Kocha: Mashabiki Yanga subirini utamu zaidi

0

Na Mwandishi Wetu

Kocha wa Yanga, Cedric Kaze, amesema mambo makubwa yanakuja na mashabiki wa klabu hiyo wasubiri kushuhudia sapraizi nyingine kubwa zaidi kutoka kwa timu hiyo.

Kocha huyo aliyetua Jangwani hivi karibuni kuchukua nafasi ya Zlatko Krmpotic wiki chache zilizopita alisema baada ya kuacha vilio mjini Musoma bado hajaridhika hadi azibebe tena pointi tatu kutoka kwa Gwambina ili atimize lengo la kuondoka na alama tisa Kanda ya Ziwa.

Kaze ameshavuna alama sita kwa mechi mbili za awali ugenini Kanda ya Ziwa akitwaa kwa KMC waliohamishia pambano hilo jijini Mwanza na kuwafumua mabao 2-1 na juzi tena kuwanyoosha Biashara United kwa kuwalaza bao 1-0 mjini Musoma mkoani Mara.

Kocha huyo alisema kwa sasa anaona kuna mabadiliko kwa vijana wake, lakini atafurahi zaidi kama atavuna pointi tatu dhidi ya Gwambina wanaovaana nao kesho Jumanne.

Licha ya Kaze kuamini vijana wake wamebadilika, lakini bado kikosi hicho kimekuwa kikicheza kama ilivyokuwa chini ya Zlatko na hata matokeo yake ni yale ya mabao kiduchu, japo eneo la kiungo chini ya Mukoko Tonombe ikituliza mpira na kupiga pasi za mbele.

Ushindi wa juzi umeifanya Yanga kufikisha pointi 22 na kulingana na Azam ila wakitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa, Azam ikiwa na kileleni, lakini Jangwani ikiendeleza rekodi ya kushinda mechi saba mfululizo bila kupoteza.

Akizungumza mara baada ya mcheza wao na Biashara, Kaze alisema kwa sasa hawakumbuki tena matokeo yaliyopita isipokuwa wanaziwaza pointi tatu dhidi ya Gwambina, akisisitiza kuwa mambo bado kabisa kwake katika kuhakikisha timu inapiga soka tamu na kupata matokeo
mazuri.

Alisema licha ya wapinzani kupoteza mechi iliyopita kwa kuruhusu mabao mengi, haiwezi kuwafanya Yanga kudharau wapinzani hao badala yake wanaenda kwa umakini kuhakikisha wanapata ushindi.

“Hata Gwambina walianza vizuri japo mechi iliyopita walipoteza hivyo hatuwezi kuwadharau, tunachotaka ni ushindi ili kuendelea kujiweka kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu na kuweka rekodi zaidi, kwani nasikia hapa Musoma Yanga ilikuwa haijawahi kushinda,” alisema Kaze anayeenda kukutana na aliyewahi kuwa Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Ufundi wa Gwambina inayoshika nafasi ya 14 kwenye msimamo ikiwa na alama 9 tu kwa michezo yake tisa.

Hata hivyo Kocha hiyo hakusita kuweka wazi ugumu wa ligi ulivyo na kwamba anaamini kujituma
kwa nyota wake itawasaidia kufikia malengo yao na kueleza kuwa juzi waliupiga mwingi.

Pia Kaze alieleza kuwa winga wake, Ditram Nchimbi aliyeumia wakati wa mchezo wao na Biashara, haitamweka sana nje kwani hayakuwa maumivu makubwa ambayo yanaweza kumzuia kuendelea na kazi yake.
“Leo (juzi) nimefurahishwa na kiwango cha wachezaji wangu, ligi ni ngumu lakini wanapambana kuona timu inapata ushindi, kuhusu Nchimbi ni maumivu ya kawaida na haitamweka sana nje” alisema kocha huyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here