KMC yamuombea radhi Kabunda “Hakulenga kuidhihaki Yanga”

0

NA MWANDISHI WETU

IKIWA vitendo vya kibaguzi vinapigwa vita michezoni hivi karibuni mchezaji wa KMC Hassan Kabunda alizua mijadala baada ya kitendo chake cha kushangilia huku akiwa amevaa kinyago chenye mfano wa nyani usoni.

Baadhi ya mashabiki walishangaa na kuhoji kitendo hicho huku wakimwiita mchezaji huyo, limbukeni na asiyejitambua.

Hata hivyo, baadhi ya mashabiki walikerwa na mchezaji huyo wakidai kuwa huenda alikuwa anaungana na aliyekuwa Kocha wa Yanga Luc Eymael ambaye alifulushwa kazi baada ya kuwaita Watanzania Manyani.

Lakini baadhi ya Watanzania bila kujijua wamekuwa wakionekana kuendelea kuiunga mkono kauli hiyo ya kibaguzi iliyotolewa na mzungu huyo ambaye aliwadharau Watanzania wote bila kutofautisha huyu ni wa klabu gani.

Baada ya mijadala hiyo kupamba moto Uongozi wa Klabu ya KMC umeibuka na umemuombea radhi mchezaji wake Hassan Kabunda kwa kitendo hicho cha kushangilia na kinyago usoni baada ya kuifunga Yanga SC katika uwanja wa CCM Kirumba Mwanza.

KMC inaeleza kuwa Kabunda hakuwa na dhamira yoyote ya kuonesha vitendo vya ubaguzi wa rangi au dhihaka kwa Yanga kama baadhi ya watu walivyotafsiri.

“Tunaomba radhi kwa wote waliosumbulika kwa kitendo hicho cha ushangiliaji wa goli uliofanywa na mchezaji wetu na nasisitiza kuwa haukuwa na nia mbaya kwa wapinzani bali ni furaha ya kufunga goli iliyosababisha kufanya hivyo.

“KMC inaungana na TFF, TPBL na vilabu vyote katika kukemea vitendo visivyo vya kiungwana kuoneshwa katika mchezo wa mpira wa miguu kwani michezo ni furaha,”ilisema sehemu ya taarifa yao kwa vyombo vya habari na kusainiwa na Kaimu Katibu Mkuu KMC.

Uamuzi wa uongozi wa KMC umepokelewa kwa mikono miwili na wadau wa soka kwamba umekuwa wakiungwana huku baadhi ya wadau wa soka wakitahadharisha kuwa hata baadhi ya viongozi wawe makini na vitendo kama hivyo hususan wale wanao kuwa kwenye benchi.

Ikumbukwe katika mchezo huo, Yanga SC walitoka nyuma na kushinda mabao 2-1 dhidi ya wenyeji wahamiaji, KMC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza.

Ushindi ambao, uliwafanya mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi Kuu, kufikisha pointi 19 katika mchezo wao uliokuwa wa saba, ingawa wanabaki nafasi ya pili, nyuma ya vinara, Azam FC waliokusanya pointi zote 21 kipindi hicho, katika mechi saba wakati mabingwa Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Ramadhan Kayoko aliyekuwa anasaidiwa na Hamisi Chang’walu na Abdul Malimba wote wa Dar es Salaam KMC walitangulia kwa bao la Hassan Salum Kabunda dakika ya 27.

Kabunda, mtoto wa beki wa Yanga SC miaka ya 1990, Salum Kabunda, sasa marehemu alimtungua kipa Metacha Boniphace Mnata kwa shuti kali la umbali wa mita 22 baada ya kuwahadaa walinzi wa Yanga kufuatia kupokea pasi ya kiungo mwenzake, Kenny Ally Mwambungu.

Kiungo Tuisila Kisinda kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) akaisawazishia Yanga SC kwa mkwaju mzuri wa penalti dakika ya 41 akimchambua kipa mkongwe Juma Kaseja kufuatia mshambuliaji Mghana, Michael Sarpong kuangushwa kwenye boksi.

Kipindi cha pili, Yanga SC wakafanikiwa kupata bao la ushindi kupitia kwa mshambuliaji wake mpya, Waziri Junior aliyemalizia kwa kichwa kona ya mtokea benchi Farid Mussa Malik dakika ya 61.
Baada ya kufunga bao hilo, Waziri, alivua jezi kuonyesha fulana iliyoandikwa “The King of CC Kirumba Stadium’, akimaanisha yeye ni Mfalme wa Uwanja huo kutokana na rekodi yake ya mabao tangu akiwa anachezea Toto Africans na Mbao FC zote za Mwanza ambazo zimeshuka Daraja.
Mechi nyingine za Ligi Kuu siku hiyo zilikuwa; Biashara United imeshinda 1-0 dhidi ya wenyeji, Polisi Tanzania bao pekee la Deogratius Judika Mafie dakika ya 53 Uwanja wa Karume, Musoma mkoani Mara.

JKT Tanzania ikaichapa 6-1 Mwadui FC Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga mabao ya timu ya Jeshi la Kujenga Taifa yakifungwa na Adam Adam matatu dakika ya 24, 48 na 82, Danny Lyanga dakika ya 40 na 52 na Said Luyaya dakika ya 90 na ushei, wakati la wenyeji limefungwa na Pastory Athanas dakika ya 62.


Kikosi cha KMC kilikuwa; Juma Kaseja, Israel Mwenda, David Bryson, Lusajo Mwaikenda, Andrew Vincent ‘Dante’, Jean Baptiste Mugiraneza/Cliff Buyoya dk85, Abdul Hillary/Martin Kiggi dk73, Kenny Ally, Paul Peter, Emmanuel Mvuyekure na Hassan Kabunda/Relliants Lusajo dk.
Yanga SC; Metacha Mnata, Kibwana Shomary, Yassin Mustapha, Lamine Moro, Bakari Mwamnyeto, Mukoko Tonombe, Deus Kaseke/Farid Mussa dk59, Feisal Salum, Michael Sarpong, Waziri Junior/ Haruna Niyonzima dk82 na Tuisila Kisinda/Abdallah Shaibu ‘Ninja’ dk89.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here