Magufuli: Dk. Slaa alikuwa mwanasiasa bora wa upinzani

0

Na Mwandishi Wetu

MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) Dk.John Magufuli amewaambia maelfu ya wananchi wa Wilaya ya Karatu mkoani Arusha tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi nchini, kiongozi bora kwake kutoka vyama vya upinzani ni Dk.Wilbrod Slaa na ndio maana aliamua kuteua kuwa Balozi katika nchi tisa za Ulaya.

Dk.Magufuli ameyasema hayo leo mbele ya wananchi hao wakati akiwaomba kura ili aweze kuongoza tena nchi kwa kipindi cha miaka mitano ambapo ametumia nafasi hiyo kufafanua mwaka 1992 nchi ilianzisha mfumo wa vyama vingi ili kupanua na kuongeza wigo wa wananchi kutoa maoni mbadala.

“Msema ukweli mpenzi wa Mungu, tangu kuanza kwa mfumo huu wamejitokeza viongozi wengi vizuri.Kiongozi bora kwangu mimi kutokea katika upinzani ni Dk.Wilbroad Slaa , nina mfahamu wakati anakuja kuomba Ubunge hapa Karatu aliomba kupitia CCM, lakini alifanyiwa figisu na kuamua kwenda upinzani.

“Nakumbuka Dk.Slaa hata akiwa bungeni baada ya kuchaguliwa alikuwa mtu makini, alikuwa anajenga hoja, anawakilisha mawazo ya wananchi wa chini, tulimpenda sana hata sisi tuliokuwa CCM, alikuwa anajenga hoja, alikuwa anachagua maneno ya kusema, huenda inatokana na kazi yake ya Upadre au kuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu.

“Kama kuna mtu mmoja kutoka upinzani ambaye tunaweza kusema alikuwa kwa ajili ya watu basi ni Dk.Slaa lakini mnafahamu na ndio maana baada ya kukaa huko upinzani na kuona upinzani mambo yalivyo aliamua kujitoa, wote ni mashahidi.

“Kwa kutambua uwezo wake na kwa kutambua kama kuna mpinzani mmoja katika wapinzani wote walioko Tanzania yeye alikuwa mpinzani wa kweli,”amesema Dk.Magufuli.

Ameongeza wakati anajenga barabara ya Karatu , Dk.Slaa alimuomba kutengeneza daraja , alikuwa mstaarabu, ni tofauti na wapinzani wanaonekana hivi ambao wakiingia bungeni badala ya kuwakilisha wananchi kwa kuwasemea matatizo yao wao wanaondoka.

“Tumepita kwenye Corona waliwakimbia wananchi, ukitangaza bajeti wao hawasapoti, mkiwa mnajadili maendeleo wao wanatoka.Sijawahi kuona katika maisha yangu Dk.slaa akiweka plasta mdomoni akiwa bungeni, hivyo kutokana na uwezo mkubwa wa mwana mapinduzi Dk.Slaa.

“Na kutokana na upendo mkubwa alionao kwa wananchi bila kubagua, niliamua kumteua kuwa Balozi wa kuniwakilisha katika nchi tisa za Ulaya.Wala hawakilishi nchi moja , anawakilisha nchi tisa wakati mabalozi wengine wanawakilisha nchi moja , mbili au tatu lakini kwa Dk.Slaa anawakilisha nchi tisa ambazo ni Swiden, Norway, Denmark, Iceland, Finland, Rativa, Estonia, Lithuania na Ukrane,”amesema Dk.Magufuli alipokuwa akimuelezea Dk.Slaa mbele ya wananchi hao.

Amefafanua sio wapinzani wote ni wabaya ila wapinzani wengi wabaya na ameshatoa mifano mingi, akimuelezea Anna Mghwira ambaye mwaka 2015 aligombea urais na wakati anafanya kampeni alihubiri amani, alihubiri upendo na umoja na upendo.

“Kuna maisha baada ya kampeni, kuna maisha baada ya uchaguzi, ndio maana baada ya uchaguzi nikamchukua kutoka Chama kingine na kumteua kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.Pia nimemteua Profesa Kitila Mkumbo kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Maji.Dk.Slaa hakutoka bungeni wakati wa bajeti aliweka mawazo yake,”amesema Dk.Magufuli.  

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here