Kuna maisha baada ya uchaguzi- Magufuli

0

NA HAFIDH KIDO, DODOMA

ILI kuimarisha amani, utulivu na mshilamano kwa maslahi ya nchi wananchi wametakiwa kuelewa kuna maisha baada ya uchaguzi.

Hayo yamesemwa jana na mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli wakati akizungumza na wazee wa Jiji la Dodoma katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete jijini humo jana.

Alisema kwa kipindi chote cha kampeni ndani ya siku 60 nchi ilikuwa na amani ya hali ya juu hivyo isiharibiwe kwa siku chache zilizobakia.

“Ndugu zangu kuna maisha baada ya uchaguzi, tusivuruge amani yetu kwa thamani ndogo. Tutambue nchi yetu ni kubwa kuliko vyama vya siasa. CCM tulianza kampeni Agosti 29 hadi leo (jana) Oktoba 27 tumekutana na wanachi nchi nzima.

“Tulifanya kampeni za kistaarabu na za kisayansi kwa kushirikiana na Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na Rais wa Zanzibar pamoja na viongozi wastaafu. Ndiyo maana CCM tumekuwa na uwezo wa kusimamisha wagombea wa ngazi zote nchi nzima, hakuna chama kilichoweza haya,” alisema Dk. Magufuli.

Alibainisha, serikali yake ikipewa dhamana ya kuongoza nchi kwa miaka mingine mitano itaipeleka Tanzania katika uchumi wa kisasa kwa sababu nchi kwa sasa ina nidhamu ta makusanyo na matumizi pamoja na ujenzi wa miundombinu ikiwemo reli ya kisasa na ufufuaji reli ya Kaskazini kutoma Dar es Salaam hadi Arusha.

“Mambo yote haya yanahitaji mtu anayehubiri amani na kumtanguliza mbele Mungu. Kamwe tusiwachague viongozi wanaohubiri kutugawa kikabila, kikanda na kidini,” alisema Dk. Magufuli na kubainisha:

“Ndiyo maana nawaomba kura vyama vyote vya siasa. Nataka taifa hili tusimame pamoja, tusikubali kuchonganishwa na yeyote iwe kwa njia ya mitandao ya kijamii au mtu mmoja mmoja. Ukishapiga kura nenda nyumbani tuwaachie kazi ya kuhesabu kura NEC (Tume ya Taifa ya Uchaguzi).”

Katika hatua nyingine Dk. Magufuli aliitangaza siku ta leo kuwa ya mapumziko ili wananchi wapate nafasi ya kupiga kura.

Hii ni ahadi aliyowapa Watanzania baada ya kuingia madarakani ambapo alitaka waumini wa dini zote wasikose nafasi ya kuabudu kwa sababu ya uchaguzi. Hivyo, siku ya kupiga kura ikawa Jumatano badala ya siku za mwishoni mwa wiki kama ilivyozoeleka.

Awali, Katibu Mkuu wa CCM Dk. Bashiru Ally akiwa katika mkutano huo alisema CCM inawashukuru wazee wa Dodoma kwa kuwa wamekuwa wakiwapokea makada wa chama hicho tangu walipoanza mchamato wa uteuzi ndani ya chama hadi kupitishwa majina ya wagombea na hata walipoanza kampeni Agosti 29 mwaka huu walianzia Dodoma na jana Oktoba 27 siku ya kufunga kampeni wamefungia Dodoma.

“Nidhamu ya chama ipo imara kwa kuwa kwa kipindi chote ndugu Mwenyekiti tulifuata maelekezo yako ya kunadi sera nzuri na ilani ya chama chetu kwa kuegemea hoja badala ya majibizano,” alisema Dk. Bashiru.

Kwa upande wake akiwakilisha wazee wa Dodoma, Waziri Mkuu Mstaafu Mzee Samuel Malecela alisema kitu kinachomfurahisha akiwa miongoni mwa wazee wa Dodoma ni kuona mabadiliko makubwa ya jiji hilo ndani ya kipindi kifupi cha miaka mitano.

“Nchi yetu imekuwa na bahati kubwa ya kuwa na kiongozi wa namna hii, kiongozi mzalendo, mchapakazi na anayemuogopa Mungu. CCM huwa hatubahatishi kwenye kupata viongozi,” alisema Mzee Malecela na kusisitiza:

“Tulipokuchagua mwaka 2015 ilikuwa kwa ajili ya kukaa miama 10, hivyo haya mapumziko ni kama kituo cha kuongezea kasi treni.”

Jana CCM ilihitimisha kampeni zake nchi nzima kwa ngazi ya urais, ubunge na udiwani pamoja na nafasi nyingine kwa upande wa Zanzibar. Ambapo wamewafikia wananchi wote nchi nzima kwa kutumia mbinu mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii, mikutano ya hadhara, kuzungumza na makundi maalum pamoja na vyombo vya habari.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here