Magufuli atoa pole vifo 14 ajali Singida

0

Na Mwandishi Wetu 

Rais Dk. John Magufuli amemtumia  salamu za rambirambi mkuu wa Mkoa wa Singida,  Dk Rehema Nchimbi kutokana na ajali  ya gari ilioua wa watu 14 iliyotokea jana Desemba 13, 2020 wilayani Ikungi.

Ajali hiyo ilitokea saa 9 alasiri  barabara kuu ya Dodoma Singida katika kijiji cha Mkiwa baada ya  basi dogo lililokuwa limebeba watu waliokuwa wanatoka Mwanza kwenda Itigi kugongana uso kwa uso na lori la mizigo lililokuwa likitokea  Dar es Salaam  kwenda  Kahama. Katika ajali hiyo watu watatu walijeruhiwa.

Taarifa iliyotolewa leo Jumatatu Desemba 14, 2020  na mkurugenzi wa mawasiliano ya rais Ikulu,  Gerson Msigwa inaeleza kuwa kiongozi mkuu huyo wa nchi amemtaka Dk Nchimbi kufikisha salamu zake za pole kwa wafiwa, ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na vifo hivyo na kwamba anaungana na familia hizo katika kipindi hiki cha majonzi.

“Nawapa pole wafiwa wote,  Mungu awatie nguvu, uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na wapendwa wenu, nawaombea marehemu wote wapumzishwe mahali pema peponi na majeruhi wote wapone haraka” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli amevitaka  vyombo vyote vinavyosimamia usalama wa barabarani, kuongeza jitihada za kuthibiti ajali hasa katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka kwa kuwa kumekuwa  kukitokea ajali nyingi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here