Janga la corona lilivyvoathiri sekta ya burudani

0

NA MWANDISHI WETU

Mwaka 2020 unakumbukwa kama mwaka uliokabiliwa na changamoto si haba.

Sekta mbali mbali za uchumi ziliathirika kutokana na janga la Corona.

Lakini mojawapo sekta iliyoathirika pakubwa ni burudani, hususan baada ya kufungwa kwa migahawa na kumbi za burudani katika juhudi za kudhibiti ugonjwa wa Corona. Lakini kando na hayo, wadau katika sekta hii waliathirika vipi?

Na je, kuna baadhi waliofaulu licha ya hali hiyo ngumu? Mwandishi wa BBC Roncliffe Odit anatathmini washindi na washindwa katika sekta ya burudani mwaka huu wa 2020.

Sauti ya Zuchu ndio sauti inayosikika zaidi katika kumbi za burudani mwaka huu wa 2020. Msanii huyu mpya wa kundi la WCB Wasafi kutoka Tanzania alitambulishwa wakati makali ya Corona yakiwa yameshika kila mahali. Lakini licha ya changamoto hiyo, Zuchu amevuma, ameng’ara, na ameinukia kidedea.

Miezi michache tu baada ya kujulishwa kwa umma, Zuchu alishinda Tuzo za Mwaka huu za AFRIMMA, kama Msanii Bora Mpya wa Afrika.

Akizungumzia ushindi wake, Zuchu amewashukuru sana mashabiki wake, na kutoa shukran za kipekee kwa bosi wake Diamond Platinumz ambaye anasema amechangia pakubwa katika ufanisi wake.

‘Hii tuzo ni yetu mimi na mashabiki zangu na wasichana wote wanaonitazama kama mfano hii ni tuzo yetu. MY FAMILY I love you so much mamangu wewe ndo icon na role model wangu AM BOWING DOWN TO YOU MY QUEEN. TO my management, thank you so much for investing in me, kuwekeza kwangu ikawe mfano wa kuendelea kusapoti wasichana muwaamini kwamba wanaweza sana #WCB4life. Diamond Platnumz the hero of all time, this award goes to you GOAT. NOBODY FIGHTS FOR ME LIKE YOU,’ aliandika Zuchu.

Mwingine aliyeshinda tuzo mwaka huu ni Rais wa kundi la WCB Wasafi Diamond Platinumz aliyeshinda kitengo cha msanii bora wa Afrika Mashariki, na kumrambisha sakafu mtani wake wa jadi Alikiba pia kutoka Tanzania.

Lakini haijakuwa rahisi kwa wasanii wengine msimu huu wa Corona. Kwa mfano mwanamuziki Alicios Theluji ambaye kwa kawaida huishi Nairobi, alijipata Brussels Ubelgiji na akafungiwa na lockdown.

Anasema maisha hayakuwa rahisi.

‘Kwa upande wa mapato, imekuwa ngumu kabisa. Matamasha yamefungiwa kabisa, na sasa hauna kipato. Unatumia kile kidogo ulikuwa umeweka mpaka kinaisha,’ anasema Alicios.

Lakini licha ya changamoto hiyo, Alicios alifanikiwa kuachia nyimbo kadhaa mpya, na hata albamu yake mpya ALFA.

Kumbi za burudani zilifungwa, harusi zikasimamishwa, matamasha yakapigwa marufuku, na maisha ya wanamuziki yakawa magumu kweli.

Lakini hayo yote pia yaliyokeza nafasi ya kujifunza mambo mapya, kama vile biashara ya muziki kwenye mtandao.

Na sasa wasanii, pamoja na mameneja wakajitosa katika mitandao ya kijamii kutangaza kazi zao…

‘Usimamizi wangu uliamua kwamba nita’launch EP yangu kwa mtandao wa YouTube. Mwanzoni tulikuwa tumepang tamasha, lakini wakati huo kwa sababu ya Corona hatungewe,’ anasema Zuchu.

Lakini licha ya baadhi ya wasanii kuendelea na shughuli zao za kisanii, kuna baadhi walisambaratika kabisa.

Aidha kuzimwa kwa matamasha, pamoja na zuio la kutotoka nje usiku katika mataifa mbali mbali kuliathiri kabisa sekta ya muziki.

Na meneja wa wanamuziki kadhaa kutoka Kenya, Agnes Nonsizi anasema hilo ni funzo muhimu kwa wasanii.

‘Kama msanii lazima uwe na kitu kingine ambacho unafanya pembeni ili kufaulu kimuziki, kwa sababu muziki unahitaji pesa nyingi sana. Na pia wanamuziki lazima wajifunze kuweka akiba, ukipata hela, tumia kidogo, weka kidogo,’ anasema Nonsizi.

Kwa ujumla sekta ya burudani iliathirika pakubwa sana na jinamizi la Corona mwaka huu, lakini bado wasanii wamejitahidi kuachia nyimbo mpya, na kuburudisha mashabiki wao.

Lakini kando na Corona, viwango vya sanaa, hususan muziki mwaka huu wa 2020 vimeimarika sana.

Wasanii wengi kutoka ukanda wa Afrika Mashariki na Kati wametumia kipindi hiki cha kufungiwa majumbani kuimarisha usanii wao, na kuacia mistari mizito.

Kama vile kundi la Mbogi Genje kutoka Kenya; vijana wa mtaa wa Kayole jijini Nairobi.

Nyimbo zao kama vile Ngumi Mbwekse, Kidungi na Wamocho, zina mamilioni ya ‘views’ kwenye mtandao wa YouTube, licha ya kwamba baadhi ya watu wamewalaumu kwa kutumia misemo inayohusisha jeuri katika nyimbo zao.

Na wakati tukiukaribisha mwaka wa 2021, bado Diamond amesalia mfalme wa muziki Afrika Mashariki na Kati baada ya kuandikisha rekodi mpya na wimbo wake Waah aliomshirikisha Koffi Olomide.

Wiki mbili tu tangu wimbo huo ulipoachiwa, umepata zaidi ya ‘views’ milioni 16 katika mtandao wa YouTube; hii ni sawa na kusema kila siku wimbo huo unatizamwa mara milioni 1.

Lakini sasa ni upi wimbo mkubwa zaidi wa mwaka 2020?

Jibu liko wazi kabisa; Jerusalema, ushirikiano wake Master KG na Nomcebo kutoka Afrika Kusini.

Tayari wimbo huo umeshinda zaidi ya tuzo 10 za kimataifa, na kutazamwa zaidi ya mara milioni 277 katika mtandao wa YouTube.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here