Jaji Warioba awataka viongozi wa siasa kuungana kulinda amani

0

Jaji Mstaafu Joseph Warioba amewapongeza viongozi wa dini nchini kwa jitihada zao za kudumisha amani na haki nchini na kuwataka viongozi wa siasa bila kujali itikadi za vyama vyao kukaa pamoja na kutafakari namna ya kulinda amani ya nchi.

Aidha Jaji Warioba alisema yapo mambo yanayohitaji kuzingatiwa ili kudumisha hali ya amani.

Akizungumza katika maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Haki za Binadamu, iliyoandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) jana, Jaji Warioba ambaye alishawahi kuwa Waziri Mkuu nchini alisema ipo haja ya kujiuliza masuala yanayowezesha amani.

“Amani ni tunda la haki, penye haki kuna amani lakini bila amani huwezi kuwa na haki za binadamu,” alisema Jaji Warioba na kuongeza kuwa vurugu zinazoleta uvunjifu wa amani zinatokana na shughuli za siasa, jambo ambalo ni changamoto kubwa.

Alisema vyama vya siasa vinatakiwa kufanya tathmini inavyopata wagombea wa nafasi mbalimbali za uchaguzi kwa kuwa ni eneo ambalo linahitaji kufanyiwa maboresho ili haki itendeke na hivyo amani iendelee kutawala.

Alisema kazi ya kuhubiri amani ingepewa viongozi wa siasa kama inavyofanywa na viongozi wa dini nchini, jambo litakalosaidia kuimarisha amani na haki za binadamu kwa kuwa matatizo mengi yanatokana na shughuli za siasa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga alisema katika kuadhimisha siku hiyo wanaendelea kuhamaisha wananchi kupambana na matukio ya ukatili dhidi ya watoto hususani ukatili wa kingono unaosababisha pia ukatili wa kisaikolojia, mimba na ndoa za utotoni.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here