Kafanyeni Maamuzi :Rais Magufuli

0

NA MWANDISHI WETU

RAIS Dk. John Magufuli amewataka Mawaziri na Manaibu Waziri aliowateua kufanya maamuzi kwaajili ya maslahi ya Taifa yatakayosaidia kuondoa shida za wanyonge.

Aliyasema hayo jana jijini Dodoma mara baada ya kuwaapisha Mawaziri 21 wanaounda Baraza la Mawaziri na Manaibu wao 23.

Alisema licha ya kupata wakati mgumu kuwateua kutokana na wingi wa wabunge wa Chama chake lakini wamezingatia uzoefu na mgawanyiko wa kijografia.

“Tuna mikoa zaidi ya 20 lakini tusingeweza kuwa na mawaziri zaidi ya 26 lakini tumezingatia uwezo na maeneo husika.

“Nawaomba mawaziri na naibu mawaziri mkafanye maamuzi, ni nafuu ukafanye uamuzi mbaya kuliko kutokufanya uamuzi kwa sababu tatizo letu jingine tulilonalo unashindwa kutoa uamuzi kwa sababu hutaki uonekane mbaya,” alisema na kusisitiza;

“Kafanyeni  uamuzi hasa unaohusu maslahi ya Taifa, uamuzi utakaosaidia kuondoa shida ya wanyonge waliopo vijijini na mimi naamini nimechagua watu wote watakaokwenda kufanya maamuzi.”

Hata hivyo aliwapongeza na kuwaomba kujituma kwani kazi waliyopewa na mjukumu si mepesi hivyo wakamtangulize Mungu kwani watanzania wana matumaini makubwa.

“Nasema ndugu zangu mkafanye kazi kweli.”

Alisema pia wamechanganya Mawaziri kwa kuzingatia umri na uzoefu katika uteuzi wao na kuwaweka wazee akiwemo Nkuchika kwaajili ya kutoa ushauri.

“Si kwamba ninyi ni wazuri sana kuna vidosari vingine mahali lakini tunajua mtavirekebisha kwasababu yaliyopita si ndwele tugange yajayo”

Alisema ana matumaini watakwenda kutekeleza majukumu yao kikamilifu, “Makamu wa Rais kasema msikae sana ofisi katatueni kero za watanzania kama ni maji watanzania wapate maji.”

Aidha aliwataka washirikiane “kuna mahali nimewahi kuwa Naibu Waziri saa zingine Mawaziri hamuwapangii kazi Manaibu Waziri wanakuwepo ofisi tu mnamonopolize kila kitu na nyinyi msiogope kufanya kazi, mkiogopa hamtaonekana.”

Hata hivyo alisema hataki ule mwonekano wa kisasa “ukifanya kazi utaoneka tu.”

Aidha aliwatahadharisha kuwa makini na njia za mawasiliano wanazotumia hususani za mitandao ya kijamii. “Governmet goes on paper. Hii teknolojia mpya ni nzuri lakini mwangalie mnatumia mahali gani.”

“Na hii sizungumzii tu Mawaziri niwaombe kwenye serikali tufanye kazi yetu kwa uadilifu mkubwa si kila kitu cha kupeleka kwenye makundi.”

MKURUGENZI KUFUKUZWA

Rais Magufuli alisema haridhishwi na usimamizi wa matumizi ya fedha katika Halmashauri na kumtaka Waziri wa Tamisemi, Selemani Jaffo kumwachisha kazi Mkurugenzi wa Geita kwa kununua gari la thamani kubwa.

“Tamisemi kuna matumizi mabaya ya fedha Jafo (Suleiman- Waziri wa Tamisemi) umefanya vizuri sana lakini kwenye kudhibiti fedha bado, nimefikiria sana kukurudisha au kutokukurudisha. Hapo nataka kusema ukweli tuelewane hili la matumizi  ni baya. Unakuta mkurugenzi ananunua gari la milioni 400 fedha tumehangaika nazo kuzipata za CSR, wananchi, watoto wanachangishwa unakuta madawa hayatoshi.

“Nataka  kazi yako ya kwanza kwenda kumsimamisha mkurugenzi wa Geita ndio kazi yako ya kwanza ukaanze nayo na utume watu wafanye uchunguzi wa matumizi ya hovyo,” alisema.

Akielezea sifa za kila waziri alisema walimweka mama Ummy Mwalimu ambaye alifanya vizuri wizara ya afya “Tukaona Wizara ya Mazingira ina legalega juzi tumekamata magari yanasomba vyuma chakavu vinaitwa hivyo lakini ni vifaa vya SGR vinapelekwa kutengeneza nondo na wapo watumishi wanahusika wakiwemo polisi Mkuu wa Kituo cha Mlandizi na OCD na nimeagiza waondolewe.”

Kwa upande wa elimu alisema anatamani kuona somo la Historia linakuwa la lazima na ifundishwe historia ya Tanzania “na hiyo ndiyo iasaidia kujenga uzalendo wajue walikotoka vijana hawajui mapambano, reform zilizofanyika.”

Kwenye nishati alisema anataka vijiji 2338 vilivyobaki vikawekewe umeme na kuanza ujenzi wa Njombe wa MW 300 “maamuzi yakafanyike na wewe (Dk. Kalemani) hufanyagi maamuzi ya haraka haraka.”

Kwa upande wa madini alisema bado yanatoroshwa kwenda nchi jirani kutoka Chunya, Mirerani na maeneo mengine na kutaka juhudi ziongezwe zaidi na maeneo yenye madini yaanze kuchimbwa.

Kwa upande wa Wizara ya Katiba alisema kuna sheria nyingi na mambo mengi ya haki wakiwemo watu waliodhulumiwa, “wakina mama wanadhulumiwa miradhi inachukua muda mrefu kufanyiwa uamuzi.”

Wizara ya mawasiliano na teknolojia ya habari alisema anataka ikifanye kazi kwasababu wizara hiyo ndo usalama wa nchi, “watu wanacheza tu wanavyotaka.”

Wizara ya Kilimo alisema anataka kilimo kikainue uchumi “Profesa Mkenda wewe ni mchumi ukashirikiane na Bashe.”

Kwa upande wa Wizara ya Uwekezaji alisema anataka wawekezaji waje wengi wa ndani na wa nje na majibu yapatikane kwa haraka.

MSAMAHA KWA WAFUNGWA

Akizunguzmia kuhusu maadhimisho ya siku ya uhuru Rais Magufuli alitangaza kupunguza adhabu za watu 256 waliohukumiwa kunyongwa na badala yake watumikie kifungo cha maisha jela.

“Leo (jana) ni siku ya uhuru wa Taifa letu kutimiza mika 59 nataka niwapongeze watanzania wote kwa kusheherekaea siku hii muhimu ya ukombizi wa Taifa letu.

“Najua katika kipindi cha miaka mitano mpaka leo nilitakiwa niwe nimenyoika watu 256 waliohukumiwa kunyongwa. Sijanyonga hata mmoja na wale kwa mamlaka niliyopewa nawapunguzia kifungo cha kunyongwa wahukumiwe kifungo cha maisha.”

“Nimeshindwa kuwanyonga naomba mnisamehe kwa hilo. Wizara ya mambo ya ndani mkashughulikie hilo,” alisema

Pia alitangaza kukubali maombi ya Kamishna wa Magereza kupunga adhabu za wafungwa zaidi ya 3000.

“Kuna wafungwa 3316 wapo wenye makosa madogo, wengine wametumikia kifungo kwa muda mrefu kwa mujibu wa maombi yaliyoletwa na kamishana nimekubali wapunguziwe adhabu zao kwa mujibu wa sheria.”alisema.

Wakati akihitimisha aliwataka viongozi wote kuhakikisha wanasimamia uchumi wa nchi “tusimamie yale tunayoyaweza. Tanzania ina miradi mingi sana ukishakuwa unajenga…unatoa elimu bure, mikopo maji maadui zetru hawawezi kufurahi wengine wanajiuliza tunapata wapi fedha.”

“Nchi hii siku moja tukikubali kuchezewa tutakuwa maskini maisha yote kwasababu tuna mali tusikubali mtu akatuingizia udini, ukabila, sisi ni taifa moja,” alisisitiza “Tuchape kazi tulitengeneze Taifa letu”

Aliwashukuru viongozi wa dini “Kwa kutumia ninyi vioongozi wa dini Corona imeondoka. Sifahamu Mungu tulimfanyia nini nendeni mataifa mengine watu wanakufa lakini sisi Tanzania hakuna watu wanaokufa tunatakiwa kumshukuru Mungu na kumtangulia katika mambo yetu.

“Tuendelee kusimama na kumtukuza Mungu kwa mambo makubwa aliyotufanyia.

Kwa upande wake Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan alimshukuru Rais kwa kufanya kazi hiyo kwa umakini mkubwa.

“Kupata safu hii tumeangalia taaluma uwajibikaji katika maeneo mliyotoka na katika siasa na maisha yenu ndani ya jamii tabia hulka na mambo yenu ndani ya jamii tumeyaangalia.,”alisema

Kwa upande wake Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliwataka mawaziri kutimiza wajibu wao “Uteuzi huu lazima mjue tuna jukumu kubwa kwa watanzania.”

“Tumeapa kumsaidia na kumshauri Rais ipasavyo, lakini pia tuna wajibu wa  kuwatumikia watanzania, serikali imejipambanua kuwa ni ya kusema na kutenda.

“Serikali imejinga msingi imara katika matendo tunayoenda kutenda kwa kujenga nidhamu kwa watendaji wote ambao tayari wamejipanga kufanya kazi.

“Moja ya jukumu letu ni kutenda kazi kwa kuwatumikia watanzania, tutakumbushana lakini tujipange vizuri kwani jukumu letu ni kutenda kazi twende tukachape kazi.,” alisistiza Majaliwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here