Magoti, wenzake wakiri, wahukumiwa kulipa fidia Mil. 17

0

NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewahukumu Ofisa wa Programu kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Tito Magoti (26) na mwenzake kulipa fidia ya Sh milioni 17.3 baada ya kukiri mashtaka yao kwa Mkurugenzi wa Mashtaka Tanzania( DPP).

Mahakama hiyo iliwapata na hatia ya kuongoza genge la uhalifu lililopelekea washtakiwa hao kujipatia fedha hizo kwa njia ya udanganyifu.

Pia mahakama hiyo imewahukumu adhabu ya kutokutenda kosa lolote la jinai kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia jana Januari 5, 2021.

Mbali na Magoti, mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 137/2019 ni Theodory Giyani (36) ambaye ni Mtaalamu wa Tehama.

Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Janeth Mtega ambaye alisema mahakama imewatia hatiani washtakiwa hao kama walivyoshtakiwa na hivyo kuwa hukumu adhabu hizo.

“Mahakama hii imewatia hatiani kama mlivyoshtakiwa hivyo mnatakiwa kulipa kiasi cha Sh 17,354,535  kama fidia kwa Serikali na pia mahakama hii inawahukumu adhabu ya kutokutenda kosa lolote la jinai ndani ya mwaka mmoja kuanzia leo,” alisema Hakimu Mtega.

Awali, jopo la mawakili wawili wa upande wa mashtaka likiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi akishirikiana na wakili wa Serikali Mwandamizi,  Wankyo Simon ulidai kuwa kuwa kesi hiyo iliitwa kwa ajili ya uamuzi baada ya washtakiwa kukiri mashtaka yao kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini( DPP).

Wakili Kadushi alisema washtakiwa hao walikuwa wanakabiliwa na mashtaka matatu, lakini baada ya kufanya majadiliano na DPP walifutiwa mawili na kubakisha shitaka moja ambalo ni kuongoza genge la uhalifu.

Akiwasomea shtaka hilo, wakili Simon alidai kuwa washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa la kuongoza genge la uhalifu.

Ilidaiwa katika tarehe tofauti kati ya Februari mosi na Desemba 17, 2019 jijini Dar es Salaam na  katika maeneo mbalimbali ya ndani ya nchi Tanzania,  mshtakiwa Magoti, Giyani na wenzao ambao hawajafikishwa mahakamani, kwa makusudi walishiriki makosa ya uhalifu wa kupanga kwa kumiliki programu za kompyuta iliyotengenezwa mahususi kwa ajili ya kufanya uhalifu na kupelekea kujipatia  fedha kiasi cha Sh 17.35 milioni.

Hata hivyo, kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, mawakili wa washtakiwa hao, Flugence Massawe, Jebra Kambole na Pacience Mlowe waliiomba mahakama hiyo kuwapunguzia adhabu kwa sababu ni vijana wadogo na wanategemewa na familia zao.

“Pia washtakiwa hawa walionyesha ushirikiano tangu siku ya kwanza walipofikishwa mahakamani hapa kwa mara ya kwanza na kwamba umri wao ukilinganisha na kiasi ambacho wameilipa Serikali kama fidia ni hela nyingi sana, hivyo tunaomba mahakama izingatia haya yote” alidai wakili Massawe.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here