EAC yajivunia Mradi wa Ujenzi wa Bwawa la kuzalisha umeme la Julius Nyerere

0

Na Mwandishi Wetu 

Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), imeeleza jinsi inavyojivunia na mradi wa ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme la Julius Nyerere ambalo baada ya kukamilika kwake hapo Juni 2022 linatarajiwa kuzalisha Megawati 2115 za umeme.

Haya yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya Jumuiya hiyo anayeshughulikia masuala ya Mipango, Miundombinu, Fedha na Utawala Mhandisi Steven Mlote alipotembelea mradi huo ambao kwa ndio mradi pekee mkubwa wa umeme kwa sasa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Mradi  huu sio tu ni muhimu kwa Tanzania bali utazinufaisha pia nchi wanachama za Jumuiya ya Afrika Mashariki na nchi zingine jirani. Mhandisi Mlote pia ameeleza kuridhishwa kwake na ushiriki wa Watanzania katika katika ujenzi wa mradi huo, ambapo kati ya Wafanyakazi zaidi ya 5000, asilimia 90 ni Watanzania,” alisema.

Mhandisi Mlote ameonesha furaha yake baada ya kuelezwa kuwa mradi huo mkubwa Afrika Mashariki kwa sasa unafadhiliwa na Serikali ya Jamhuri  ya Muungano wa Tanzania kwa asilimi 100, chini ya Uongozi wa Rais Dk. John  Magufuli.

“Nitoe wito kwa Watanzania hasa ambao wanazunguka eneo la mradi kwa kutunza mazingira ili kuufanya mradi huo kuendelea kuwa katika mazingira mazuri na salama wakati wote,” alisema Mlote.

Awali ujumbe huo wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki umetembelea mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kwa lengo la kijionea maendeleo ya ujenzi wa maradi huo na kueleza kufurahishwa na kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya Tanzania, vilevile ametumia fursa hiyo kuwasihi vijana wa Kitanzania waliopata fursa ya ujenzi wa reli kuendelea kujifunza kwa moyo na kwa kujituma ili kupata maarifa na ujuzi wa kuendelea kutunza, kuendesha na kuendeleza miradi hata baada ya wataalmu kutoka makampuni yanayohusika na ujenzi kuondoka nchini.

Aidha Mhandisi Mlote ameeleza kujivunia na miradi mikubwa na ya kimkakati inayotekelezwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwamba kukamilika kwake kutachochea ukuaji wa uchumi na biashara katika Jumuiya hiyo pia kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here