Kaze aahidi kumbakiza Shikalo, Yanga

0

NA MWANDISHI WETU

KOCHA Mkuu wa Yanga, Mrundi, Cedric Kaze, ametaja sababu za kipa wake Mkenya Farouk Shikalo kuwekwa benchi na Metacha Mnata huku akiahidi kumbakisha ndani ya kikosi.

Hiyo imekuja siku chache tangu kuwepo tetesi za kipa huyo kutemwa na kocha huyo katika usajili wa dirisha dogo lililofunguliwa Desemba 16.

Shikalo ameonekana kutopata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo tangu kuanza kwa msimu huu huku Metacha akipata nafasi ya kukaa mara nyingi golini akidaka michezo 15 huku akiwa hajaruhusu bao golini kwake katika mechi 10.

 Kaze ametaja sababu ya kwanza ni majeraha aliyoyapata mwanzoni mwa msimu ambayo yalitoa nafasi kwa Metacha kuonyesha kiwango chake akiwa golini akiipambania timu yake.

Kaze amesema kuwa kipa huyo ana kiwango kikubwa cha kudaka, lakini ushindani anaoupata kutoka kwa Metacha, ndiyo sababu ya pili ya kumuweka benchi kipa huyo aliyewahi kuidakia timu ya taifa ya Kenya

Aliongeza kuwa hana mpango wa kumuacha kipa huyo katika usajili wa dirisha dogo kutokana na kiwango kikubwa alichonacho, licha ya kukosa nafasi ya kudaka katika michezo 15 iliyopita ya Ligi Kuu Bara.

“Shikalo bado ataendelea kuwepo kwenye timu yetu ya Yanga, kwani bado msaada wake unahitajika katika kikosi changu kilichopanga kuchukua ubingwa msimu huu, hiyo ni kutokana na kiwango chake kikubwa alichonacho.

“Shikalo ni kipa mwenye uzoefu mkubwa na pia ni kipa anayeweza kuwachezesha wachezaji wenzake katika mechi, hivyo ni ngumu kumuacha kipa wa aina hii katika timu yangu yenye malengo.

“Kikubwa majeraha ndiyo yaliyomsababishia akapoteza nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza, mwanzoni mwa msimu Shikalo alipata majeraha hivyo akasababisha kupoteza namba katika timu, kwani baada ya kuumia kwake Metacha akaitumia nafasi hiyo kuonyesha kiwango kikubwa na kupata nafasi ya kudumu,” amesema Kaze.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here