Kotei atajwa kurejea Simba

0

NA MWANDISHI WETU

KUNA tetesi kuwa uongozi wa Simba upo kwenye mchakato wa kuongeza kiungo mkabaji ndani ya timu hiyo ambayo inaiwakilisha Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu wa 2020/21 na itaanza kibarua chake kati ya Novemba 27-29.

Simba imepangwa kucheza na Klabu ya Plateu United kutoka Nigeria mchezo wa kwanza itakuwa ugenini na ule wa pili utachezwa Uwanja wa Mkapa kati ya Desemba 4-6.

Kwa sasa mabingwa hao watetezi kwenye nafasi ya kiungo mkabaji wanamtumia Jonas Mkude, Said Ndemla na Mzamiru Yassin huku wakiikosa huduma ya raia wa Brazil, Gerson Fraga ambaye atakuwa nje kwa msimu mzima.

Nyota anayetajwa kurejeshwa kundini ni James Kotei ambaye ana tuzo ya mchezaji bora ndani ya Simba kwa upande wa viungo aliyoitwaa msimu wa 2018/19 kwenye tuzo za Mo Award.

Pia kwenye mchakato wa kuachwa kwa kiungo huyo ambaye alitimkia Afrika Kusini kuliibuka mvutano mkubwa kabla hajasajiliwa na Klabu ya Kaizer Chief na kwa sasa yupo zake FC Slavia anapewa nafasi ya kurejea tena.

“Kwa sasa Simba ipo kwenye mpango wa kumrejesha kiungo wao mkata umeme  namba moja, Kotei, (James) ambaye wakati anaondoka bado kocha alikuwa anahitaji huduma yake,” ilieleza taarifa hiyo.

Kocha Mkuu wa Simba Sven Vandenbroeck, aliweka bayana kuwa wanahitaji umakini katika kusaka ushindi kwenye mechi zao za Ligi ya Mabingwa Afrika.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here