Magufuli :Marufuku fomu za maadili viongozi wa umma kujazwa mtandaoni

0

Na Mwandishi Wetu 

Rais Dk. John Magufuli ameiagiza sekretarieti ya maadili ya viongozi wa umma kusitisha utaratibu wa kupokea fomu zilizojazwa na viongozi wa umma kwa njia ya mtandao kwa lengo la kuepuka tishio la udukuzi wa taarifa za siri kwa viongozi na watumishi wanaofikia zaidi ya 15,000.

Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Disemba 24, 2020 jijini Dar es Salaam wakati wa kumuapisha kamishna wa maadili, Sivangilwa Mwangesi aliyeahidi kutekeleza majukumu yake vyema. Mwangesi alikuwa  Jaji wa Mahakama ya Rufani.

Mwangesi ameteuliwa na kisha kuapishwa leo baada ya kifo cha aliyekuwa kamishna wa maadili, Harold Nsekela kilichotokea Disemba 6, 2020 baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Rais Magufuli alimtaka Kamishna Mwangesi kuhakikisha anaepuka utaratibu huo kutokana na uwepo wa wadukuzi wengi kwa sasa kupitia mageuzi ya teknolojia ya habari na mawasiliano.

“Unaweza kufanya mambo mengine yote kwa mtandao lakini ajaze kwa mfano Chief Secretary (Katibu Mkuu Kiongozi) aeleze alichonacho na labda awe na nyumba ndogo, aseme na wala hajaitangaza kwa mke wake halafu aiweke mtandaoni halafu mtu awe anaijua ile password , sasa ule usiri na utakatifu wa Idara hiyo mnaupoteza.”

“Nilimueleza marehemu Jaji Nsekela fomu unaweza kuzipakua kwenye mtandao lakini zisirudishwe tena kwa mtandao, kila mmoja anajua anarudisha wapi, najua Spika, wewe unaleta kwangu, najua wengi wanajaza MaDC, DED, RAS, RC kwa hiyo ni vyema wapakue hizo fomu na wazirudishe mahali panapotakiwa  wenyewe.”

“Najua wasaidizi wako wamenielewa, hatutakiwi kuwa wazi kiasi hicho, mtu akishaifahamu ile programu anaweza kuhariri, wadukuzi wako wengi. Umejaza una Sh milioni 10 akakujazia una Sh milioni 100 halafu unakuja kuulizwa ulijaza hiyo na sahihi yako iko pale,” amesema Magufuli.

Rais Magufuli ameagiza viongozi na watumishi wa umma kujaza fomu hizo na kuzirejesha mapema kabla ya Disemba 30, 2020 kama inavyoelekezwa kisheria.

“Hakuna sababu tena ya kisingizio, wengi hamjapeleka fomu hata mimi yangu nilikuwa sijapeleka sasa nitaijaza haraka nikupatie kwa taratibu na sheria za nchi yetu,” amesema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here