Lema ahamia Canada kama mkimbizi wa kisiasa

0

Aliyekuwa mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema amehamia nchini Canada  baada ya kupata hadhi ya ukimbizi wa kisiasa (political assylum) akitokea Nairobi Kenya.

Hayo yameelezwa leo Alhamisi Desemba 10, 2020 na katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa wakati akizungumza na Mwananchi Digital.

Wakati Golugwa akieleza hayo, picha zinazosambaa katika mitandao ya kijamii zinamuonyesha mbunge huyo wa zamani akiwa kwenye ndege pamoja na mkewe, Neema na watoto wake watatu.

l

Novemba 8, 2020 Lema alidaiwa kukamatwa akikimbilia nchini Kenya pamoja na familia yake kwa kile alichoeleza ni kwa ajili ya usalama wake.

Gazeti la Standard la Kenya liliripoti kuwa Lema aliyekuwa mbunge wa Arusha Mjini 2010 hadi 2020 alikamatwa Ilbissil Kaunti ya Kajiado baada ya yeye na familia yake kuvuka kupitia mpaka wa Namanga.

Lema alikuwa ameondoka nyumbani kwake kwa teksi akifuatana na mkewe na watoto wao watatu na kushuka Namanga.

Gazeti hilo linaeleza kuwa Lema alisema mkewe aliwasilisha nyaraka kwa maofisa wa uhamiaji ambao walikataa kuzitia mhuri na kutaka wafuatane na Lema.

Lema alinukuliwa na The Standard akisema kuwa alikwenda ofisi za uhamiaji na hakuwa na hati ya kusafiria na kwamba alikuwa anamsindikiza mkewe kwa ajili ya kutafuta shule kwa ajili ya watoto wake.

Maofisa hao waliruhusu familia hiyo kuvuka mpaka wakati Lema aliomba ruhusa ya kwenda kubadili fedha za Kenya kumpa mkewe.

Mara tu alipovuka mpaka aliingia kwenye gari la wakili wake, George Luchiri Wajackoyah ambaye baadaye kupitia ukurasa wa mtandao wake wa kijamii alieleza kuwa Lema alikwenda Kenya kwa ajili ya kulinda uhai wake.

Mbunge huyo alikamatwa na polisi jijini Dar es Salaam Novemba Mosi, 2020 akiwa pamoja na mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe pamoja na aliyekuwa meya wa Ubungo, Boniface Jacob.

Polisi walieleza kuwa watatu hao walikuwa katika kikao huku wakiwatuhumu kupanga mipango ya kufanya maandamano yasiyo na kikomo kuanzia Novemba 2, 2020.

Maandamano hayo yalitangazwa na Mbowe, kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto mKabwe  pamoja na aliyekuwa mgombea urais wa Chadema, Tundu Lissu lengo likiwa kushinikiza uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, 2020 urudiwe kwa kuwa haukuwa huru na wa haki.

Lema, Mbowe na Jacob walipelekwa kituo cha polisi Oysterbay na kuachiwa kwa dhamana Novemba 3, 2020 huku wakitakiwa kuripoti kituoni kila watakapopangiwa

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here