Kilimanjaro haturudii makosa

0

NA HAFIDH KIDO, MOSHI

KATIKA hali isiyo ya kawaida wananchi katika Mkoa wa Kilimanjaro Kanda ya Kaskazini wamemuomba msamaha mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk. John Magufuli tangu alipoingia katika mkoa huo juzi kufanya mikutano ya kampeni.

Jana akiwa Wilaya ya Mwanga wakati akitokea Wilaya ya Same mkoani humo, Dk. Magufuli alipokewa na wananchi mchanganyiko huku mkononi wameshika majani maalum ‘Masale’ ambayo kwa utamaduni wa kabila la Wachaga mtu anayeomba radhi akibeba majani hayo kwa kiasi kikubwa anasamehewa.

Aidha,baada ya kufanya mkutano mkubwa wilayani Mwanga, Dk. Magufuli alikuwa na mikutano mingine midogo miwili katika maeneo ya Himo, Kiboroloni na Mgagao kabla ya kufika Moshi Mjini na kufanya mkutano mkubwa katika viwanja vya Chuo cha Ushirika.

Kote huko njiani alilakiwa na wananchi walioshika majani ya Masale huku wakipaza sauti zao kuwa wamekosa wanaomba wasamewe hawatarudia kuchagua wapinzani kwa kuwa hawakuwa na tija kwao wala hawakujali maslahi ya wanyonge.

“Nimeona njiani nikiingia Mkoa huu wa Kilimanjaro wananchi wameshikilia majani wanaomba msamaha, mimi nilishawasamehe siku nyingi makaribisho haya niliyoyapata inaonyesha Kilimanjaro mna jambo lenu.

“Nina hakika katika hawa waliohudhuria kuna watu wa vyama mbalimbali si CCM peke yake, kuna dini na makabila mbalimbali,” alisema Dk. Magufuli na kuongeza:

“Kilimanjaro ni tajiri, mti mrefu kuliko yote  unapatikana hapa, mlima mrefu kuliko yote Afrika unapatikana hapa Kilimanjaro, mnahitaji kiongozi atakayetumia utajiri huu wa maliasili kuwanufaisha Watanzania, ambapo mimi nimeshakubali kuwatumikia ndio maana nimekuja tena kuwaomba kura munichague.”

Alibainisha hata madini ya Tanzanite ni miongoni mwa rasilimali zinazoipaisha juu Tanzania pamoja na mwambao wa bahari wenye urefu wa kilomita 1422 kutoka Moa hadi Msimbati.

Aliweka wazi kua Tanzania ni  matajiri ndiyo maana Serikali ya Awamu ya Tano imetekeleza miradi mikubwa bila kutegemea misaada kutoka kwa wafadhili.

“Tumetoa Sh Trilioni 1.09 kwa ajili ya elimu bila malipo, tumeongeza kiango cha kukusanya mpato kwa mwezi kutoka Sh Bil 850 hadi Trilioni 1.5. tumejenga vituo vya afya 487, zahanati 1,198 na tumesambaza umeme katika vijiji 9700 wakati tukiingia madarakani vijiji vilivyokuwa na umeme vilikuwa 2018 pekee,” alisema Dk. Magufuli na kuongeza kuwa barabara za kilomita 3500 zimewekwa lami na nyingine kilimota 2500 zitawekwa katika miaka mkitano ijayo.

“Tanzania ni miongoni mwa nchi tano ambazo uchumi wake unakua  kwa kasi Afrika,hili ni jambo kubwa  watanzania tuendelee Kuchapa kazi ili uchumi uendelee  kukua na kuimarika kwa manufaa ya watanzania,” aliweka wazi na kuongeza:

“Benki  ya Dunia ilitabiri Tanzania itaingia katika uchumi wa kati mwaka 2100 huko,tumeingia uchumi wa kati mwaka  2020,wanatushangaa kwa sababu sisi tunafanya makubwa, tunataka na sisi tuanze kutoa misaada  Ulaya.”Aidha, alikitaja kiwanda cha Karanga kilichopo mkoani humo kuwa kutaweza kuzalisha viatu milioni 1.2 pamoja na mikoba na mikanda ya ngozi. Ndiyo maana serikali iliamua kujenga mitambo ya kuzalisha umeme wa Megawati 2115 ili kuimarisha sekta ya viwanda

“Miradi ya umeme yote inayoendelea itakapokamilika bei ya umeme itashuka ili kusudi viwanda viendelee  kuzalisha kwa wingi  bidhaa  mbalimbali na watanzania waweze kuendelea kunufaika,tuchagueni  tuwafanyie hayo,” alisema Dk. John Magufuli.

Katika hatua nyingine, kwa upekee ameutaja Mkoa wa Kilimanjaro una fursa nyingi za ajira ndiyo maana kuna miradi mikuba imefanyika ili kuongeza ufanisi.

Miongoni mwa miradi hiyo ni kuifufua reli ya Kaskazini iliyokufa kwa zaidi ya miaka 30 kuanzia Dar es Salaam, Tanga, Kilimanjaro hadi Arusha ambayo kwa kiasi kikubwa itawasaidia wafanyabiashara wanaosafirisha mizigo yao kwa gharama kubwa sasa.

“Tumetumia jumla ya Sh Bil 4.5 kupeleka mashine za kisasa hospitali ya KCMC ikiwemo X-Ray na CT-Scan. Pia tumepeleka fedha kuimarisha kitengo cha saratani hospitalini hapo ili kuwapunguzia adha wananchi kusafiri hadi Dar es Salaam kufuata matibabu,” alisema Dk. Magufuli na kuweka wazi:
“Vilevile tumepeleka Bil 6.67 kwa ajili ya jengo la mama na mtoto Hospitali ya Mawenzi, tumepeleka Bil 14.33 Hospitali ya magonjwa ambukizi Kibon’goto. Tumejenga hospitali za Wilaya ya Rombo na Siha pamoja na kukarabati hospitali za wilaya za Mwanga, Same na Hai.

“Tumejenga pia vituo vya afya 13 na zahanati 13, tunafanya haya yote ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya lakini pia kuweka mazingira rahisi ya kutoa bima ya afya kwa wananchi wote milioni 60 nchi nzima. Kwa sababu huwezi kuzungumzia masuala ya bima ikiwa huna mikakati imara katika sekta ya afya ikiwemo majengo, dawa na vifaa tiba. Alisema, anajua fedha zitapatikana wapi kwa kuwa mipango ipo imara.”

Aidha, alisisitia suala la amani katika kipindi hiki cha uchaguzi kwa kuwaomba viongozi wa dini waendelee kuliombea taifa ili tuvuke salama kwenye mtihani mzito wa wanasiasa wasioitakia mema nchi.

“Niwaombe viongozi wa dini  muendelee kuliweka hili taifa katika kipindi hiki ili tuendelee  kuwa na amani ambayo ni tunu kubwa ,kuna maisha baada ya uchaguzi, watanzania tudumishe amani,” alisema Dk. Magufuli.

Katika hatua nyingine mgombea huyo urais wa CCM alisema, baadhi ya wagombea urais kupitia vyama vingine vya siasa wameanza kulumbana wenyewe kwa wenyewe kutokana na uroho wa madaraka lakini kubwa zaidi ni baadhi ya wagombea kuwa na nia mbaya na amani ya nchi kwa kuhamasisha wananchi kuingia mitaani kupinga matokeo baada ya kutangazwa.

“Mungu analipa hapa hapa duniani, wenzetu wameana kugombana wenyewe kwa wenyewe wanataka madaraka, Mungu wetu analipa mapema,” alisema.

Baada ya kumaliza mkutano wa Moshi Mjini, Dk. Magufuli leo Alhamisi atakuwa na mkutano Wilaya ya Hai kabla ya kuendelea na mikoa mingine ya kanda hiyo ikiwemo Arusha na Manyara kabla ya kumalizia Mkoa wa Dodoma ambako atapiga kura Oktoba 28, mwaka huu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here