>>Ni fedha zilizotolewa ndani ya miaka kumi
>>Miradi yakamilika kwa zaidi ya asilimia 70
NA MWANDISHI WETU,DODOMA
TANZANIA ni miongoni mwa nchi zilizopo Afrika Mashariki ambazo zina vijana wana vipaji pamoja na ubunifu wa kutengeneza vitu mbalimbali vinavyotumika katika jamii na kuongeza tija.
Pamoja na uwepo wa kundi ubwa la watu hasa vijana kubuni vitu mbalimbali lakini wengi wao wamekuwa wakishindwa kuendeleza vipaji vyao kutokana na kutokuwa na mitaji pamoja na kukosa ufadhili kutoka sehemu mbalimbali.
Mitaji ama ufadhili ni muhimu na pia inakwambisha baadhi ya tafiti ama ubunifu kwakuwa zipo ambazo zinahitaji fedha nyingi ili kuweza kuzikamilisha na kuleta tija kwa jamii.
Watu wengi ambao wanafanya ubunifu ambao hauhitaji fedha nyingi ama malighafi za gharama kundi la watu hawa ni rahisi kufanikiwa kuliko wale ambao wanabunifu za kiasi kikubwa za fedha huku wenyewe wakiwa wametoka katika mazingira duni.
Kutokana na umuhimu wa ubunifu na tafiti Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) imesema katika kipindi cha miaka 10 imeweza kutoa zaidi ya Sh bilioni 50 kufadhili miradi ya utafiti na ubunifu mbalimbali ambapo zaidi ya miradi 100 imeishakamilika kwa asilimia 70 ambayo imezidi kuwaongezea kipato watanzania.
Hayo yameelezwa jana jijini Dodoma na Mratibu wa Mafunzo kutoka COSTECH, Merchades Rutechura alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari.
COSTECH iliandaa mafunzo ya siku mbili kwa Waandishi wa Habari wa Mikoa ya Dodoma pamoja na watafiti na kisha kwa siku mbili waandishi wa habari walipata fursa ya kutembelea miradi mbambali pamoja na watafiti katika Kituo cha Utafiti wa Kilimo (Tari Makutupora),Taasisi ya Mifugo (Taliri Kongwa) na (Taliri Mpwapwa).
Rutechura amesema kuanzia mwaka 2010 Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia imetumia zaidi ya shilingi bilioni 50 kufadhili miradi ya utafiti na ubunifu.
“Katika kipindi hicho miradi zaidi 100 imeishafadhiliwa na katika hiyo asilimia 70 imeishakamilika na matokeo yake yamepatikana.Pia tumefadhili ubunifu mbalimbali pamoja na watafiti wachanga na tunafadhili tafiti kutoka katika Taasisi na Vyuo vikuu kwa sasa hivi tuna mashindano ya Kitaifa yanayoitwa Makisatu,” amesema Rutechura.
Akizungumzia ziara amesema sehemu nyingi walizotembelea wamegundua kuna mbegu nyingi za wanyama ambazo zinatakiwa kuwafikia wananchi ambapo amedai kwamba hiyo ni kazi ya waandishi wa habari kuhakikisha zinafika katika jamii ili iweze kutambua.
“Matokeo ya utafiti yanatija kubwa sana kwa jamii kwa mfano baadhi ya sehemu tulizotembelea tumegundua kwamba kuna mbegu nyingi za wanyama kama vile mbuzi na ng’ombe ambazo zipo katika Vyuo vya utafiti na zinatakiwa kuwafikia wananchi.
“Lakini pia tumegundua kuna teknolojia ya malisho ya ngombe na wanyama wengine ambayo ikisambaza kwa wananchi lile tatizo la uhaba wa malisho katika kipindi cha ukame linaweza kumalizwa.
“Lakini tumeona baadhi ya matokeo kama ufugaji wa kuku na namna ya kumpima kuku kama unataka kumuuza muuzaji asiweze kudhulumiwa,”amesema Rutechura.
Amesema lengo la COSTECH ni matokeo hayo yaweze kusaidia katika uchumi wa Taifa na kila kinachofanyika katika Taasisi na Vyuo vikuu kiweze kuwafikia wananchi.
“Lengo kuu la matokeo haya tunataka yasaidie katika uchumi wa Taifa kwa sababu kila tunachofanya katika chuo cha utafiti tungependa kiwafikie wananchi na tunatumia fedha nyingi za Serikali ili zisaidie hizi teknolojia na kurahisisha maisha ya mtanzania,”amesema.
Pia, amewataka watafiti kuweka wazi kazi zao ili waandishi waweze kuwafikia na kuzipeleka katika jamii.
“Wajitahidi kuweka mazingira rafiki hata mwandishi wa habari akikufikia aweze kukipata kile ambacho anakihitaji,”amesema.
Amesema mafunzo hayo ni sehemu ya mafunzo kwa waandishi wa habari na watafiti ambayo yanafanyika nchi nzima ili kusaidia kufikia malengo kufanyika kwa tafiti mbalimbali zinazofanyika nchi nzima kwenye vituo na Taasisi mbalimbali.
Amesema kuwa toka mafunzo hayo yaanze kwenye kanda mbalimbali kumekuwa na ongezeko kubwa la Makala,vipindi na habari za Sayansi, Teknolojia na Ubunifu na hivyo kusaidia jamii kujua ni wapi wanaweza kuzipata ili kuzitumia kwenye shughuli zao mbalimbali za uzalishaji na kuongeza tija