Maajabu ya Ng’ombe aina ya Mpwapwa na kasi ya uzalishaji wenye tija

0

Na Dotto Kwilasa, DODOMA

KATIKA jamii ya kitanzania linaposikika neno Ufugaji au Wafugaji picha inayokuja kichwani kwanza ni Ngo’mbe.

Fikra ya kwanza haipeleki mawazo kwenye mbuzi, kondoo, nguruwe, sungura, kuku au mifugo mingine.

Maana yake ni kwamba ufugaji katika jamii yetu unapeperushwa na nembo ya Ngo’mbe.

Hata Serikali ikitangaza ongezeko la mapato kutokana na ufugaji, tunautizama mchango wa ng’ombe kwanza.

Itoshe kusema kwamba ,Ufugaji sasa ni fursa kubwa sana kutokana na ongezeko kubwa la uhitaji wa mifugo pamoja na mazao yake ambapo kwa bahati nzuri au mbaya ufugaji nchini umeegemea zaidi kwa jamii kadhaa zilizo zoeleka tangu awali kama jamii za kifugaji.

Kutokana na fursa hii wafugaji wamekuwa wakitumia ufugaji wao kwa ajili ya kujipatia kipato chao kinachokidhi mahitaji ya kila siku huku changamoto lukuki zikiikabili sekta ya ufugaji jambo ambalo hatuwezi kuliipuuza hata kidogo kwani kuchelewa kidogo tu tunaweza kukwamisha maendeleo zaidi katika sekta hii.

Hivyo basi kutokana na uhitaji mkubwa wa mifugo na mazao yake kuna namna mbili ambazo jamii na hasa wafugaji wanapaswa kuhakikisha wanafikia kukidhi mahitaji ya soko kwa Kuongeza idadi ya mifugo na Kuboresha mbinu za ufugaji.

KUONGEZA IDADI YA MIFUGO

Njia hii ndiyo ambayo wafugaji wengi wa asili wamekuwa wakiitumia kuhakikisha kwamba wanafikia hitaji la soko pamoja na kulinda tamaduni (kijamii) zao.

Hata hivyo ongezeko hili limekuwa na madhara makubwa katika mazingira kutokana na uharibifu unaotokana na ardhi kushindwa kustahimili ongezeko hili na kuleta madhara ya Mmomonyoko wa ardhi, uharibifu wa nyanda za malisho, vyanzo vya maji na huduma duni imekuwa ni changamoto kutokana na wingi wa mifugo, Sababu kama vile Mbegu duni za mifugo, Ukosefu wa elimu ya kutosha kwa wafugaji na Mabadliko ya tabia ya nchi.

Kutokana na hali hiyo,Taasisi ya Taifa ya utafiti wa mifugo kituo cha Mpwapwa (TALIRI) imeona haja ya kutengeneza uwezo kwa wataalam ili kuandaa utoaji huduma ya upandikizaji mimba changa na Mbegu bora za Ng’ombe kwa wafugaji hapo baadae Kama tathmini ya awali kwa ngazi ya kituo ili kuongeza Kasi ya uzalishaji wenye tija nchini.

Lengo ni kutumia teknolojia kwa wafugaji kuwa na wanyama wengi wenye tija kwa lengo la kuongeza vipato vyao na Uchumi wa Taifa kwa jumla ambapo tayari Mimba changa 34 za Ndama zimeweza kuzalishwa na kupandikizwa kwa Ng’ombe 34 katika kufanya mazoezi ya tathmini ya awali na wanasubiri matokeo.

Kwa mujibu wa Mtafiti muongozaji wa Mradi wa mifugo ambaye pia ni Dokta wa Mifugo Kabuni Thomas amesema kuwa dhima Kuu ya Mradi huo ni katika kusaidia uboreshaji wa Mbegu bora za Ng’ombe Nchini ambapo hatua zote zimekamilika Kama mpango kazi wa maabara katika kutengeneza uwezo kwa wataalam.

Amesema katika kuhakikisha kuwa wafugaji wananufaika,Taasisi hiyo imekuwa ikiwapa mafunzo ya upandikizaji wa Ng’ombe aina ya Mpwapwa ambao wana uwezo wa kutoa maziwa lita 5 mpaka lita 10 katika mazingira ya mfugaji ambayo ni zaidi ya Mara nne ya maziwa anayotoa ng’ombe wa Asili kwa siku.

“Matokeo hayo yametokana na ulishaji mzuri wa mchanganyiko wa mikunde na miti ambayo imeonekana kuongeza kwa kiwango kikubwa uzalishaji wa maziwa na nyama aina ya chotara Mpwapwa anaweza kuzalisha lita 3000 za maziwa kwa kipindi cha ukamuaji wake mmoja ambayo ni wastani wa lita 10 hadi 16 kwa siku na inategemea na atakavyotunzwa”anafafanua.

Naye Mtafiti idara ya Ng’ombe, Deogratius Masao amesema kuwa Teknolojia ya kuzalisha ng’ombe chotara lengo lake ni kuboresha mifugo Asili na kuwajengea wafugaji mazingira bora ili wajipatie kipato kizuri kupitia Teknolojia hiyo.

Serikali kupitia Tume ya Taifa ya sayansi na Teknolojia (COSTECH) imetumia jumla ya Shilingi Billioni 50 katika kufadhili Miradi ya utafiti na ubunifu nchini ambapo Miradi zaidi ya 100 imefadhiliwa na Asilimia 70 ya miradi hiyo imekamilika.

Taasisi ya Taifa ya utafiti wa mifugo kituo cha mpwapwa (TALIRI) imebainisha kuwa ng’ombe aina ya mpwapwa wanauwezo wa kutoa maziwa lita 5 mpaka lita 10 katika mazingira ya mfugaji ambayo ni zaidi ya Mara 4 ya maziwa anayotoa ng’ombe wa Asili.

Hayo yamebainishwa Leo wilayani mpwapwa jijini Dodoma na Kaimu mkurugenzi Taasisi ya Taifa ya utafiti wa mifugo kituo cha mpwapwa (TALIRI) Dk. Haruna Chawala ambapo amesema kuwa ulishaji wa mchanganyiko mzuri wa mikunde miti huongeza kwa kiwango kikubwa uzalishaji wa maziwa na nyama.

“Ng’ombe aina ya mpwapwa ni Tunu ya Taifa maana ng’ombe huyu ni matokeo ya utafiti uliolenga kuzalisha ng’ombe chotara kwa ajili ya nyama na maziwa kwa wingi katika mazingira kame” amesema Dk. Chawala.

Aidha,Dk. Chawala amesema kuwa ng’ombe aina chotara mpwapwa itaweza kuzalisha lita 3000 kwa kipindi cha ukamuaji wake mmoja ambayo ni wastani wa lita 10 hadi 16 kwa siku kutegemea na atakavyotunzwa.

Kwa upande wake Deogratius Masao Mtafiti idara ya ng’ombe amesema kuwa Teknolojia ya kuzalisha ng’ombe chotara ni kuboresha mifugo Asili na kuwajengea wafugaji mazingira bora ili wajipatie kipato kizuri kupitia Teknolojia hii.

“Halmashauri zote zenye wafugaji wengi zikifanya utaratibu wa kufikisha elimu ya teknolojia hii ngazi ya kijiji mpaka kata itawafanya wafugaji wavutiwe na ufugaji huu”. Amesema Deogratius masao.

Naye Mtafiti idara ya ng’ombe Boniface Paschal amebainisha kuwa ng’ombe aina ya mpwapwa aliyetokana na utafiti uliokusudia huzalisha bidhaa inayofaa kwa nyama na maziwa.

KUBORESHA MBINU ZA UFUGAJI

Kwa bahati mbaya mfumo huu sio tunaouona ukishamiri katika jamii tunazozitegemea kwa kiwango kikubwa katika sekta ya ufugaji.

Umekuwa ni mfumo unaoshamiri zaidi kwa wajasiriamali wanaowekeza katika ufugaji.

Maana yake ni kwamba mfumo huu haujaweza kushawishi wafugaji wetu wa asili yawezekana kabisa kwamba nguvu inayotumika kushauri wafugaji haijakidhi mahitaji.

Hivyo kwa kuliona hilo TARILI –Mpwapwa imeona vyema kuongeza nguvu kuendana na uhitaji kwa kutafuta njia mbadala kwa kuangalia jitihada za mfumo huu ambao unaendana kabisa na mabadiliko ya dunia kwa sasa.

Dk.Chawala anasema,mfumo huu Unaendana na hitaji la soko kwa kuzalisha mifugo na mazao yake bora kabisa kuweza kushindana katika masoko ya kimataifa Lakini pia vilevile ni mfumo rafiki kwa mazingira.

“Mfumo huu unahitaji mabadiliko ya kifikra kwa wafugaji na nguvu ya serikali na wadau wa mifugo kuhakikisha tunatoka katika ufugaji wa asili na kuingia mfumo huu wa kisasa”anasisitiza na kuongeza;

Ni mfumo wenye gharama sana lakini matunda yake ni makubwa zaidi kwa mfugaji,jamii na taifa kwa ujumla,”anasema Chaula.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here