Kamati ya Olimpiki Afrika na TOC kujenga kituo cha Kimataifa cha michezo singida

0
Rais wa Kamati ya Olimpiki Afrika,Gulamu Rashid (wa kwanza kutoka kushoto) na Katibu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania(TOC), Filbert Bayi (wa pili kutoka kushoto) wakisaini makubaliano ya eneo la kujenga kituo cha kimataifa cha michezo kinachotarajiwa kujengwa kata ya Marya,katika Halmashauri ya wilaya ya Singida.

NA JUMBE ISMAILLY, SINGIDA 

KAMATI ya Olimpiki Afrika kwa kushirikiana na Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) wamesaini makubaliano ya kujenga kituo cha kimataifa cha michezo kwenye eneo la Kijiji cha Sagarumba,wilaya ya Singida.

Akisaini makubaliano hayo kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya ya Singida,Raisi wa Kamati ya Olimpiki Afrika,Gulamu Rashid alisema ujenzi wa kituo hicho utakapokamilika utakuwa na viwanja vya ndani,Hosteli,riadha,basketball,netball pamoja na viwanja vya michezo ya watoto wadogo.

“Kwa hivyo tunaamini kabisa kwamba katika mwendelezo wa shughuli hizi tutafanikiwa katika kuhakikisha kwamba tutajenga kituo na tunaita “Sports Complex”kituo chenye michezo mingi kwa pamoja.”alisisitiza Rashid.

Kwa mujibu wa Rais huyo katika kipindi cha miaka takribani 14 iliyopita,kituo kama hicho kinachotarajiwa kujengwa Mkoani Singida,kilitarajiwa kujengwa Kibaha au Bagamoyo lakini kwa bahati mbaya katika ziara zao wakiwa pamoja na wanaoshughulika na shughuli za ujenzi,hawakuweza kupata kiwanja.

Aliweka bayana Rashid kwamba badala yake bahati hiyo ya ujenzi wa kituo kama hicho ilikwenda nchini Zambia na Tanzania walilazimika kuikosa bahati hiyo kutokana na kutokuwa na eneo la kujenga kituo hicho.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Singida,Dkt Rehema Nchimbi akimkaribisha kuongea,Rais wa Kamati ya Olimpiki Afrika alisema kwamba kituo hicho pamoja na kufanyika kwa michezo mbali mbali,lakini pia kitakuwa ni kituo cha mafunzo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Singida,Elia Digha aliweka bayana kuwa eneo hilo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho cha kimataifa lipo katika Kata ya Merya,tarafa ya Ilongero,wilaya ya Singida.

Kituo cha Kimataifa cha Michezo chenye ukubwa wa hekari 29 kinatarajia kujengwa katika Kijiji cha Sagarumba,Kata ya Merya wilayani Singida.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here