Kuhusu uwekezaji katika madini ya chuma, mbunge wa Ludewa ampongeza Rais Magufuli

0

Na John Simwanza, Ludewa

Mbunge wa Ludewa Mkoani Njombe, Joseph Kamonga amempongeza Rais Dk. John Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya kuwaletea wananchi na taifa maendeleo huku akieleza kubwa ambalo amefurahishwa nalo ni uwekezaji katika uchimbaji wa madini chuma yanayopatikana maeneo mnbalimbali nchini ikiwamo eneo la Liganga mkoani humo.

Akizungumza baada ya kumuapisha Prof. Shukrani Manya kuwa Naibu Waziri wa Madini katika hafla fupi iliyofanyika katika viwanja vya Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma, Disemba 11, 2020 Rais Magufuli alihoji kwanini madini ya chuma yanayopatikana maeneo mbalimbali nchini hayachimbwi na kutumika.

Rais Magufuli  alisema ; “Tanzania ina madini ya kila aina, kuna madini ya chuma, kwa nini chuma hakitumiki kutengeneza nondo badala yake vyuma vya reli ndiyo vinatumika?. Sekta ya madini ni sekta muhimu, mkijipanga vizuri mkahusisha wataalamu vizuri, mkashirikiana kweli kweli mkiamua sekta ya madini inaweza kutoa mchango mkubwa kwa Taifa hili.”

Kamonga alitoa pongezi hizo jana Disemba 14, 20202 wakati aliposhuhudia kwa mara ya kuapishwa kwa Baraza jipya la Madiwani na ufunguzi wa baraza hilo ambapo pia ulifanyika uchaguzi na wise Wise Mgina alichaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa Halmashauri hiyo.

Alisema kuwa kama watu wanataka kwenda kuwekeza kwenye upande wa madini ya chuma Ludewa wapewe maeneo  haraka na ikiwezekana wapewe hata bure.

“Mimi kama mbunge nilifurahishwa na kauli hiyo ya rais kwasababu katika jimbo langu la Ludewa kuna madini mengi ya chuma ambayo kimsingi ndiyo yanatumika kwenye kuzalisha chuma hivyo naiomba serikali kuja kuwekeza hapa.

“Ndugu zangu sisi sote ni mashahidi kwamba Ludewa katika nchi yetu ndiyo kuna madini mengi ya chuma kama Liganga, lakini tuna makaa ya mawe eneo la Mchuchuma na pia kuna madini aina ya chokaa ni fursa kubwa tunayo na tunakuomba mkuu wa mkoa (RC Njombe, Mwita Rubrya),” alisema.

Aidha mbunge huyo ambaye kitaaluma ni Wakili amewahi kuwa mtumishi wa idara ya Ardhi na baadae kuwa Kamshna wa ardhi jijini Dodoma hivyo aliwataka watalaamu na watumishi wa serikali ndani ya halmashauri hiyo kushirikiana naye kwani yeye alikuwa kwenye idara mbalimbali za utumishi hivyo yeye yupo na simu zake zipo wazi wakati wote.

Kamonga  alifafanua kuwa ndani ya halmashauri hiyo kuna changamoto mbalimbali hivyo kubwa zaidi ni kwenda kushirikiana katika ukusanyaji wa mapato huku akimpongeza Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Sunday Deogratius kwa kazi kubwa anayoifanya.

“Ndugu yangu Mkurugenzi nakupongeza Sana kwani umejitahidi kukusanya mapato kwenye halmashauri yetu na tangu umefika kila mwaka mapato ya halmashauri yetu yanazidi kuongezeka na umeniambia kwamba mwaka ujao umepanga kukusanya zaidi ya bilioni moja.” alisema na kuongeza kuwa;

“Hadi sasa katika kipindi cha nusu  mwaka umeweza kukusanya asilimia 55 ya mapato na umenihakikishia kwamba lengo ni bilioni  moja hivyo nakupongeza sana na kwakweli unafanya kazi kubwa Sana.”alisema Mbunge huyo.

Kamonga alisema yeye na Mbunge wa viti maalum mkoa wa Njombe, Balozi Pindi Chana watashirikiana kwa pamoja katika kuhakikisha kwa pamoja wanaijenga Ludewa

Naye katibu tawala wa wilaya hiyo, Zaina Mlawa aliwaeleza madiwani wa upinzani kwamba kwakuwa wamechaguliwa kuwa madiwani wajuwe kuwa wanatekeleza Ilani ya chama Cha Mapinduzi huku akiwataka madiwani wateule kwenda kushirikiana na watendaji kata lakini pia kuwa na maadili katika uongozi wao kwani ni kioo Cha Jamii.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here