HOTUBA YA KWANZA YA MWL. NYERERE BAADA YA KUCHAGULIWA KUWA WAZIRI MKUU WA KWANZA WA TANGANYIKA MWAKA 1961

0
NADHANI ni wajibu wangu kusema nanyi tena katika jioni hii ya kwanza, baada ya kushika mzigo wa kuwa Prime Minister (Waziri Mkuu) wenu wa kwanza. Labda mtafikiri kuwa kubadili jina tu kutoka Chief Minister na kuitwa Prime Minister, si jambo la maana sana. Kwa kweli, kubadili jina peke yake si jambo la maana sana. Lakini natumaini kuwa wote mnaelewa, maana ya jambo hili. Lilielezwa vizuri sana wakati wa mkutano wa Machi kwamba kubadili jina huku, kunafuatana na mabadiliko katika utawala wa nchi yetu, ambayo Watanganyika wote tunashahili kujivunia.
Mabadiliko haya ya leo, yamekamilisha serikali yetu ya wananchi, Bwana Gavana, ambaye ametusaidia sana alipokuwa Chairman wa Baraza la Mawaziri la sasa, kuondoka katika Baraza hilo. Tangu sasa, mimi nitasimamia Baraza la Mawaziri ambao wote 11, nimewachagua mimi mwenyewe. Nawaelezeni jambo hili kwa unyenyekevu mkubwa, kwa sababu mimi na wenzangu, ni watumishi wenu ninyi mnaonisikiliza. Tunajua kuwa mnatuamini, nanyi tunawaamini. Na ni ninyi tu mnaotupa nguvu zetu, tunazozihitaji kwa kazi kubwa iliyo mbele yetu.
Kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, na imani mliyonayo juu yetu, tunapata, na tutazidi kupata nguvu za kuendesha serikali yenu. Lakini tunawaomba msisahau, na mara nyingi sana, nimekukumbusheni jambo hili, kwamba serikali haiwezi kufanya kila kitu. Utajiri wa Tanganyika, bado uko ardhini. Hatuanzi na akiba kubwa ya fedha kama Ghana kwa mfano, iliyoanza nayo ilipopata uhuru wake. Hatuna mkononi fedha walizonazo ndugu zetu wa Nigeria. Kwa kweli, elimu yetu iko nyuma zaidi kuliko Kenya na Uganda.
Kwa hiyo, tunaanza bila ya kuwa na wananchi wa kutosha, wenye elimu ya juu, tunayohitaji katika jitihada zetu za kujenga utajiri wa nchi hii. Lakini matatizo haya, hayanitishi mimi, hayawatishi wenzangu, na wala hatuombi kwamba yawatisheni ninyi. Tunayaona kwamba ni jaribio tu. Lakini jaribio hili, na umasikini, si la serikali tu, ni la kila raia wa Tanganyika. Mara nyingi sana, nimesema nanyi juu ya umasikini, ujinga namaradhi, lakini kwa kweli adui yetu mkubwa ni umasikini.
Tukiweza kumshinda adui huyu, tutakuwa tumeweza kupata silaha itakayotuwezesha kuushinda ujinga na maradhi. Lakini ni ninyi tu, tunaoweza kupigana vita vya umasikini.
Namuomba kila raia wa Tanganyika, aape kiapo cha kuwa adui wa umasikini. Amshambulie adui huyo mahali popote atakapoonekana.
Ukiacha pamba yako shambani bila kuichuma, ukiwa na uwezo wa kuongeza shamba lako kwa eka moja, au nusu eka, au hata robo eka, lakini ukaacha kwa uvivu tu.
Ukaacha rutuba ya shamba lako ikaharibiwa, ikiwa shamba lako limejaa magugu na wewe hujishughulishi kuyaondoa, ukiwa unapuuza masharti unayopewa na wataalamu wa kilimo au hujishughulishi kuongeza elimu yako ya kilimo, au ukiwa unazurura tu bila kufanya kazi, ikimtegemea mjomba au shangazi, au Prime Minister wa Tanganyika akufanyie kazi, basi wewe ndugu yangu, si adui wa umasikini.
Wewe si adui wa ujinga, wewe si adui wa maradhi, wewe kwa kweli ni rafiki mkuu wa maadui hao. Wewe ni adui wa Watanganyika wote wanaofanya jitihada yao yote kumshambulia adui huyo.
Ndugu zangu, vita hivi ni vyenu, vita hivi ni vyetu wote na adui yetu ni huyo niliyemtaja. Basi, tusipoteze wakati wetu tukishambulia maadui ambao kwa sasa ni marehemu.
Tusidhani hata kidogo kwamba sifa yetu katika Afrika au sifa yetu katika Dunia nzima, itategemea ukali na ufundi wa matusi tutakayotumia kutukana ukoloni uliokufa au hata ukoloni mpya utakaojaribu kuanzishwa kwa ujanja na hila za watu wasiopenda uhuru wetu.
Sifa yetu, itategemea mambo tutakayofanya kuongeza na kudumisha nguvu zetu ili tuwe na uwezo wa kulinda uhuru wetu wenyewe, na pia kuwasaidia ndugu zetu wengine kupata uhuru wao na kuulinda pia.
Wala tusipoteze wakati wetu katika kugombania vyeo na fahari ya nafsi. Kilichotufikisha hapa leo, kwa upesi hivi na kwa amani hivi, ni umoja wa watu wa Tanganyika.
Ninapoulizwa kwa mfano, ni nini mwezi wa Machi kwa muda wa siku mbili tu, jibu langu ni moja, umoja. Wenzangu na mimi tulikuwa kitu kimoja.
Na tulikuwa kitu kimoja kwa sababu Tanganyika yenyewe ni kitu kimoja. Na vile vile katika mambo yetu yote ya maisha ya taifa letu. Nani asiyejua kwamba msingi wa kufanikiwa kwa TANU, ni umoja wa TANU.
Kadhalika katika vyama vya ushirika au vyama vya wafanyakazi wanachama wake wanaposhikana bega kwa bega, mambo yao yatawaendea vyema.
Wanachama wake wakigombana na kutengana, mambo yao na mambo ya taifa zina yatakwenda tenge. Ndugu zangu, huu si wakati wa kuchezea umoja wetu, tunauhitaji sasa kama tulivyohitaji zamani kwa ajili ya kuinua hali zetu na ndugu zetu.
Lakini umoja hauhitajiwi na Tanganyika peke yake, Afrika nzima tunahitaji umoja. Kama mnavyojua, tunahitaji umoja.
Kama mnavyojua, nilikuwa Ghana na Nigeria, huko nilikutana na ndugu zetu na wote wanatutakia kheri na baraka. Matembezi hayo, yameikumbusha tena uzito wa mzigo huu tulioanza kuubeba. Tutawezaje ndugu zangu kuubeba mzigo huu?
Tunaweza kuubeba kwa kuonyesha mfano tu, mfano wa taifa lenye umoja kamili, lenye nia moja tu, kujenga taifa letu kwa manufaa ya watu wake wote. Kusaidia ndugu zetu wa Afrika, popote walipo, kujenga undugu na mapenzi, baina yetu na binadamu wote.
Ikiwa ndugu zetu katika nchi za jirani wana taabu, na tunajua wanazo taabu nyingi, wajibu wetu ni kutumia umoja wetu kuwasaidia, na kuwaonyesha kwa mfano, jinsi umoja unavyoweza kuwasaidia wao pia. Kila nilikokwenda, nilipokuwa Ghana na Nigeria, nilikumbushwa faida ya umoja.
Ni wajibu wetu kuepukana na vishawishi vyote vya kuuvunja umoja wetu au kuleta utengano baina yetu na majirani zetu. Najua kuwa, uhuru huleta kishawishi cha kutengana na marafiki na majirani ili kuonyesha kwamba tuna nguvu sana, japo tukiwa peke yetu.
Hiki ni kishawishi cha kuepukwa kama ugonjwa, kwa sababu tusipokiepuka, tunaweza tukawadhuru ndugu zetu, na tukiwadhuru wao, nasi pia tunajidhuru. Pana haja gani ndugu zangu, kutumia uhuru wetu kwa kutamba na kujitutumua mbele ya waafrika wenzetu? Hivyo ndivyo mataifa ya kizungu yalivyofanya, na kwa upande wake.
Leo, Ulaya haina umoja. Wazungu wanajuta, na wanafanya kila jitihada kuujenga tena umoja wao. Ni wajibu wetu ndugu zangu kujifunza kwa makosa yao.
Ni wajibu wetu kuchagua yaliyo mazuri, na kuacha yaliyo mabaya. Umoja ni jambo zuri, basi na tuudumishe umoja wetu. Lakini, kujitenga na majirani ni jambo baya, basi na tuliepuke kosa hilo.
Basi ndugu zangu, ndiyo mawazo niliyopata kushirikiana nanyi jioni hii. Kwanza, kazi. Kwani ni kazi peke yake itakayotuondolea umasikini wetu.
Pili, umoja. Kwani bila umoja, hatuna nguvu ya kuendelea na jambo lolote. Tatu, Undugu. Ili uhuru usilete utengano baina yetu na Waafrika wenzetu au binadamu wenzetu. Katika jitihada ya kutimiza shahada hizo, mimi pamoja na wenzangu, tutawatumikieni kwa uwezo wetu wote.
Na kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, tutajitahidi kuwatumikieni bila kujitafutia faida zetu wenyewe au fahari ya cheo. Ndugu zangu, wazee wangu na akina mama, tupeni msaada wenu.
Asanteni kwa kunisikiliza.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here