Kuongeza unga kwenye maziwa kunavyoharibu soko

0

NA DOTTO KWILASA

MOJA ya changamoto ya bidhaa za Tanzania kukosa soko hasa la nje ni pamoja na nyingi kushindwa kukidhi viwango vya ubora vinavyotakiwa kutokana na kushindwa kufuata njia bora za uzalishaji zinazotakiwa na masoko hayo.

Miongoni mwa bidhaa ambazo zinapigiwa kelele hapa nchini maziwa ni miongoni mwa bidhaa yenye changamoto ya ubora kuanzia katika soko la ndani na hata masoko ya nje. Hii imekuwa ikiondoa imani ya wateja kwa bidhaa husika na wengi kuishia kununua maziwa yaliyosindikwa au ya unga kuepuka kero ya maziwa yaliyochakachuliwa.

Moja ya changamoto ya bidhaa hiyo ni wazalishaji kuongeza maji ili kupata faida kubwa. Licha ya uwepo wa vipimo vya kiwango cha maji katyika maziwa lakini si kila mtu anaweza kuwa navyo na badala yake maziwa yamekuwa yakipimwa kwa wauzaji wa jumla lakini wale wanaokwenda kuuza rejareja wanatumia mwanya wa kutokuwepo kwa upimaji kwa kuongeza maji. Sambamba na hilo upo pia mtindo wa kuongeza unga katika bidhaa hiyo.

Kutokana na vitendo hivyo Serikali imewataka wafugaji wenye mtindo wa kuongeza unga katika Maziwa kuacha kufanya hivyo kwani sio tu inaharibu biashara ya maziwa katika soko la ndani ya nchi bali hata soko la nje.

Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel anatoa onyo hilo alipotembelea Banda la Maonesho la Bodi ya Maziwa lililopo katika Viwanja vya Maonesho ya bidhaa za Viwanda yanayoendelea kufanyika katika Viwanja vya Maonesho vya Mwl. Nyerere jijini Dar es Salaam.

Kaimu Msajili wa Bodi ya Maziwa, Noely Byamungu (kulia) akimueleza jambo Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi(Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (wa kwanza kushoto) alipotembelea banda la Maonesho la Bodi hiyo katika Maonesho ya Bidhaa za Viwanda yanayofanyika katika Viwanja vya Mwl. Nyerere (sabasaba) jijiji Dar es Salaam

Prof. Gabriel anasema wanaofanya hivyo wanapaswa kutambua kuwa kitendo hicho ni kibaya, wanajidanganya wao wenyewe na wasipo jirekebisha wataishia pabaya.

“Bodi endeleeni kutafuna wale wote ambao wanaochakachua maziwa kadri iwezekanavyo na sheria ichukue mkondo wake na hatutakuwa na huruma yeyote kwa sababu wanaharibu taswira nzima ya biashara ya maziwa ndani na nje ya nchi,” anasema.

Anaongeza kwa kusema kuwa Wafugaji wajue kwamba Serikali ina vipimo ambavyo vinaweza kutambua maziwa yaliyowekwa unga na hivyo anawataka wale wote wanaojihusisha na uhalifu huo kuacha kufanya hivyo kwani watakaokutwa sheria itachukua mkondo wake.

Aidha, Prof. Gabriel anaitaka Bodi ya Maziwa kuhakikisha unywaji wa maziwa unaongezeka na wawahamasishe Watanzania kadri iwezekanavyo walau ndani ya miaka mitano ijayo wazidi  lita zaidi ya 100 kwa mwaka kwani kwa sasa unywaji upo kwenye lita 54 jambo ambalo ni aibu kwa nchi yenye ng’ombe milioni 33. 4 na inazalisha lita za maziwa bilioni 3.01 huku kukiwa na viwanda vya kuchakata maziwa 99.

“Bodi fanyeni kazi ya ziada, msifanye kazi kwa mazoea, wekeni sayansi kwenye kazi yenu na pia pimeni elimu mliyoitoa imeeleweka kiasi gani ili wale wanaofanya vizuri muwapongeze na wale wanaokosea muwaadhibu kwa mujibu wa sheria na taratibu ili kuifanya tasnia iwe bora zaidi,” anaongeza Prof. Gabriel.

Kwa upande wake Kaimu Msajili wa Bodi ya Maziwa, Noely Byamungu anasema kuwa wamejipanga kuhakikisha wanajenga utamaduni kwa jamii kupenda kunywa maziwa na wameanza na kundi la wanamichezo lakini kuna mpango mkakati wa kitaifa wa kuwafikia Watoto mashuleni.

“Mpango wa kitaifa unalenga kukuza utamaduni wa unywaji wa maziwa kwa Watoto wadogo na kwa kufanya hivyo kutasaidia kujenga jamii inayopenda kunywa maziwa, hivyo tunawaomba Waandishi wa Habari mtusaidia kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa unywaji wa maziwa ili tuwe na jamii inayopenda kunywa maziwa kwa afya,” anasema Byamungu.

Anaongeza kwa kusema kuwa katika kutekeleza mpango huo Bodi itashirikisha wadau tofautitofauti ikiwemo Wizara ya TAMISEMI, Wizara ya Afya na Wizara ya Elimu na Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili kuhakikisha unywaji wa maziwa unaongozeka lakini pia wafugaji wazalishe na waweze kupata masoko ya uhakika.

JAMII YASHAURIWA KUNYWA MAZIWA KWA WINGI

Mpaka sasa kuna Viwanda 99 vya Maziwa nchini na maziwa ambayo yanazalishwa sasa kwa mwaka 2020 yamefikia lita Bilioni 3.01.

Prof.Elisante anasema uchakataji wa maziwa bado unahitajika kuongezeka zaidi kwasababu ulaji wa maziwa upo.

“Mpaka sasa ng’ombe milioni 2 nchini huzalisha maziwa hivyo tunampango wa kuongeza ng’ombe wa maziwa zaidi bado tunaamini wigo bado upo”. anasema Prof.Elisante.

Anasema ili uzalishaji na uchakataji uongezeke lazima soko la ndani na nje liweze kuwa kubwa.

Aidha, Prof.Elisante anasema unywaji wa maziwa nchini kwa siku ni zaidi ya lita milioni 8.3.

Pamoja na hayo anawataka wenye Viwanda kuongeza ubora wa uzalishaji wa maziwa ili kuweza kumnufaisha mnyaji wa maziwa nchini.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, anawataka wananchi kupendelea kunywa maziwa kwasababu yana protini, wanga na virutubisho vingi vinavyosaidia kuimarisha afya.

Nae Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TANTRADE Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade Latifa Khamis anasema wataendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kama vilabu vya Jogging na wengine wengi kuzalisha bidhaa zilizobora hapa nchini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here