Huduma ya maji na vyoo vya kisasa inavyovutia wanafunzi

0

NA MWANDISHI WETU, LINDI

Mara nyingi baadhi ya shule zimekuwa zikifanya vibaya kitaaluma na sababu mbalimbali zimekuwa zikitolewa ikiwemo utoro pasipokuwekwa bayana umechangiwa na kitu gani.

Baadhi ya wasichana wamekuwa watoro huku wengi wao wakisema hali hiyo  huchangiwa na kutokuwa na mazingira rafiki ya vyoo shuleni hasa wakati wanapokuwa kwenye siku za hedhi.

Hata hivyo katika baadhi ya shule katika halmashauri ya Mtama mkoa wa Lindi wameondokana na changamoto hiyo baada ya kuchimbiwa visima vya maji, kujengewa vyoo vya kisasa vilivyozingatia mahitaji maalumu pamoja na uchimbaji wa visima katika baadhi ya vituo vya afya.

Lengo la mradi huo ni kupunguza au kumaliza magonjwa yanayoenezwa kwa njia ya maji (waterborn diseases) na kutoa huduma nzuri ya maji safi na salama ya kunywa kwa wanafunzi na wagonjwa wanapokuwa kwenye vituo vya afya unaotekelezwa na taasisi ya Heart to Heart kupitia Shirika la Maendeleo la Korea Cooperative Agency (KOICA) kwa ufadhili wa serikali ya  Korea Kusini.

Kulia ni muonekano wa vyoo vinavyotumiwa na wanafunzi wa shule ya msingi Milamba mkoani Lindi, na kushoto ni muonekano wa vyoo vya kisasa vinavyojengwa na Shirika la KOICA kwa kuzingatia mahitaji maalumu.


Shule ya msingi Mtama ni wanufaika ambapo mwanafunzi Arafa Ally anasema kwa sasa hakutakuwa tena na wasichana watoro kwani baadhi ya utoro wao ulisababishwa na kukosekana kwa miundombinu rafiki hasa wakati wa hedhi.

“Kabla ya kupata huduma ya maji tulikuwa tunapata shida kwenda mbali mtoni kuchota maji kwa ajili ya matumizi mbalimbali na wakati mwingine mtu uliokuwa unaona ni bora ukae nyumbani  kwani tulikuwa tunapata shida hasa kwa sisi wasichana tukiwa kwenye hedhi inabidi kukaa nyumbani kwa sababu tukija shule maji hamna,” anasema Arafa

Arafa anasema kwa sasa wanafunzi wa jinsia zote wanafurahia mazingira ya shule kwani uda wote vyoo ni safi lakini wanapata maji ya kunywa na kunawa wakati wowote.

“Sasa tunakuja shuleni tukiwa kwenye siku zetu hata mtu akitaka kuoga anaoga kwa sababu maji yapo na muda wote vyoo ni safi, kabla na baada ya kula tunanawa na maji ya kunywa yanapatikana wakati kuna wengine wakiwa nyumbani hawayapati,”anasema Arafa

Kauli yake inaungwa mkono na mwalimu mkuu Seif Mavele ambapo anasema shule hiyo kupata mradi wa maji umebadili hata muonekano wake kwani tayari wamaeanzisha bustani kufanya iwe na muonekano wa kijani kulinda mazingira.

“Zamani ulikuwa ukija shuleni kwetu huwezi kukutana na bustani kama ambavyo mnaona leo hii kwa sababu maji kulikuwa hamna hivyo haikuwa na mvuto kama ilivyo sasa ambapo kila anayekuja anaona mabadiliko,”anasema Mavele

Hata hivyo shule ya msingi Milamba imeondokana na changamoto ya baadhi ya wanafunzi kujisaidia kwenye choo cha matundu mawili na wengine kujisaidia vichakani kando mwa shule kutokana na vyoo kutojitosheleza.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo Hassan Sefu anasema kabla ya mradi huo hali haikuwa nzuri kwani baadhi ya wanafunzi walilazimika kujisaidia vichakani  lakini pia hawakuwa na huduma ya maji.

“Tumepata matundu manne kwa wasichana na manne kwa wavulana na yamezingatia mahitaji maalumu, kabla ulikuwa unaweza kukutana na vinyesi kando kando ya shule na ilitupa wakati mgumu lakini sasa baada ya mradi huu tatizo litaisha,”anasema Mwalimu Sefu

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Nyundo 1, Oga Oga ambao ni wanafuika wa mradi wa vyoo na kisima anasema awali walikuwa na vyoo hatarishi ambavyo shimo la choo liliambatana na matundu na hivyo shule hiyo kuhesabika kama haina choo pindi walipotembelewa na wakaguzi wa elimu.

Anasema kwa sasa mradi umeshatekelezwa kwa asilimia 90 na kukamilika kwake wataondokana kabisa na changamoto ya vyoo lakini pia vitakidhi uwiano wa wanafunzi na matundu ya choo.

“Tuna wanafunzi 507 , wasichana  231 na wavulana  276 kwa haya matengenezo madogo madogo yaliyobaki yakikamilika suala la vyoo litakuwa historia lakini pia watatuchimbia na kisima hivyo mazingira yake yatakuwa mazuri hata msimu wa kiangazi,”anasema Mwalimu Oga.

Afisa wa mradi wa program ya wash unaolenga kutokomeza magonjwa yanayoenezwa kwa maji kutoka taasisi ya Heart to Heart, Eston Waliha anasema mradi huo ni wa miaka mitatu utagharimu bilioni 2.8 kwa kuchimba visima vya maji kwenye baadhi ya shule, vituo vya afya na ujenzi wa vyoo vya kisasa kwenye baadhi ya shule za msingi katika halmshauri ya Mtama mkoa wa Lindi.

Amesema mradi huo unaofadhiliwa na serikali ya Korea Kusini kupitia shirika shirika la maendeleo la Korea Cooperation Agency (KOICA) watachimba visima 38 kwenye shule na vituo vya afya tisa sambamba na ujenzi wa vyoo vya kisasa kwenye shule 26 za msingi.

“Mradi ulianza Mei mwaka jana na tunategemea utakamilika 2021 na mpaka sasa tayari tumeshaanza kuutekeleza kwenye shule na vituo vya afya na umelenga wanafunzi wa shule za msingi na watoto walio chini ya miaka mitano ambao ndio waathirika wakubwa wa magonjwa yatokanayo na maji,”amesema Wariha

Afisa elimu wilaya ya Mtama, Danstan Ntauka anasema mradi wa kuchimba visima na vyoo kwenye shule kwa kiasi kikubwa utapunguza magonjwa yanayoenezwa kwa maji( waterborn Diseases) kutoa huduma nzuri ya maji safi na salama ya kunywa kwa wanafunzi na jamii zinazoizunguka shule.

Pia, anasema kukosekana kwa miundombinu rafiki ya vyoo huchangia kwa kiasi kikubwa utoro na hata mdondoko wa wanafunzi shuleni huku watoto wenye mahitaji maalumu wakiwa wahanga zaidi.

“Kwa sasa shule zilizonufaika na miradi hiyo zimeondoa kabisa tatizo la uhaba wa maji safi na salama kwa matumizi ya kila siku kama vile unawaji mikono baada ya kutoka chooni, kabla na baada ya kula na baada ya kufanya kazi za mikono,”anasema Ntauka

Mikakati iliyopo

Anasema kwa sasa wanaendelea kuhamasisha jamii na serikali za vijiji kuchangia fedha na nguvu kazi kujenga miundombinu ya vyoo vya kisasa kwa shule zote zenye upungufu.

“Aidha tutatenga bajeti ndani ya halmashauri toka mapato ya ndani kwa ajili ya kujenga kwa awamu matundu ya vyoo kwenye shule zenye upungufu mkubwa na kumalizia maboma  ya vyoo kwenye shule zilizoanzisha miradi ya ujenzi wa vyoo,”anasema Ntauka

Kwa sasa halmashauri ya Mtama ina shule 79 na mahitaji ya matundu ya vyoo ni 1,289, yalipo ni 842 na pungufu ni 447

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here