Kagere, Kahata waomba kuondoka Simba

0

NA MWANDISHI WETU

KUNA tetesi kuwa Francis Kahata raia wa Kenya na mshambuliaji wa timu hiyo, Meddie Kagere raia wa Rwanda, hawana mpango wa kuendelea kuongeza mikataba ya kubaki ndani ya kikosi hicho huku kocha mkuu wa timu hiyo, Mbelgiji, Sven Vandenbroeck akitajwa kuwa chanzo cha wachezaji hao kuamua hivyo.

Kahata msimu uliopita alijiunga na Simba kwa mkataba wa miaka miwili ambapo huu ni msimu wake wa mwisho wakati Kagere alijiunga na Simba mwaka 2018 akitokea Gor Mahia ya Kenya kabla ya kuongeza mkataba unaofikia ukingoni mwishoni mwa msimu huu.

Taarifa kutoka ndani ya timu hiyo zinadai kuwa wachezaji hao hawana furaha kutokana na kocha huyo kushindwa kuwapa muda wa kucheza kadiri muda unavyokwenda licha ya kuwa wapo fiti hali inayopelekea wao kugomea kuongeza mikataba mipya iwapo kocha huyo ataendelea kuwepo.

Mtoa taarifa huyo alienda mbali kwa kusema kuwa hata kuondoka kwa Sharaf Eldin Shiboub raia wa Sudan kumechochewa na kocha huyo kushindwa kumpa nafasi ya kucheza.

Kwa sasa vita hiyo, imegeukia kwa mshambuliaji mzawa, Charles Ilanfya anayedaiwa kuomba kutolewa kwa mkopo katika dirisha dogo linalotarajiwa kufunguliwa Desemba 15, mwaka huu.

“Kahata na Kagere wao walishasema hawataki kuendelea kubakia kucheza Simba kutokana na hali inavyokwenda kwa sababu mwalimu anaonekana kuwa tatizo kwao, hakuna ambaye yupo tayari hata ikiwa uongozi watahitaji wafanye hivyo.

“Hakuna anayeumwa kati yao isipokuwa mwalimu mwenyewe ndiyo hataki kuwatumia na hawajui kwa nini, hivyo kwa kuwa mikataba ipo ukingoni hawaoni haja tena ya kubakia.

“Kuondoka kwa Shiboub mwalimu wanadai amechangia lakini hata kwa sasa upande wa Ilanfya ambaye pia hamtaki licha ya kuwa alimsajili mwenyewe,” alisema mtoa taarifa kutoka ndani ya timu hiyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here