Kituo cha Mbezi Luis kitavyotoa fursa za kiuchumi kwa wananchi

0

>Kutumiwa na zaidi ya mabasi  ya abiria 1,000

>Yamo pia mabasi yanayoenda nchi za jirani

 NA AZIZA MASOUD, DAR ES SALAAM

MRADI wa stendi  ya mabasi  yaendayo mikoani na nchi jirani Mbezi Luis  ni  miongoni mwa miradi mikubwa iliyopo jijini Dar es Salaam inayotekelezwa na serikali ya Rais Dk.John Magufuli.

Mradi huo ambao ulianza kujengwa mwanzoni mwa mwaka jana ni mbadala wa kituo cha mabasi Ubungo  ambacho kwa sasa  kinaonekana kuwa kidogo kulingana  kuongezeka kwa idadi ya watu  wanaosafiri  na kukua kwa eneo husika.

Oktoba nane mwaka huu Rais Dk.Magufuli  akiwa na rais wa  Malawi Dk. Lazarus Chakwera  waliweka jiwe la msingi  la ujenzi wa kituo hicho  kinachojengwa na  mkandarasi ‘Hainan International Limited’.

Dk.Magufuli amemtaka mkandarasi huyo kuhakikisha ifikapo Novemba 30 mwaka huu kuhakikisha ujenzi wa kituo hicho uwe umekamilika.

Amesema kuwa iwapo Mkandarasi huyo atachelewa kufanya hivyo atapaswa kukatwa fedha kwa kuwa hakuna sababu ya msingi inayozuia ukamilishwaji wa mradi huo kwa wakati.

Rais Magufuli ambaye pia ameagiza ndani ya kituo hicho cha mabasi kuwepo na ofisi ya Uhamiaji kwa kuwa kitakuwa na mabasi yanayoingia na kutoka nchi jirani na pia uwekwe mgawanyo mzuri wa maeneo ya maegesho ya magari ikiwa ni pamoja na kutenga eneo la mabasi yaendayo nje ya nchi, mabasi yaendayo mikoani, teksi, bodaboda na bajaji.

“Nimeambiwa hapa pakikamilika patakuwa na uwezo wa kuhudumia mabasi ya abiria 1,000, teksi 280 kwa siku,patakuwa na maeneo ya bodaboda na bajaji na patakuwa na eneo la mamalishe na babalishe”, Alifafanua Rais Magufuli.

Kauli ya Dk.Magufuli imeonekana kuongeza kasi kwa mkandarasi huyo ambapo mwanzoni  mwa wiki hii  Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Aboubakar Kunenge  ametembelea eneo hilo ili kuangalia maendeleo ya ujenzi wa stendi hiyo  ambapo alidai kuwa unaridhisha.

Kunenge amesema kituo hicho kikuu cha mabasi kitaanza majaribio ya kwanza November 25 na kuanza kutumika rasmi November 30, mwaka huu.

Kutokana na kuanza kwa ujenzi huo Kunenge ametoa wito kwa wananchi na wafanyabiashara kuchangamkia fursa zinazopatikana kituoni hapo.

“Wananchi wanatakiwa kuchangamkia fursa kwenye standi hiyo ikiwemo fremu za maduka, migahawa, ofisi, huduma za kifedha, supermarket, ofisi za kukata tiketi na hoteli.

“Zoezi la kutuma maombi ya kufanyabiashara katika standi hiyo limeanza leo November 9 na linatarajiwa kufungwa Novemba 25, mwaka huu,” amesema Kunenge.

Aidha, Kunenge amesema uwepo wa kituo cha mabasi  hiyo utaendelea kufungua fursa za maendeleo kwa wakazi wa Ubungo hivyo amewataka kujiandaa kwa hilo.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Halmashauri Jiji la Dar es Salaam, Sipora Liana amesema mradi wa huo kituo upo katika hatua za mwisho za kukamilika kwake.

“Kama mnavyoona mradi umefikia hatua za mwisho na tarehe 30 ya mwezi huu utakuwa umekamilika kwa hatua ya kwanza kama ambavyo Mheshimiwa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli aliagiza mradi huo uwe umekamilika hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Novemba” Amesema Liana.

Liana ameongeza kuwa kuanzia tarehe 25 ya mwezi huu mabasi yataanza kutumia Kituo cha Mabasi cha Mbezi Luis huku akiwataka wafanyabishara mbalimbali ambao wanataka kutumia fursa ya kufanya biashara katika Kituo hicho wajitokeza kufanya maombi.

Aidha, Liana amewataka wafanyabiashara ambao wanataka kufanya biashara katika Kituo hicho kuepuka matapeli ambao wanatumia mwanya huo kuwatapeli wafanyabiashara huku akiwasihi waombaji kufuata utaratibu ambao umewekwa wa kuomba kupitia mtandao kupitia anuani www.pangisha.tamisemi.go.tz kuanzia tarehe 09 Novemba, 2020.

Mkurugenzi Liana pia amezungumzia gharama halisi ya mradi huo kuwa ni Sh bilioni 50.9 ambazo zilitengwa hapo awali na kufafanua kwamba hakutakuwa na nyongeza ya fedha kwenye mradi huo.

“Nawaambieni mpaka sasa tumeweza kuokoa zaidi ya shilingi za Kitanzania bilioni 12 katika hizo bilioni 50.9 zilizotengwa kutokana na usimamizi dhabiti wa mradi huo kwa kuzingatia maelekezo ya Rais Magufuli katika kusimamia fedha za Serikali na sisi Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam tumesimamia na kuweza kuokoa fedha hizi” amesema Liana.

Liana ameendelea kueleza kwamba mradi huo ukikamilika utaweza kuingizia mapato Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam zaidi ya Sh Bilioni 10 kwa mwaka.

Aidha, amesema Kituo Kikuu cha mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani katika eneo la Mbezi Luis kitaweza kutoa ajira kwa Watanzania zaidi ya elfu kumi na kuchochea uchumi kwa Watanzania na taifa kwa ujumla.

Mkurugenzi Liana amehitimisha kwa kueleza changamoto ya ucheleweshaji wa vifaa kulikotokana na mlipuko wa ugonjwa COVID-19 unaotokana na virusi vya CORONA na kupelekea makampuni ya nje kushindwa kuzalisha bidhaa kutokana na ugonjwa huo.

Rais Dk. John Magufuli akiwa na Rais wa Malawi Dk. Lazarus Chakwera walipoweka jiwe la msingi la ujenzi wa kituo hicho Oktoba nane mwaka huu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here