Bethsheba Wambura, Dar es Salaam
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imesema Kata nne hazijafanya uchaguzi wa Madiwani kutoka na sababu mbalimbali ikiwamo wagombea kufariki na nyingine karatasi za kura kukosewa.
Kata hizo ambazo hazifanya uchaguzi ni Igumbilo (Iringa), Kisingia (Kilolo) na Nyahanga (Kahama) na Kibosho Kati (Moshi).
Akieleza sababu za kata hizo kutofanya uchaguzi Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu Stemistocles Kaijage amesema kata za Igumbilo, Kisingia na Nyahanga zoezi la uchaguzi halijafanyika kutokana na wagombea wa udiwani kufariki na huku Kata ya Kibosho Kati haujafanyika kutokana na karatasi za kura kukosewa.
“Pamoja na sababu hizo lakini ikumbukwe uchaguzi wa Urais na wabunge katika kata hizo unafanyika kama ilivyopangwa. Na uchaguzi wa udiwani utafanyika mara tu NEC itakapotangaza tarehe ya kufanyika zoezi hilo chini ya kanuni na sheria za uchaguzi wa Serikali za Mitaa.” amesema Jaji Kaijage