachinga kwa mara ya kwanza wamekipata baada ya kuhangaika sana lakini kwa busara zake Magufuli aliona kwanini zoezi hilo linasuasua akawapatia.

“Kitambulisho hiki kimetusaidia kupata mikopo, Magufuli katuondolea adha ile ya kukimbizwa kimbizwa mitaani tukifanya biashara leo hiii tusingekuwepo lakini pia nina bima ya afya hii haijawahi kutokea tangu uhuru.

“Tunapata mikopo CRDB na NMB, yaani ni nafasi yako hakuna hati ya nyumba wala kiwanja. Jukumu letu ni kumfurahisha yule eliyetuweka sisi tuwe juu. Hakuna chinga aliyekuwa anakipenda chama chochote isipokuwa yeye ametufanya tuipende CCM, tumeanza pamoja na tutamaliza pamoja.

Mjumbe wa Bodaboda Mkoa wa Dar es Salaam, Mussa Chengula alisema Serikali ya awamu ya tano inatofautiana sana na awamu zilizopita kwani kafanya makubwa sana hususani kwa bodaboda pale aliporidhia kutambua boda kuwa usafiri rasmi kisheria.

“Nasiki kuna miaka mitano tena na miaka mitano kwanza, hakuna sababu ya mitano kuipeleka sehemu nyingine zaidi ya CCM.

“Hakuna asiyemfahamu Farao aliwaua watoto wa kiume lakini Mungu alimvumilia Musa akakua. Lakini tukizungumia Sodoma na Gomora Mungu hakuvumilia, huyu mgombea wa miaka mitano kwanza anatuletea mambo ambayo katiba yetu hairuhusu.

“Ibara ya 18 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mawasiliano siyo mahusiano, nchi yetu hairuhusu mambo hayo,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here