Kaduguda afafanua kuhusu suala la Kichuya

0

NA MWANDISHI WETU

KAIMU Mwenyekiti wa Simba SC, Mwina Kaduguda, amesema kuwa hadi jana asubuhi alikuwa hajazipata taarifa za Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), kuhusu mchezaji Shiza Kichuya.

Jana Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Namungo FC, Kindamba Namlia, alisema juzi walipokea barua kwa njia ya email ambayo ilieleza kuwa mchezaji huyo hataruhusiwa kutumika ndani ya Klabu ya Namungo kwa kuwa alisajiliwa akiwa na matatizo ya kimkataba na timu yake ya zamani ya Pharco ya Misri.

Kutokana na utata huo, Kidamba aliongeza kuwa Simba SC wanatakiwa walipe faini kwa kosa la kumsajili mchezaji wakati akiwa na mkataba huku wao Namungo wakizuiwa kumtumia mchezaji huyo mpaka fedha hizo zitakapolipwa.

Habari zilieleza kuwa kiasi ambacho Simba inatakiwa kulipa ni Mil. 300 kwa kosa la kumsajili mchezaji ambaye mkataba wake haujaisha na bila kuwasiliana na timu ambayo ilikuwa inammiliki mchezaji.

Akizungumzia suala hilo, Kaduguda, alisema kuwa anatarajia taarifa hiyo itakapomfikia Mtendaji Mkuu wa Simba SC, Barbra Gonzalez, ataifikisha kwenye Bodi ya Wakurugenzi wa timu hiyo.

“Halafu Bodi italidadavua halafu, itajua nini cha kufanya, itatoa maamuzi, basi tutawafahamisha wanachama wetu kama lipo maanake kama ninavyosema CEO akilipata atatuletea sisi viongozi wenzake ili ngazi inayofuata kwa maana Bodi.

“Na kwa utaratibu wetu Bodi ndio ina weza kuwa na maamuzi yanayo husu klabu, sio mtu mmoja mmoja kwa sababu atatuletea tutajadiliana na kuona nini cha kufanya.

“Wakati mwingine mnaweza kuwa hamna makosa mkawaelekeza FIFA yani mkajieleza FIFA halafu wakaona jinsi ya kupitia maamuzi yao, hayo mambo yapo kwenye mpira kwa uzoefu wangu.

“Pengine umeangukiwa na zahama ambayo sio ya kwako na unapotoa maelezo ya kina Yule aliyetoa adhabu akairudia upya ile adhabu hayo yote yapo kwenye mpira kwa uzoefu wangu mimi.

“Kwa hiyo hebu tuwe wavumilivu, Barbra Gonzalez CEO wetu yuko makini atalileta kwenye Bodi halafu tutalijadili kwa pamoja tuna vichwa 17 pale ambavyo vyote vinafanya kazi vizuri haliwezi kukosekana jibu la msingi kwa manufaa ya Simba SC.

“Hillo ndio naweza kukwambia vinginevyo mimi ndio naipata tarifa hii kutoka kwako mwandishi.

Shiza Kichuya

Kwa mujibu wa uongozi wa Namungo, barua hiyo ambayo walitumiwa na FIFA kuhusu mchezaji wao Shiza Kichuya kuna uwezekano wa Klabu ya Simba kufungiwa kufanya usajili kwa muda wa miaka mitatu ikiwa hawatatimiza vigezo vilivyopo kwenye barua hiyo.

Kichuya ambaye kwa sasa anacheza ndani ya Namungo FC ambayo jana ilikuwa na mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Biashara United alisajiliwa akiwa ni mchezaji huru baada ya Simba kumuweka kando mkataba wake wa miezi sita ulipokwishwa.

Kichuya kwa msimu wa 2019/20 alipotua ndani ya Simba bado hakuwa na nafasi kikosi cha kwanza chini ya Sven Vandenbroeck na walisajiliwa kwa wakati mmoja na Luis Miquissone zama za Mtendaji Mkuu, Senzo Mbatha ambaye kwa sasa yupo Yanga.

Luis bado anaendelea maisha yake ndani ya Simba huku Kichuya akiendelea na maisha yake ndani ya Namungo ambayo inashiriki Kombe la Shirikisho.

Namlia alisema:”Sisi tulimsajili akiwa mchezaji huru hivyo bado kuna vitu ambavyo havipo sawa kwa kuwa ni wenye mamlaka wamesema basi tuna kazi ya kufuatilia na kukaa chini kujua kwa sababu haya ni masuala ya sheria.

“Hatukukurupuka kufanya usajili hivyo inabidi ujiulize kwa nini tulipata kibali cha kumtumia, kwa kuwa ni mamlaka basi tutafuata utaratibu ila tutaumia kumkosa Kichuya kwa sababu tayari alishaingia kwenye mfumo,” .

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here