Huku matokeo yakiendelea kutangazwa,wapinzani washinda majimbo mawili kati ya 220

0

Ni Waandishi Wetu

Wakati wasimamizi wa uchaguzi wakiendelea kutangaza matokeo ya ubunge katika majimbo mbalimbali nchini Tanzania, hadi leo Ijumaa Oktoba 30, 2020  saa 12:30 jioni wapinzani walikuwa wameshinda majimbo mawili kati ya 220.

Jumla ya majimbo yote nchini Tanzania ni 264, hivyo vyama vya upinzani vitalazimika kusubiri matokeo ya majimbo 44 yaliyosalia kuona kama vitaibuka na ushindi huku CCM wakiwa wameweka kibindoni majimbo 218.

Aida Khenan wa Chadema aliibuka mshindi katika jimbo la Nkasi Kaskazini baada ya kupata kura 21,226 na kumshinda mgombea wa CCM, Ally Kessy aliyeshindwa kutetea kiti cha ubunge baada ya kupata kura 19, 972.

Mwingine ni Shemsia Mtamba wa CUF aliyeibuka mshindi katika jimbo la Mtwara Vijijini baada ya kupata kura 26,215 huku Hawa Ghasia wa CCM akipata kura  18,564.

Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi mbunge huyo mteule amesema, “nimefurahi sana. Unajua nilitarajia ushindi kwakuwa niliona ushirikiano niliokuwa nikionyeshwa na wapiga walionichagua, kipaumbele cha kwanza ni kuhakikisha kuwa wananchi wangu wanapata huduma za uzazi salama na elimu bora.”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here