Karatu Iwe mvua iwe jua ni Magufuli

0

Na Hafidh Kido, Karatu

WANANCHI katika Wilaya ya Karatu mkoani Arusha wametoa madukuduku yao juu ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano ulivyofanikiwa kufuta makosa ya upinzani uliodumu kwa miaka 25.

Wameeleza, kazi kubwa iliyofanywa na Dk. John Magufuli kwa nafasi yake ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa miaka mitano imeleta mabadiliko makubwa kwa wakazi wa wilaya hiyo.

Jonathan Roito alisema: “Mimi ni mkulima wa vitunguu, kwa miaka mingi tumekuwa na malalamiko ya ubovu wa barabara pamoja na mazingira mazuri ya kuuza mazao yetu hasa suala la ushuru kuwa mkubwa. Lakini ndani ya miaka mitano ya baba huyu ‘Dk. Magufuli’ kuna mambo mengi yamebadilika, sasa naachaje kumpa kura yangu ya ndio.”

Kwa upande wake mfanyabishara ya chakula maarufu mama lishe, Bibi Agusta Juma aliyekuwa anauza matunda na vinywaji katika uwanja wa Mnadani ambako ulifanyika mkutano wa kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndani ya wilaya hiyo jana, alisema kwa sasa kitendo cha kupewa vitambulisho vya ujasiriamali kumewasaidia kwa kiasi kikubwa kuondokana na umasikini.

“Mimi leo nisingepata jeuri ya kuja kuuza bidhaa zangu katika mkutano wa rais (Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Magufuli), ni kwa sababu yake ndiyo nipo hapa kwa kuwa awali tulifukuzwa na mgambo. Si haya tu lakini yapo mengi tuliyofanyiwa ambayo shukurani yetu ni kuwapa kura wagombea wote wa chama hiki (CCM),” alisema.

Aidha, Dk. Magufuli ambaye amekuwepo katika Mkoa wa Arusha kwa siku ya pili sasa, alisema anafahamu changamoto zilizopo katika mkoa na Arusha na wilaya hiyo ya Karatu, lakini wakimchagua Daniel Awack mgombea ubunge wa Jimbo la Karatu ili awaletee maendeleo.

“Nitahakikisha ninaibeba Karatu kwa mikono yote miwili, tulianza na kujenga wodi mbili katika Kituo cha Afya cha Karatu kujenga, tumejenga Zahanati na tumeongeza bajeti ya dawa kutoka Sh Milioni 131 hadi Mil 450,” alisema Dk. Magufuli na kuongeza:

“Tumeleta jumla ya Bil 7.4 kugharamia elimu ya msingi hadi sekondari. Pia tumesambaza umeme katika vijiji 47 ambapo vimebaki vijiji 10 pekee. Mkituchagua  miaka mingine mitano vijiji kumi vilivyobakia vyote vitapata umeme,ahadi zetu ni za kweli ndugu zangu wanakaratu,haya yatatekelezwa kweli.”

Akizungumzia maana ya upinzani katika siasa, Dk. Magufuli alimtaja mwanasiasa mkongwe Dk. Wilbrod Slaa ambapo alisema yeye ndiye alitimiza lengo la kuanzishwa vyama vingi mwaka 1992 ambalo ni kuhakikisha kunakuwa na mawazo mbadala.

“Dk. Wilbroad Slaa alikuwa mpinzani mwenye hoja zenye mashiko na ndio maana nilimpa ubalozi na tena anawakilisha Tanzania katika nchi tisa ,wengine wanawakilisha nchi moja au mbili au tatu,yeye ni tisa.Kwa hiyo kuna wapinzani wazuri,” alisema Dk. Magufuli.

Alisema, Dk. Slaa apoingia bungeni alikuwa mtu wa kujenga hoja na kuelezea matatizo ya wananchi na kuchagua maneno ya kuzungumza hata wabunge wa CCM akiwemo yeye Dk. Magufuli walimpenda.

“Baadaye alipoona ubabaishaji katika upinzani akaamua kutoka. Nami kwa kuona uzalendo wake wa kweli nikamteua kuwa balozi. Yeye ndio alikuwa akinisumbua kwa ujenzi wa barabara hii ya kutoka Karatu kwenda Ngorongoro,” alisema.

Katika hatua nyingine Dk. Magufuli alimuombea kura mgombea ubunge katika Jimbo la Karatu, Daniel Awack kwa kuwataka wananchi waache kumzungumzia vibaya kwa sababu anao uwezo wa kuwavusha walipo.

“Mnasema mgombea ubunge wa hapa hana shahada ya chuo kikuu, lakini je nyinyi watu wa Karatu nyote mna shahada,” alihoji Dk. Magufuli na kuongeza: “Nataka mbunge atakayeteliuwa awe kiunganishi cha watu.

Tunachagua kiongozi atakayekuwa mchapakazi. Karatu tunahitaji maendeleo tusiwe na watu wababaishaji.

Kueleza shida za watu mpaka uwe na shahada?”

Alibainisha, maendeleo hayana chama lakini yanahitaji ilani nzuri inayotekelezeka. Ndiyo maana CCM wanayo ilani yenye kurasa 303 yenye mambo mazuri kwa ajili ya wananchi.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here