
ABIDJAN, Ivory Coast
Tume ya Uchaguzi ya Ivory Coast imemtangaza Alassane Ouattara kuwa mshindi wa uchaguzi baada ya kupata ushindi wa asilimia 94.27 ya kura zilizopigwa.
Taifa hilo lilifanya uchaguzi Jumamosi iliyopita ambapo Ouatara alikuwa akiwania muhula wa tatu wa kuliongoza Taifa hilo la Afrika Magharibi.
Wakati akimtangaza mshindi wa uchaguzi huo jana, mwenyekiti wa Tume huru ya uchaguzi, Ibrahime Coulibaly-Kuibert alisema Ouattara alipata kura nyingi kuliko wagombea wengine wote.
“Watu waliojitokeza kupiga kura walikuwa asilimia 53.90 na Alassane Ouattara amepata kura milioni 3,031,483 kati ya kura zote zilizopigwa. Hiyo ni sawa na asilimia 94.27. Hiyo inamaanisha Rais mteule wa Jamhuri ni Alassane Ouatara.”
Matokeo hayo ya uchaguzi yanasubiri kuhalalishwa na Baraza la Katiba ya nchi hiyo. Kwa sasa kuna kipindi kifupi cha kusubiri kama kuna changamoto au malalamiko yoyote yatakayojitokeza kuhusu uchaguzi huo.