Magufuli aagiza waliohamia tume ya madini wakitokea TMAA wapunguziwe mishahara

0
Rais Dk. John Magufuli akizungumza na viongozi mbalimbali mara baada ya kumuapisha Naibu Waziri wa Madini Profesa Shukrani Manya katika hafla fupi iliyofanyika katika viwanja vya Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma leo Disemba 11, 2020
Na Mwandishi Wetu 

Rais John Magufuli ameagiza waliokuwa wafanyakazi wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) na kuhamishiwa Tume ya Madini (TMC) kupunguziwa mishahara yao waliyotoka nayo huko.

Ameeleza hayo leo Ijumaa Desemba 11, 2020 baada ya kumwapisha Naibu Waziri wa Madini, Profesa Shukrani Manya Ikulu jijini Dodoma.

Amesema wafanyakazi hao wamekuwa wakipokea mishahara mikubwa kuliko hata wakurugenzi wao.

“Mmehamishwa kule mmekuja na mishahara yenu, ile mishahara katibu mkuu kiongozi ipunguzwe kwa sababu wale walitakiwa wawe retrenched kwa sababu kazi waliyoifanya TMA ilikuwa ya ovyo lakini hatutaki kuhukumu ‘generally.”

“Haiwezekani wewe ukapelekwa kwenye Tume ya Madini kutoka kule na mshahara wa Sh milioni 10 ukamzidi hata mkurugenzi wako wakati hata sio mkurugenzi, ukamzidi hata executive chairman ambaye yuko hapo anapokea sijui Sh milioni 5, wewe una Sh milioni 10,” amehoji.

Amesema anayetakiwa kuzidiwa mshahara ni yeye ambaye anapokea Sh milioni 9 wakati mtu wa Mamlaka ya Mapato (TRA) anapata Sh milioni 15.

Amesisitiza kwamba lazima wafanye mabadiliko ya kanuni katika Tume ya Madini na kupunguza mishahara ya wafanyakazi hao. Amesema kama kuna mtu hataridhishwa na uamuzi huo aache kazi.

“Kama wapo ambao hawataki kuteremshwa, waache kazi,” amesema Rais Magufuli wakati akitoa maagizo kwa Katibu Mkuu Kiongozi, John Kijazi.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here